Na Cresensia Kapinga, Songea
Amina Maketu (34), mkazi wa eneo la Namanditi Kata ya Lilambo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma amewaua watoto Wake wawili mmoja kwa kumnyonga na mwinginekwa kumpiga na kitu kizito kichwani kisha na yeye kujinyonga.
Habari zilizopatikana jana mjini Songea ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa Ruvuma Marko Chilya zimesema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Desemba 15, mwaka huu, ambapo aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Amina Maketu (34),Jeska Peter Komba na Jenifa Peter Komba mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi nane wote wakazi wa Namanditi.
Kamanda Chilya amesema kuwa tukio hilo lilitokea katika eneo la Namanditi A na kuleta taharuki kubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Songea na inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa mgogoro wa ardhi kati yake na ndugu zake pia kabla hajaamua kujinyonga ameacha ujumbe wa maandishi ambao umeeleza kuwa amejiua yeye na watoto wake ili watoto wake asije akawaacha wakipata tabu hapa duniani.
Amefafanua kuwa taarifa za awali kuwa Amina alikuwa akidaiwa madeni kwenye vicoba hivyo kutokana na madeni hayo aliamua kuchukua uamnuzi wa kuwaita watoto wake na yeye kujiua katika chumba chake.
Kamanda amesema kuwa Polisi wanaendelea kufanya upelelezi kwa kina ili kubaini ukweli halisi wa chanzo cha tukio hilo na imeelezwa pia kuwa Amina alikuwa ametengana na mume wake kwa muda mrefu.
Naye mkuu wa Wilaya ya Songea Pololeti Mgema amethibitisha kutolea Kwa tukio hilo na kuiasa jamii kuacha kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Ameshauri ni vizuri jamii inapopata tatizo ikashirikiana namna ya kulitatua kuliko kukimbilia kujiua.
Kwa upande wake Peter Komba mkazi wa Namanditi ambaye ni mzazi mwenzake na Amina amesema kuwa Amina alikuwa mke wake lakini walishatengana hakuwahi kumwambia kuwa alikuwa na matatizo yaliyomfanya ajiue yeye na watoto licha ya kuwasiliana naye kila siku.
‘Nimesikitika Sana maamuzi aliyochukua Amina , huyu ni mzazi mwenzangu lakini hakuwahi kuniekeza kuhusiana na madeni yake’ amesema Komba.
Zainabu hamisi Mkazi wa Namanditi alipohojiwa na waandishi wa habari nje kidogo na eneo la tukio kuhusiana na tukio hilo amesema
”Amina kwa muda wote aliokuwa wanaishi naye alikuwa ni mcheshi na pia aliishi vizuri na majirani na hivi karibuni kulikuwa na sherehe ambayo mshereheshaji alikuwa ni Amina hivyo nashindwa kuelewa ni magumu yapi aliyokutana nayo”
Rashid Athumani ameliomba Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kupitia dawati la jinsia kuona umuhimu wa kutoa elimu ya jinsia kwa wananchi kwa kila kata ili waweze kuondokana na matatizo wanayoweza kukutana nayo pia kukabiliana nayo na si vinginevyo.