Mabingwa watetezi, Yanga SC wameonyesha wanaweza kuendelea kufanya vizuri bila kiungo Feisal Salum Abdallah aliyesusa akishinikiza kuondoka baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam FC usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Ilikuwa mechi tamu ya funga nikufunge ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya timu mbili zinazofukuzana kwenye mbio za ubingwa, ambayo hatimaye ikaamuliwa mchezaji wa zamani wa Azam FC, Farid Mussa Malik aliyefunga bao la ushindi.
Lakini sifa zimuendee kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki aliyehusika kwenye mabao yote matatu ya Yanga.
Kwanza alimsetia mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala Mayele kufunga bao la kwanza dakika ya 31, kabla ya kufunga mwenyewe la pili dakika ya 33 na baadaye kupiga mpira wa adhabu ambao kipa wa Mcomoro wa Azam aliutema ukakwamishwa nyavuni na Farid dakika ya 78.
Lakini pia ilikuwa siku nzuri kwa kiungo mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Abdul Suleiman Sopu ambaye alifunga mabao yote ya Azam FC dakika ya 27 na 47, kabla ya kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Ayoub Lyanga dakika ya 71.
Kwa ushindi huo, Yanga SC wanafikisha pointi 47 katika mchezo wa 18 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi tisa zaidi ya Simba SC ambao hata hivyo wana mchezo mmoja mkononi na 10 zaidi ya Azam FC, ambayo pia imecheza mechi 18 na inabaki nafasi ya tatu.
Katika mchezo wa leo Yanga imemkosa kiungo wake tegemeo, Mzanzibari Feisal Salum ambaye ameandika barua ya kuomba kuvunja mkataba, jambo ambalo lilitarajiwa kuiathiri timu – lakini nyota waliobaki wameonyesha wanaweza bila yeye.