Kuuza au kukodisha ardhi ni sawa na kuuza au kukodisha uhuru.
Katiba za mataifa ya Afrika zinatakiwa zipige marufuku hizi sera za ufisadi wa kisaliti za uuzaji na uwekaji rehani wa ardhi; kwani ardhi ni mali ya wananchi (si ya marais, mawaziri au wabunge) na ni haki ya kuzaliwa ya kila raia nchini, inatakiwa isiwe zao la biashara.
Tena kwa Waafrika walio wengi ardhi inakwenda ng’ambo ya uhuru; ardhi ndiyo tegemeo pekee walilonalo la kuwawezesha kuishi; ardhi ni uhai.
Kweli ambayo kila Mwafrika inabidi aizingatie kwa uwezo wote ni kwamba hakuna maendeleo hata kidogo yatakayoletwa Afrika kupitia miradi ya kuuza ardhi.
Mtu yeyote atakayesema kuwa kitendo cha watu, mashirika na mataifa ya nje kuja kulima Afrika ili walishe watu wao ni hatua ya kuiendeleza Afrika (mtu huyo awe ni msomi mwenye wadhifa gani) ni kibaraka tu huyu, tena ni wa kuepukwa, nikiazima msamiati wa Mwalimu Nyerere, “…kama ukoma.” Hicho kinachoitwa “uwekezaji wa waja katika ardhi” ni ufisadi mtupu.
Kadhalika, hii ardhi si yetu sisi tu tulio hai leo, bali na watakaozaliwa kesho na keshokutwa. Hatima ya kuuza ardhi ni kuwanyima haki za kuzaliwa za raia watakaokuja baada ya kizazi kilichopo kuchukuliwa na faradhi; kitendo ambacho zaidi ya kuwa hakitakiwi tukifanye kimila na desturi, lakini pia kinapanda mbegu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Tanzania, imezungukwa na nchi zenye madonda na makovu ya kufuata kichwa kichwa ama kiubinafsi, hizi sera ninazoita za “ufisadi wa kisaliti.” Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi mauaji ya wao kwa wao yamekuwa ni mazoea kwa sababu ya umiliki wa ardhi waliorithishwa na wakoloni na walishindwa kuwa na ubavu wa kufanya masahihisho baada ya uhuru wao. Afrika Kusini, miaka zaidi ya ishirini baada ya ubaguzi wa rangi (Apartheid) kukomeshwa Wazungu 60,000 tu bado wameatamia zaidi ya asilimia 80 ya ardhi.
Hakuna Serikali iliyowahi kurudisha ardhi mikononi mwa wananchi baada ya kuitoa kwa mikataba ya miaka 99 bila vita. Haipo. Hivyo basi, hizi hati za kumiliki ardhi zinazotolewa holela kana kwamba kesho haipo – ziwe ni za miaka 66 au 99 – kimatendo zitakuwa za milele.
Kwa nini viongozi huru wa Afrika wanaendeleza sera ambazo matokeo yake yatakuwa aidha ni kuliweka bara kwenye utumwa wa karne ya 21 wa kudumu au vita vya sisi kwa sisi visiyo na mwisho?
Tanzania, kwa mfano, migogoro baina ya wakulima na wafugaji; na kati yao wenyewe ilikuwa haipo katika upeo tulio nao sasa kabla ya utekelezaji wa sera ya Kilimo Kwanza; sera iliyozinduliwa Dodoma rasmi hivi majuzi tu – mwaka 2009 – lakini tayari watu wameanza kuuana nchi nzima kwa ajili yake; hali hii itakuwa mbaya kiasi gani baada ya miaka 50 wakati idadi ya Watanzania itafikia milioni 138 au mwaka 2100 watakapofikia milioni 276?
Ama hilo haliwasumbui viongozi leo kwa sababu watakuwa hawapo? Huo ndiyo usaliti; na mtu anayesema yatakayotokea wakati mimi sipo hayanihusu, basi huyo hana sifa za kuwa kiongozi.
Kati ya mwaka 2001 na mwaka 2012 sheria za umiliki ardhi Tanzania zimebadilishwa mara nane ili kuhalalisha wageni kuja kupora ardhi; lakini wananchi walio wengi wanapinga haya mamlaka ambayo Serikali zao zimejitwalia; ndiyo sababu ya ugomvi baina ya wananchi na wanaodaiwa kuwa ni “wawekezaji” yanazidi kuongezeka siku hadi siku.
Kwa mujibu wa “Land Rights Research and Resources Institute – LARRI” kati ya migogoro 1,825 ya ardhi iliyotokea Tanzania mwaka 2011, migogoro 1,095 iliwahusu hawa wanaoitwa “wawekezaji”. Hii ni dalili ya kuwa uvumilivu wa wananchi unaelekea ukingoni. Wakati mwafaka wa viongozi kuzingatia kilio hicho cha watu wao ni huu.
Machafuko katika nchi yoyote duniani mara nyingi huwa yanasababishwa na viongozi kupuuza vilio vya wananchi na kulazimisha sheria ambazo si za haki. Historia ya ulimwengu imejaa tele kweli hii.
Lakini hata tukitupia macho historia ya hivi karibuni: “Civil disobediences” zilizoongozwa na Mahatma Gandhi wa India, Martin Luther King Jr, wa Marekani pamoja na vita zote za ukombozi zilizopiganwa katika bara la Afrika zilikuwa na lengo moja – kupinga sheria zisizo za haki. Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema: “… hatukuwapinga makaburu kwa ukaburu wao, bali kwa ubaguzi wao.”
Kadhalika, viongozi wa Afrika leo wasijidanganye kuwa wataweza kuendeleza sheria dhulumati za kikoloni na kwamba hawatapingwa kwa sababu tu eti wao ni wazawa. Huko ni kufumbia macho ukweli.
Wakoloni walipigwa vita si kwa sababu ya rangi zao au uja wao, bali kwa sababu ya ubaguzi wao wa kikoloni uliofanya haki isijitegemee. Kunyang’anya ardhi wenyeji na kuwapa wageni ni ukoloni, unakataliwa na raia leo na kesho kama ambavyo ulikataliwa jana na juzi.
Na ni kwa sababu hii ninamtafadhalisha Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Tanzania, kwa kusema chonde futilia mbali hii sera ya Kilimo Kwanza ambayo inatumiwa kuhalalisha wageni kuja kupora ardhi yetu.
Kila mtu mwenye macho anaona kuwa umeanza vizuri sana; na kwa mwendo unaokwenda katika miaka yako mitano, Tanzania itakuwa ni nchi ya kuajabiwa. Tena katika muhula huo, kwa wema kabisa nchi itarudishwa kwenye chama kimoja kwa sababu hata wapinzani watalazimika kuunga mkono unachokifanya, kama kweli lengo lao ni kuwahudumia Watanzania.
Watapinga kitu gani? Lakini juhudi hizo zinaweza kuwa ni bure ghali kama sera ya Kilimo Kwanza haitafutwa, kwa sababu hatima yake ni vita ya sisi kwa sisi; na vita yoyote inabomoa, haijengi.
Tumeyaona hayo: Sierra Leone, Ivory Coast, Liberia, Kenya, Libya, Kongo (DRC), Uganda, Rwanda, Burundi, Angola, Msumbiji, Iraq, Afghanistan; tunayaona hivi sasa Somalia, Mashariki ya Kati ,Yemen, Syria na kwingineko.
Aidha, Mheshimiwa Magufuli, nitakuomba si tu ufute hii sera, lakini ardhi iliyokwishatolewa irejeshwe kwa wananchi kwa sababu kuu mbili:
(a) sehemu kubwa ya ardhi ilitolewa bure, hivyo gharama ya fidia itakuwa haipo au ni ndogo sana.
(b) utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia mwaka 2011, ulionesha kuwa asilimia 80 ya ardhi ambayo imekwishaporwa (duniani kwa ujumla) bado haijaendelezwa, kwa kuwa lengo kuu (prime motive) ya kuchukua hizo ardhi imekuwa ni kamari (speculation); hilo nalo litafanya gharama ya kulipa fidia iwe ni ndogo.
Viongozi wa Afrika wanapochangamkia kuigawa ardhi kwa waja, kweli wanazifikiria athari za hatua wanazochukua? Au ndiyo hizo hongo zimepofusha macho, zimeziba masikio na kupiga ganzi fikira? Afrika hivi sasa inasumbuliwa na tatizo la rushwa; yaani watu wanataka wahongwe kwa kutimiza wajibu wao; sasa watu aina hii hawawezi kamwe kutoa kitu chenye thamani kubwa kama ardhi bure tena kwa wageni.
Ninachokisema ni kuwa viongozi wanafumbia au watafumbia macho athari za kuuza ardhi kwa sababu wamenunuliwa.
Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania iwapo kweli inayo nia ya kutatua migogoro ya ardhi nchini, basi inatakiwa isisite kufuta sera ya Kilimo Kwanza; kwa namna inavyotekelezwa, sera hii haina tija, haifai na si lazima.
Kilimo Kwanza haitakiwi kufanyiwa ukarabati, bali kufutwa kabisa; hii ni sera ambayo imeanza kuvunja mshikamano na umoja wa Taifa letu kwa kugombanisha wananchi, bila kutaja athari za kulirudisha Taifa letu kwa wakoloni mamboleo waliojipachika nembo ya “wawekezaji katika ardhi.”
Sambamba na hili ifutwe kanuni ya kuanzisha benki za ardhi (Land Banks), wazo lenye madhumuni ya kuongeza kasi ya kuhamisha ardhi kutoka kwenye mikono ya wananchi na kuweka kwenye makwapa ya wakoloni mamboleo. Matokeo ya ndoa ya Kilimo Kwanza na uundaji wa “land banks” itakuwa ni kujenga unyonge kwenye nyoyo za wananchi, (yaani raia wajione hawana haki na ardhi yao) wakati nchi itakuwa inatawaliwa na “wawekezaji” kwa “remote control” kupitia vibaraka wa ndani ya nchi.
Asiyeliona hili basi ni kiongozi wa ajabu ya kuogopesha. Uhuru ni ardhi. Unapomkabidhi ardhi mja kwa mikataba ya miaka 66 au 99 kwa sababu iwayo yoyote, basi unavua uhuru wako; mmiliki wa ardhi ndiye anayemiliki Taifa – awe analala au halali Ikulu.
Kama ambavyo Serikali ya awamu ya pili ilifuta sera za Ujamaa kwa madai ya kuwa Ujamaa ulikuwa umechoka, (rejea Tamko la Zanzibar: “Kila Zama na Kitabu Chake”) wakati mwasisi wa Ujamaa, Mwalimu Nyerere, yupo hai, basi Magufuli na timu yake wasisite kufuta hizi sera ambazo si tu zimedhihirika kuwa zimechoka kikweli bali pia zimebainika kuwa zinatishia usalama na usitawi wa Taifa letu.
Hatua ya kwanza iwe ni kujitoa (opt out) katika kipengele cha shirikisho kwenye mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa sababu shirikisho halina faida kwa Watanzania, tena ni tishio kubwa kwa amani ya nchi yetu.
Shirikisho leo hii halina lengo la kujenga umoja wa kisiasa wa Jimbo la Afrika Mashariki, bali kunyemelea ardhi ya Tanzania. Na kufikiri kuwa Tanzania inaweza kuchukua watu wote walionyimwa ardhi na walimbikizaji mashuhuri wa ardhi kutoka Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi na kuwa tutaendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu ni kuota ndoto za Ali Nacha.
Hivyo basi, iwapo fursa ya kujiengua kutoka kwenye shirikisho haipo, basi tusiwepo kabisa katika mradi mzima wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Watanzania tusiruhusu Taifa letu lisambaratike katika juhudi za kinafiki za kuunda Umoja wa Afrika Mashariki. Watanzania hatuhitaji shirikisho lakini wenzetu wanaihitaji Tanzania kwa ajili ya ardhi yake na huo si msingi imara wa kujenga shirikisho.
Madai ya kuunda umoja nayo ni ulaghai mtupu. Kama baada ya miaka hamsini ya uhuru, Wakenya siyo wamoja; Wauganda sio wamoja na Wanyaruanda wa Burundi na Rwanda si wamoja watawezaje kuwa wamoja na Watanzania? Huu ni uongo ambao unatakiwa uzikwe wakati muasisi wa mradi huu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi bado yu hai.
Tuendeleze ushirikiano wa kibiashara na kusema hilo haliwezekani bila shirikisho ni utapeli. Kama nchi za Afrika zinafanya biashara na nchi za Ulaya na Marekani bila ya shirikisho sioni kwa nini ishindikane Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burudni kufanya biashara kati yao bila ya shirikisho. Fauka ya hilo hivyo ndiyo ilivyokuwa tangu 1884 (tangu ukoloni hadi leo) huu ulazima wa shirikisho unatoka wapi?