Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana amesema ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.
Kinana amesema hayo juzi wakati akitoa salamu za CCM kwenye hafla ya zoezi la ujazaji maji kwenye Bwawa la JNHPP iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kushuhudiwa na Marais wastaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete, Spika Dk Tulia Ackson na wengine wengi.
Alisema matarajio yao ni baada ya mradi huo kukamilika utapunguza makali ya bei ya ununuzi wa umeme, lakini pia utakuwa bora na salama.
“Hiki ambacho kinafanyika hapa ni cha kupongezwa sana, kwani Ilani ya CCM inatekelezwa, tumpongeze Rais Samia kwa uthubutu huo,” alisema.
Kinana amesema katika kuhakikisha wanazungumzia mradi huo kwa kina wanatarajia kufanya ziara ya kichama katika mradi huo.
Amesema chama kipo pamoja na Rais Samia katika kutekeleza miradi mbalimbali nchini.