Na Mwandishu Wetu

Imeshauriwa kuwa katika kupunguza kama si kumaliza kabisa rushwa ya ngono katika vyumba vya habari ni vvyema kukawa na dawati la jinsia.

Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari kwenye mkutano uliofanyika tarehe 16 Desemba 2022, jijini Dar es Salaam.

Katika mada iliyochokonolewa na mwendasha mada James Marenga, wakili wa kujitegemea kuhusu wanawake kupewa nafasi walau asilimia 30 kwenye vyombo vya habari, alianza kwa kuhoji sababu za wanawake kuwa wachache kwenye tasnia hiyo.

Kwenye mkutano huo, imeelezwa kwamba miongoni mwa sababu kwa wanawake kupata nafasi za chini katika vyombo vya habari, ni kutojiamini, mfumo dume na rushwa ya ngono.

“Kuna tatizo la rushwa ya ngono kwenye vyumba vya habari, na ii husababishwa na baadhi ya wanawake kwenye vyumba hivyo vya habari kutojiamini lakini pia mfumo dume,” amesema Lilian Timbuka, mhariri kutoka Gazeti la Mwananchi.

Imeelezwa kwamba, kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika vyumba vya habari kutatoa fursa kwa wale watakaofanyiwa matukio kinyume na maadili ya tasnia hiyo, kuwa na mahali pa kupata msaada.

Akichangia mada hiyo, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa TEF, amesema miongoni mwa sababu kwa wanawake kuangukia kwenye rushwa ya ngono kwenye vyumba vya habari ni kutokana na ugeni.

“Wapo wanaoangukia kwenye rushwa ya ngono kwa sababu wanawahiwa kwa kuwa ni wageni, ugeni huo unaambatana na woga.

“Nashauri kuwe na utaratibu kwamba wakiwa mwaka wa pili, waweze kuingizwa katika vyombo vya habari mara kwa mara walau wapate uzoefu kabla ya kumaliza masomo yao,” amesema Balile na kuongeza:

“Kwa kufanya hivyo, wataweza kujenga mazingira ya kuzoea tabia za vyumba vya habari na hapo baadaye, hawatakuwa na ugeni ambapo na woga pia utapungua.”

Akizungumzia asilimia 30 wanawake kwenye vyumba vya habari, Balile amesema kuwepo kwa sheria hiyo ambayo imependekezwa katika vikao vya maoni ya wadau wa habari na serikali, kutasaidia kumlazimisha mwajiri kuajiri wanawake.

“Walau kukiwa na sheria hii, itamlazimisha mwajiri kuajiri wanawake kwenye vyombo vyetu vya habari hata kama hataki, na kama hatofikia asilimia 30 lakini walau atafika asilimia 25,” amesema Balile.