SERIKALI imewatoa hofu wananchi kwa kuwahakikishia kuwa vitambulisho vya uraia vitatolewa bure kwa Watanzania wote. Msimamo wa Serikali ulitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge.
Amewatahadharisha wananchi akiwataka wasirubuniwe kwa kutoa fedha kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo, na kuwathibitishia kuwa gharama zote zitabebwa na Serikali.

Pinda alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Betty Machangu (CCM). Amesema kuna baadhi ya watendaji wanaoshirikishwa kwenye mchakato wa utoaji wa fomu,  lakini wanawarubuni wananchi watoe fedha ili wapewe fomu za vitambulisho vya uraia. Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kulipinga jambo hilo.

Amesema utoaji wa vitambulisho hivyo ambao kwa sasa uko katika hatua za utekelezaji kwa watumishi wa umma; ni bure kuanzia fomu, upigaji picha hadi uchukuaji wa alama za vidole.

“Wananchi wasikubali, zoezi (shughuli) lote linagharamiwa na Serikali,” amesema Pinda.

Waziri Mkuu ametoa rai kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi ili waweze kusajiliwa, mara maofisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) watakapozuru maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Pinda amesema Serikali itakaa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuangalia taratibu za upigaji kura kwa wapigakura wasiokuwa na vitambulisho, lakini majina yao yapo kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.