Klabu ya Coastal Union ya Tanga imekuwa na matokeo ya kushangaza wiki hii hali ambayo sio njema sana kwa kila mpenda maendeleo ya mpira wa miguu hapa nchini.
Coastal Union walimtimua kocha wao Yusufu Chippo masaa 12 kabla ya mechi yao dhidi ya Yanga ambapo walikula kipigo cha 3-0 na baada ya matokeo hayo kocha msaidizi Sanifu Lazaro alisema kipigo hicho kilitokana na timu kumfukuza kocha mkuu ghafla.
Ukisikiliza namna kocha msaidizi wa Coastal Union, Sanifu Lazaro, anavyoulalamikia uongozi kwa maamuzi yasiyo na tija mbele ya vyombo vya habari ni wazi kwamba Coastal Union hali sio shwari hata kidogo. Sanifu Lazaro ameonesha wazi kwamba hakukubaliana na maamuzi ya viongozi wake na hakuhofia kutoa matamko makali mbele ya umma jambo ambalo liliwashangaza wengi.
Tukirudi nyuma kidogo timu hiyo ilikuwa chini ya kocha mzawa, Juma Mgunda, ambaye alijiunga na Simba SC na walipoulizwa viongozi wa Coastal Union walisema kwamba hawakuwa na taarifa zozote kuhusu kocha huyo kujiunga na Simba.
Wengi walishangazwa na hoja za Coastal Union kwamba timu yao haikuwa na mkataba kabisa na kocha Juma Mgunda na kwamba kocha huyo alikuwa akifanya tu kazi kama kibarua na alikuwa huru kujiondokea muda wowote akihitaji kufanya hivyo.
Ukichukua hilo ukaunganisha na tukio la kutimuliwa kwa Yusufu Chippo na kisha kocha msaidizi kupingana na maamuzi ya uongozi mbele ya waandishi wa habari unabaki na maswali mengi kichwani bila majibu.
Swali gumu zaidi vichwani mwa watu ni kwamba ikiwa timu ya ligi kuu inaendeshwa kwa ‘kuungaunga’ namna hiyo vipi timu za madaraja ya chini? Coastal Union ni timu kongwe na tena ipo chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto, ilitarajiwa iwe mfano na sio kituko.