Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kuwa kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kutangaza rasmi kuruhusu kuanza kufanyika kwa mikutano ya vyama vya siasa nchini kuanzia leo ni cha kufufua tena siasa kwani tayari wananchi walishasahau masuala ya siasa.
Akizungumza katika mahojiano na JAMHURI DIGITAL amesema kuwa Rais Samia ameanza vizuri mwaka 2023 kwani kitendo cha kuruhusu na sisi wana siasa kusimama kwenye majukwaa na kuzungumza changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hii ni kati ya maendeleo ambayo yanakwenda kufanyika.
“Huko nyuma kama mnakumbuka sisi wanasiasa tulikuwa kimya kiasi kwamba wananchi wametusahau lakini hatukuamua sisi ni Serikali ambayo iliamua tukae kimya bila ya kufanya mikutano lakini sasa kifungo hicho kimekwisha.
“Tunapongeza sana rais Samia kwa maamuzi yake haya kwani sasa tutaanza kufanya mikutano yetu kwa amani na usalama kama ambavyo yeye ameahidi kutupa ushirikiano katika suala la ulinzi.
“Kitendo cha kufumbwa mdomo kwa muda mrefu kimechangia siasa kurudi nyuma kwa kuwa hakuna chama chochote wala mwanasiasa aliyekuwa akiruhusiwa kupanda kwenye majukwa na kuanza kunadi sera zake hii ni sawa na kuwa kifungoni bila kupenda,” amesema.
Lipumba ameongeza kuwa hata hivyo Serikali inatakiwa kukaa chini na kuangalia suala la katiba mpya kwa kuwa mchakato wa katiba uliokuwa chini wa Jaji Joseph Walioba unapaswa kuangaliwa kwa makini kwa kuwa ulilenga serikali tatu badala ya serikali mbili.
“Hili suala la katiba mpya linapaswa kuangaliwa kwa mapana zaidi kwani mchakato wa katiba mpya ya Jaji Walioba ulilenga Serikali tatu, wakati kuna serikali mbili hivyo bado haujakaa sawa na inahitaji kutolewa kwa maoni,” amesema.
KAULI YA CHADEMA
Mwenyekiti wa Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freema Mbowe amesema kuwa maamuzi ya rais kuruhusu mikutano ni ya kupongezwa hata hivyo kuna sheria nyingi ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho kwani ni za kukandamiza wananchi.
“Kwanza na nampongeza rais hata hivyo kikatiba ilikuwa ni haki yetu ya msingi kufanyika kwa mikutano ya hadhara lakini tulishindwa kufanya hivyo kutokana na sheria kandamizi ambazo rais ameahidi kuzifanyia marekebisho.
“Kuna mambo yanahitaji muda katika kujadiliana hivyo bado kuna vipengele ambavyo tunaendelea navyo kufanya mazungumzo na Serikali ili kuweka sawa na kuondokana na uonevu.
“Sisi kama CHADEMA tumelipokea hili na tunakwenda nalo kwenye vikao vyetu na kujadiliana kwani bado kuna sheria nyingi kandamizi ambazo zipo kwenye Tume ya Uchaguzi, Vyombo vya Habari,Kuwepo kwa Tume huru ya uchaguzi,taasisi mbalimbali, wasimamizi wa chaguzi hivyo masuala kama haya ambayo ni ya msingi hayahitaji haraka katika kutolewa maamuzi.
“Hata hivyo kwa hatua hii rais imerejesha matumaini kwa Watanzania kwani masuala ya maendeleo yanahitaji ushirikishwaji wa wananchi na si mtu mmoja kujiamulia,’ amesema Mbowe.
KAULI YA ACT-WAZALENDO
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe, amesema kuwa amefarijika sana na hatua ya rais kutangaza kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ambayo kwa muda mrefu ilisimamishwa na bila kufuata sheria.
Zitto amesema kuwa hadi kufikia leo kulikuwa na mazungumzo ambayo yalikuwa yakifanyika kwa njia tofauti tofauti kwa kila chama lakini hivi sasa wote tumekuwa katika njia moja.
“Unajua kilichokuwpeo hapa ni kuwa ACT-WAZALENDO, CHADEMA kila mmoja alikuwa akipita njia yao kutafuta muafaka lakini wote sasa tumekubaliana na kuanza kupita njia moja.
“Kilichotokea leo ni kuwa rais samia amepita katika kiapo chake kwake siku hiyo aliahidi kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi, pia kutatua kero mbalimbali wanazokabiliana nazo wanasiasa hivyo leo ametekeleza ahadi yake kwa vitendo.
“Pia ameanza vizuri mwaka huu wa 2023 kwa kuhakikisha sasa siasa inarudi katika reli kwa maana ya kuendeleza demokrasia hivyo tumefarijika sana kwani sasa maendeleo yatasonga mbele,” amesema.
CHAMA CHA UMMA
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Taifa,Hashim Rungwe amefurahishwa na ruksa ya kufanyika kwa mikutano iliyotolewa na Rais Samia kwani wananchi walishaanza kuwasahau kama kuna wanasiasa hapa nchini.
“Tangu tulipopigwa stop na sheria isiyojulikana ni muda mrefu na tayari wananchi wameshaanza kutusahau kabisa kama kuna wanasiasa hivyo kwa hatua hii wananchi wataanza kurudisha imani kwetu na sisi tutaendelea na ratiba zetu za mikutano ya hadhara,’ amesema Rungwe.
Amesema kuwa chama chake kitazingatia sheria za nchi kwa kufanya mikutano yenye amani na kutumia lugha stahiki kama ambayo Rais Samia amesisitiza katika hotuba yake.
“Chama kitaanza mikitano yake ya hadhara na kitatumia lugha zisizo na ukakasi kwani rais amesisitiza hilo ikiwa ni pamoja na kupewa ulinzi kwani kwa kufanya hivyo sasa tutarudisha imani kwa wananchi ambayo huko nyuma imepotea,” amesema.
Doyo Hassan Doyo ambaye ni katibu Mkuu wa Chama cha ‘Alliance For the Democratic Change’ (ADC), amesema kitendo cha Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuitisha mkutano na vyama vya siasa kinapaswa kupongezwa kwa kuwa kinaimarisha afya katika siasa za hapa nchini.
Akizungumza katika mahojiano na JAMHURI DIGITAL ,Doyo amesema hatua hiyo ya Rais Samia, ni wazi imeonyesha dhamira yake ya kweli kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika siasa hususani kwa vyama vya upinzani na kwamba kwa kuliona hivyo ameona ni vyema kukaa nao pamoja na kuzungumza.
Doyo amesema kuwa hatua ya rais kuruhusu kwa mikutano ya hadhara ni jambo la kupongeza sana kwani sasa wadau wa masuala ya siasa nchini wameona ushirikiano ulipo kati ya Serikali na vyama vya siasa.
“Ukweli binafsi nimefarijika na hatua ya Rais Samia kuitisha mkutano huu mapema kabisa kwa mwaka, na kutoa maamuzi ya kuruhusu kwa mikutanoi ya hadhara sasa Tanzania itakuwa na mipango ya pamoja katika kuleta maendeleo” amesema Doyo.
Amesema wao kama ADC watahakikisha wanatimiza wajibu wao na kwenda kutoa mchango wa mawazo yao pale watakapopewa nafasi, lengo ni kuona hali ya kisiasa nchini inahimarika kama ambavyo imeanza kujionesha hivi karibuni tangu Rais Samia Suluhu Hassan ashike madaraka ya kuongoza nchi.
Akizungumza katika Rais Samia ametoa ruhusa hiyo leo Januari 3,2023 wakati wa kikao kati yake na vyama vya siasa nchini ambao kimefanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba mikutano ya hadhara ni haki ya vyama vya siasa.
“Moja ya jambo ambalo limezungumzwa sana hata kwenye kikosi kazi ambacho nilikiunda kwa ajili ya kufuatilia hali ya kisiasa ni eneo la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.Hivyo uwepo wangu leo mbele yenu nimekuja kutoa ruhusa , kuja kutangaza lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoshwa.
“Vyama vya siasa ni haki kuendesha vyama vya siasa lakini tunawajibu kwa upande wa Serikali tumeshajipanga na wajibu wetu ni kulinda mikutano ya hadhara.Wajibu wa vyama vya siasa ni kufuata wajibu wa kufuata kanuni, niwaombe ndugu zangu tunatoa ruhusa twendeni tufanye siasa za kistaarabu, siasa za kujenga.
“CCM tuaamini kukoselewa na kukosoa, kosoeni, mimi naamini mkinikosoa najua changamoto iko hapa na changamoto niikifanyia kazi na kuitatua basi nitaendelea kuwepo.Ndio maana mimi siwaiti vyama vya upinzani bali ni vyama vinavyotuonesha kasoro,”amesema Rais Samia.
Hata hivyo amewaomba vyama vya siasa kwenda kuonesha siasa za kistaarabu, kufanya siasa siasa zenye kuheshimu mila na desturi.”Samia anaweza kuwa na uvumilivu , Samia anaweza kustahamili lakini chawa wa samia anaweza asistahimili.Vyama vya siasa nendeni mkaseme waliahidi hawajatekeleza.
“Kazi yetu itakuwa ni kutekeleza. Twendeni tukafanye siasa, kama tumekosea haki za binadamu tuambieni,lakini tukitukanana , tukaanza kurusha mashfa nchi haitakalika. Niwaombe ndugu zangu twendeni tufanye siasa, isemeni Serikali na ikosoeni .Ukiamua kupanda jukwaani jizatiti na pale Serikali ambapo imefanya vizuri semeni.
“Najua mtakwenda kusema Serikali ina madeni lakini semeni maedeni yamefanya nini, yanajenga SGR hadi kigoma.Uongo haujengi, bali jengeni hoja, nimekaa na kuzungumza na vyombo vya ulinzi na usalama na vitawalinda lakini tukumbuke hakuna ambaye yuko juu ya Sheri.
Aidha, Rais Samia amevitaka vyama vya siasa kuikosoa na kuishauri Serikali kupitia mikutano ya hadhara kistaarabu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo.
Rais Samia ametangaza maamuzi hayo leo wakati akizungumza na viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa 19 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Serikali imedhamiria kuukwamua mchakato wa kupata Katiba mpya baada ya kukaa na kukubaliana na vyama vya siasa.
Vilevile, Rais Samia amesema hatua hiyo itazingatia hali halisi ya nchi, uwezo wa kiuchumi pamoja na mila na desturi zetu.
Rais Samia ameongeza kuwa Serikali inajiandaa kurekebisha Sheria anuai zikiwemo Sheria za Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa ili kujenga taifa lenye umoja.
Rais Samia amesema ili taifa liwe moja lazima kuwe na maridhiano baina ya vyama vya siasa kwa lengo la kuendesha taifa lenye amani na utulivu kwa maendeleo ya taifa letu.