Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma
Imeelezwa kuwa tatizo la Sumukuvu nchini Tanzania linachangiwa na ukosefu wa elimu kuanzia uzalishaji wa chakula na kusababisha madhara ya ugonjwa wa saratani na ini.
Hayo yamebainishwa leo Januari 9,2023 mkoani Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula kutoka Wizara ya Kilimo,Dkt.Honest Kessy ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wakati wa mafunzo kwa kwa wahariri wa vyombo vya habari.
“Haya ni mafunzo kwa wahariri ili kuwa na uelewa wa kina wa tatizo la sumukuvu na na athari zake na sumukuvu ambapo tatizo hilo lipo katika mikoa mbalimbali lakini elimu bado ipo chini hivyo kupitia mafunzo haya wananchi watapa elimu kupitia vyombo vya habari,” amesema.
Wizara ya Kilimo kupitia mradi wake wa Kudhibiti Sumukuvu (TANPAC) imewakutanisha wahariri wa vyombo mbalimbali kwa ajili ya kuwapatia semina ya udhibiti wa sumukuvu kwa lengo la kuelimisha jamii ambapo katika tafiti imebainika kuwa kuwepo kwa tatizo kubwa la sumukuvu nchini.
Amesema kuwa mwaka katika utafiti uliofanyika mwaka 2016 ilibainika kuwa wananchi 20 walifariki kutokana na ulaji wa chakula ambacho kilichafuliwa ambapo mazao yalikuwa na sumukuvu.
“Kulikuwa na athari kubwa kwani mwaka 2021 mahindi ya Tanzania yalizuiliwa kuingia Kenya hivyo kusababisha hasara kwa wafanyabiashara na wakulima pia kwa kuathiri uzalishaji hivyo kutokana na tatizo hilo Serikali iliamua kutoa elimu kwa wakulima ya namna ya kuanika mazao kwani sumukuvu huanzia ardhini,” amesema.
Amesema kuwa kupitia mradi huo utasaidia kupunguza athari hizo pia kujenga uelewa na kufahamu athari za sumukuvu.
Mratibu wa Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu, Josephat Clepin amesema tatizo la sumukuvu hapa nchini Tanzania lilianza tangu mwaka 2016 katika Mkoa wa Dodoma.
Amesema Malengo ya mrdai huo ni pamoja na mambo mengine ni kuimarisha usalama wa chakula hapa nchini , kuimarisha uchumi wa nchi kupitia mauzo ya chakula nje ya nchi pamoja na kuimarisha Afya ya jamii.
Aidha Clepin amesema ili kufikia malengo hayo mradi huo unajenga miundombinu ya msingi katika kudhibiti sumukuvu lakini pia umelenga kuimarisha taasisi za udhibiti na utafiti Ili udhibiti wa sumukuvu iwe endelevu.
Kwa upande wake Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria Dkt. Happy Magoha amesema elimu kuhusu usalama wa chakula inatakiwa kutolewa mara kwa mara,ili kuepuka mazao kupata Sumu Kuvu ikiwemo kuepusha madhara kwa jamii.
Amesema elimu hiyo inatakiwa kutolewa kwa jamii mara kwa mara ili kuhakikisha jamii inatambua umuhimu wa kuhifadhi vizuri mazao ili yasipate Sumu Kuvu ambayo ina madhara kwao.