BAADHI ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wamemwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu, Balozi Ombeni Sefue wakidai kuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe anafanya kazi kwa kutumia majungu anayopelekewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Omar Chambo.

Wanadai kwamba Chambo ametenga fungu kubwa la fedha kwa ajili ya propaganda katika vyombo vya habari na kuyataja magazeti (Jamhuri halimo) kwamba yanatakiwa kuandika chochote anachofanya waziri huyo ili kumpamba, lengo likiwa kumpa umaarufu kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

 

Wanadai kwamba mtu aliyeteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande ni rafiki wa muda mrefu wa Mwakyembe. Mbali na kuiweka pabaya CCM kuelekea mwaka 2015, wafanyakazi hao wanadai kuwa Dk. Mwakyembe huenda anatumiwa na wapinzani nchini, vinginevyo anatumikia kundi la ndani katika chama hicho ili kutaka kidhoofike.

 

Nimewahi kumsifu Dk. Mwakyembe kutokana na utendaji wake mzuri tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Uchukuzi Mei 4, mwaka huu. Imenilazimu kuandika makala nyingine kwa vile ninaamini kuwa tayari ameanza kutengenezewa majungu na vitisho.

 

Katika nchi zote duniani zenye bandari za bahari kama Kenya, Msumbiji, Afrika Kusini, Angola, Ghana, Tunisia, Morocco, Brazil, Argentina, Chile, Panama, Kyuba, Marekani, Canada, Hispania, Indonesia, Australia, New Zealand, Malaysia, Japan, India, Denmark, Finland na kadhalika sehemu kubwa ya uchumi wake unajitegemea. Tanzania ni kinyume.

Kenya inaingiza fedha nyingi za kigeni kutokana na bandari yake ya Mombasa, lakini Tanzania yenye bandari tatu, hainufaiki vya kutosha.

 

Imekuwa na kila aina ya tuhuma za kashfa, ukiwamo wizi wa mizigo inayotoka nje ya nchi. Magari yanaibwa vifaa mbalimbali, zikiwamo radio. Hali hiyo imesababisha wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Zambia na Malawi kuhamia bandari za mataifa mengine.

 

Wamekimbia kwa sababu ni ujinga kung’ang’ania bandari iliyokithiri kwa wizi huku zipo nyingine ambazo hazina tatizo hilo wala ucheleweshaji wa mizigo kama ilivyo ya Dar es Salaam. Hilo Dk. Mwakyembe tayari ameliona kuwa tatizo linalosababisha Tanzania ikose mabilioni ya fedha.

 

Mapato ya hujuma hizo yote yanakwenda mifukoni mwa wajinga wachache baadhi yao wakiwa ni hao ambao sasa wamemwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi.

Wanalenga kuwatisha ili washindwe kutekeleza wajibu wao wa kupambana na hujuma ndani ya TPA. Wakurugenzi wa TPA wanaotetewa hawajafukuzwa, bali wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi.

 

Endapo hawana shaka kwamba wanaweza wakatiwa hatiani, hatua ambayo imeelezwa kuwa yeyote kati yao atakayekutwa na tuhuma za kujibu atafunguliwa mashtaka, wapambe wao wasingeanza kuibua vitisho vya kutunga. Kama hawana wasiwasi wangekuwa wa kwanza kusaidia uchunguzi ili ukweli kubainike,na wapendwa wao warejee kazini.

 

Haingii kichwani, kwa mfano kudai eti Chambo ametenga fungu kubwa la fedha kwa ajili ya propaganda katika vyombo vya habari, kazi inayolenga kumpamba Dk. Mwakyembe kwa kila jambo analofanya ili kumpa umaarufu kuelekea mwaka 2015.

 

Wanawakashfu waandishi wa habari kuwa watu waliobobea kwa rushwa, hivyo wanaweza kuandika chochote hata kama cha uongo iwapo wamehongwa. Wanadai udhaifu wao huo ndiyo unatumiwa na Chambo kuwaelekeza cha kufanya, wakabaki wanaimba nyimbo za kumsifu waziri wake ili kukidhi malengo yake ya kisiasa na siyo ubora katika utendaji wake.

 

Sikatai kuwa rushwa ipo hata katika vyombo vya habari na hata TPA na vitengo vyake, lakini tuhuma walizotoa dhidi ya waandishi wa habari kuhusu suala hilo ni kiwewe na kuchanganyikiwa. Wanalenga kuwatisha ili kuficha madudu yao yasianikwe, hatua ambayo itaficha maovu yao yanayosababisha mamlaka hiyo isitoe mchango stahiki kwa uchumi wa taifa.

 

Ndiyo maana wanachanganya hata tuhuma ambapo kwanza wanadai kwamba waziri huyo anatafuta umaarufu wa kisiasa kuelekea mwaka 2015, kisha wanadai kuwa anatumiwa na wapinzani. Hawataji umaarufu gani anaoutafuta na ili iweje, na pia hawasemi chochote kuwa inakuwaje anafanya hivyo huku pia akitumiwa na wapinzani kutaka CCM idhoofike! Hawasemi anasaka umaarufu huo ili agombee nafasi ipi kwa vile tayari ni mbunge na waziri, nyadhifa ambazo kamwe hakuzipata kwa kuandikwa sana magazetini, kutangazwa redioni au katika televisheni.

 

Katika hali hiyo, majungu dhidi ya Dk. Harrison Mwakyembe na Chambo ni tuhuma zinazopikwa ili kuwapaka matope na kuwatisha. Ushauri wangu ni kuwa wachape kazi zaidi na kuongeza kasi yao ya kupambana na wezi na wazembe.

 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244