Na Stella Aron,JamhuriMedia
DHAMIRA njema inayooneshwa wazi Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni wazi kuwa itafanikisha kiu ya mchakato wa mabadiliko ya sheria ya huduma za habari nchini.
Hatua hiyo inatokana na wasaidizi wa Rais Samia kuonyesha kwa vitendo na hatua kwa hatua katika kukutana na wadau wa habari kwenye vikao vya pamoja na kujadili mchakato huo.
Akizungumza na JAMHURI DIGITAL, Rais wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Deogratius Nsokolo, anasema kuwa tangu kuanzishwa kwa mchakato kuhusu mwenendo wa mabadiliko ya sheria ya huduma za habari nchini kumekuwa na mafanikio makubwa.
“Kitendo cha viongozi mbalimbali wakiongozwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye tangu aingie madarakani amekuwa ni rafiki wa waandishi wa habari kutokana na kuonyesha nia ya kufanyiwa kwa marekebisho baadhi ya vifungu vya sheria ya huduma ya habari vilivyoonekana kuwa ni mwiba katika sekta ya habari.
“Rais Samia tangu alipoingia madarakani, alikuwa karibu na sekta ya habari na kutoa matumaini ya kufanyiwa marejeo kwa sheria hii ya mwaka 2016. Na tayari matokeo yake ni wadau wa habari na Serikali kukaa kwa pamoja na kuainisha vipengele gani ambayo wangependa viondolewe,” anasema.
Wadau wanataka marekebisho ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni ya kila mwaka na badala ya ufanyike usajili wa mara moja.
Kwa mantiki hiyo, wadau wanapendekeza magazeti yasilazimike kisheria kuhuisha/kujisajili kila mwaka ili yapate leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya kufutwa au kunyimwa lesini kama ambavyo ilishuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambako baadhi ya magazeti yalifutwa na mengine kunyimwa leseni.
Wadau wanajenga hoja kwamba uhakika wa leseni ya muda mrefu utajenga uhakika na kuaminika kwa mazingira ya uwekezaji hivyo kuvutia wawekezaji katika tasnia ya habari nchini.
Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho ya kifungu cha 7 (2) (b) (lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadri itakavyoelekezwa na Serikali, wadau wanakieleza kipengele hiki kuwa kinaingilia uhuru wa uhariri.
Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.
Serikali inasema inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ili wabunge wakiridhia utekelezaji wake ufanyike huku ikihimiza kuwa dhamira yake katika tasnia hiyo ni njema.
Serikali inasema kutokukamilika kwa kwa baadhi ya taratibu ndiyo sababu iliyokwamisha kupeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hiyo bungeni katika Bunge la Novemba mwaka huu.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma anasema Serikali ilitarajia kupeleka mapendekeo hayo, lakini haikufanya hivyo kwa kuepuka mivutano kutoka kwa wadau wa habari.
Waziri Nape anasema Serikali ipo tayari kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari kwa watunga sheria kwani haikuwa vyema kupeleka mapendekezo ya sheria ya huduma za habari bungeni wakati kuna maeneo ambayo wadau wa habari na serikali walikuwa hawajakubaliana.
“Sisi kama Serikali hatujakaa kimya, bado tupo vizuri kwenye mchakato huu. Nia ya serikali mpaka sasa bado ni njema. “Sisi kama tupo happy (tuna furaha) na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya huduma ya habari unavyokwenda, lakini pamoja na yote haya, ni vizuri uhuru uliopo tukautumia vizuri,” anasema.
Waziri huyo anaongeza kuwa: “Pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria kuwa njiani kukamilika, serikali inaangalia pia uhalisia wa mabadiliko hayo ya sheria na mazingira ya sasa. Hata kama kuna mapitio tunayofanya, lakini lazima tuangalie uhalisia wa nchini.”
“Wito wangu, mchakato huo uende kwa kasi ile ile kwa sababu mabadiliko hayo yatawezesha waandishi wa habari kuwa huru zaidi, pia kufanya kazi zao kwa weledi, kwa sababu vile vitu ambavyo tuliviona ni vikwazo, vitakuwa vimeondolewa.
“Mambo hayo yanayokwaza uhuru wa habari yakiondolewa, yatasaidia sana maendeleo ya nchi yetu, kwa sababu habari ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi,” anasema.
Gerson Msigwa, Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), anashauri wanahabari kubaki pamoja kwenye mchakato wa mabadiliko ya sheria ya huduma za habari.
“Tutumie vizuri kipindi hiki ambacho serikali imekuwa tayari kusikiliza. Tubaki pamoja mpaka mwisho,” anasema.
TEF YASEMA KUNA DALILI NJEMA
TEF chini ya mwenyekiti wake Deodatus Balile anasema kuna mwelekeo mzuri kuelekea mabadiliko ya sheria ya habari.
“Serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ambayo ilikuwa nayo tangu mwanzo. Tumemaliza na serikali inaendelea na hatua zake kabla ya kupelekwa bungeni.
“Suala la mabadiliko ya vipengele vya sheria lina mchakato wake, cha msingi serikali imetoa fursa, na si kutoa peke yake, inaendelea kuchukua hatua,” anasema Balile.
Balile anasema mchakato huu unakwenda vizuri sana kwa kuwa, Rais aliyepo madarakani ana dhamira njema na sekta ya habari.
Balile anasema kuwa baada ya wadau wa habari kufanya vikao na serikali, wadau wanasubiri matunda ya vikao hivyo kwa kupelekwa mapendekezo ya wadau wa habari bungeni.
“Katika mchakato huu, tumekuwa tukishiriki kuzungumza na waziri husika ili tukubaliane katika sehemu mbalimbali ya vifungu vya sheria ya habari,” anasema Balile na kuongeza:
“Tulifanya mkutano wa mwisho Novemba ambao tulisema, sasa huu uwe mkutano wa mwisho ili sheria ya huduma za habari ipelekwe bungeni.” anasema.
Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa serikali ni pamoja na mamlaka ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) yapunguzwe; kuundwa kwa chombo ambacho pamoja na mambo mengine kitashughulikia masuala ya ithibati kwa waandishi wa habari, maadili ya uandishi na usuluhishi wa malalamiko dhidi vyombo vya habari na masula ya mafunzo. Chini ya shieria ya MSA mambo haya yametawanyika katika vyombo vinne. Hivyo ni MAELEZO, Baraza Huru la Habari, Bodi ya Ithibati na Mfuko wa Mafunzo.
Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Salehe Mohamed anasema kuwa mchakato wa mabadiliko ya sheria ya huduma za habari, unalenga kupata uhuru wa kihabari na kuondoa sheria zinazovizia wanahabari ili kuwaingiza matatani.
Anasema malengo ya mchakato huo ni kuweka mipaka na malengo ya uhuru wa habari bila kuumiza wengine.
“Mchakato wa mabadiliko haya, unalenga kuweka mipaka, lakini pia uhuru wa habari bila kuumiza mtu yeyote. Tunalenga kupata uhuru zaidi wa habari na wajibu kwa mwanahabari,” alisema na kuongeza:
“Tunapozungumzia uhuru wa vyombo vya habari, sio kwamba tunataka upendeleo kutoka serikalini, la! Tunacholenga hapo kila mmoja apate haki na awajibike.”
Hata hivyo anasema Rais Samia ameonesha nia ya kubadilisha sheria za habari zinazolalamikiwa na kwamba, kinachofuata ni utekelezaji.
Anasema anamshukuru Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kupitia sheria za habari na kuagiza zifanyiwe maboreshio ili kuendana na mazingira yaliyopo.
Anasema hatua ya kwanza ya maombi ya wanahabari ya kuiondoa tasnia ya habari chini ya Wizara ya Michezo na Utamaduni na kuipeleka kwenye Wizara ya Mawasiliano, ilionesha dhamira ya kweli katika kushughulikia matamanio ya wanahabari.
Anasema ingawa wadau wa habari wanasimamia mabadiliko hayo, uhuru wa habari unawahusu hata wale wasio wanahabari.
Kwamba nchi ambayo uhuru wa habari haupo, wananchi hukosa fursa ya kupata taarifa sahihi na hivyo kunyima haki yao ya msingi ya kuhabarika.
“Tufahamu kuwa uhuru wa habari ni haki ya msingi ambayo wengine wanaitaka. Vyombo vya habari visipokuwa huru, wananchi nao pia wanakosa uhuru ikiwa ni pamoja na kutoa maoni yao pia kupata taarifa zinazowahusu moja kwa moja,” anasema.
Tasnia ya habari nchini Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi zinazoathiri moja kwa moja dhima yake ya kuendeleza demokrasia, utawala bora na uwajibikaji.
Katika miaka mitano iliyopita Tanzania ilimetunga sheria kadhaa zinazozuia uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kujieleza, na zinazokazia ukali wa sheria zilizopo ambazo ni vikwazo katika kuhabarisha wananchi. Kwa pamoja, sheria hizi zinajinaisha makosa ya kashfa badala ya kuwa madai, pia ukali wake umesababisha vyombo vingi vya habari kuepuka habari za kiuchunguzi ili kujiweka mbali na makali yake.
Kwa mfano kati yam waka 2016 na 2020 vyombo vingi vya habari viliadhibiwa kwa kutozwa faini, kusimamishwa kwa muda au kufungiwa kabisa kwa kukiuka kanuni za maudhui ya vyombo vya kieletroniki. Magazeti kadhaa yakiwemo Mawio, Mwanahalisi, Raia Mwema na Tanzania Daima yalisitishwa kwa kuchapisha habari zinazokosoa watawala, huku waandishi wakishitakiwa kwa uchochezi na kuchapisha taarifa za uongo.
Mwaka 2017 Serikali ilisitisha utamaduni uliodumu kwa takriban miongo miwili wa kutangaza moja kwa moja shughuli za Bunge kwa kisingizio cha Shirika la Utangazaji la Taifa lisingeweza kumudu gharama za kurusha matangazo hayo.
Hata vyombo binafsi ambavyo vilitaka kurusha matangazo hayo kwa gharama zao, navyo vilikatazwa.
Vikwazo vimewagusa hadi wachapishaji na wasambazaji wa habari mitandaoni, huku mwanzilishi wa mtandao maarufu wa kupashana habari na kufichua maovu wa
Jamii Forums akishitakiwa kwa kukataa kueleza vyanzo vya taarifa anazochapisha.
Vyombo mbalimbali vya habari vimeadhibiwa kwa kutakiwa kulipa faini kubwa kwa
kuchapisha na kusambaza maudhui ya ripoti ya uangalizi wa uchaguzi iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, ambayo ilionesha ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi uliohusisha jeshi la Polisi kwa baadhi ya wagombea.
Madhara ya vitisho hivyo ni pamoja vyombo vya habari kuogopa kuripoti kuhusu shughuli muhimu za asasi za kijamii, hivyo asasi hizo kushindwa kuarifu wadau wake na jamii kwa ujumla juu ya shughuli zao, au kutoa taarifa mbadala wa zile zinazotolewa na upande wa Serikali na taasisi zake.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye vyombo vingi vya habari Afrika Mashariki. Hata hivyo, vyombo vingi kati ya hivyo ni vidogo, havina rasilimali za kutosha, dhaifu na ambavyo waandishi wake wa habari hukutana na changamoto mbalimbali katika kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma.