Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Same
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki amewataka machifu ambao ni viongozi wa kimila kuhamasisha jamii kulinda miundombinu ya miradi ya maendeleo.
Waziri Kairuki ametoa wito huo wakati akisimika machifu wa Kipare kwenye hafla iliyofanyika kwenye Kata ya Suji wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Halmashauri zote nchini hivyo jamii zinawajibu kushiriki kuilinda na kuitunza miradi hiyo ili iweze kudumu.
“Machifu ni watu muhimu na wana mchango mkubwa kwenye jamii zetu, hivyo niwasihi mtumie nafasi zenu kuhamasisha jamii yetu kutunza miundombinu ya miradi inayoletwa na Serikali katika maeneo yetu.”
Kairuki alitaja baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali kwa hivi sasa kuwa ni ujenzi wa madarasa 8,000 nchi nzima yanayogharimu Sh bilioni 160.
“Kwa mwaka 2022/2023, Serikali imetoa fedha shilingi bilioni 160 kujenga madarasa 8,000 kwenye shule za sekondari ili kuwezesha wanafunzi wote wenye sifa ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 wanaenda shule kwa wakati mmoja.” amesema.
Kairuki amesema pia kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), Serikali itajenga Shule za sekondari za Kata 1,000 katika kipindi cha miaka 5 kuanzia 2021-2025.
” Kwa mwaka 2021/2022 jumla ya shilingi bilioni 143.47 zimetolewa kwa ajili ya kujenga shule za sekondari 232 na shule 10 za Sekondari za wasichana za Mikoa.”
Kairuki amesema pia kupitia Mradi wa Uimarishaji Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), Serikali itatumia Sh trilioni 1.15 katika kutekeleza Mradi huo kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2026/27.
” Na kwa mwaka 2022/23 shilingi bilioni 250.9 zimepangwa kutumika ambapo zaidi ya madarasa 9,000 ya shule za awali na msingi yatajengwa.”
Kairuki ameongeza: “kupitia mradi wa BOOST shule za msingi zingine zitabomolewa kutokana na kuwa chakavu sana, zingine zitakarabatiwa, zingie zitagawanywa na kujengwa mpya kwa kadiri wataalamu watakavyoshauri kutokana na uchakavu wa shule au idadi kubwa ya wanafunzi.”
Katika hafla hiyo, Chifu Reubern Amani Mnyuku amesimikwa kuwa mwenyekiti wa machifu wa Wapare