Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Abdel Raphael (42), mkazi wa Mtaa wa Uwanja Halmashauri ya Mji Geita,Mkoa wa Geita amekutwa amefariki ndani kwake akiwa kwenye mfungo wa siku 30 akitarajia kufufuka Desemba 8,2022.
Akizungumzia tukio hilo mmoja wa waumini wake Kanyasi John amesema kuwa, marehemu alikuwa ni mchungaji wake ambaye kabla ya kifo chake walikuwa kwenye maombi maamuli kwa ajili ya kujiandaa na mkutano wa injili.
Amesema kuwa marehemu aliwaeleza kuwa kabla ya kuanza kwa mkutano huo ni vyema wakafunga kwa siku 30 kuanzia Novemba 8 na kuhitimishwa Desemba 8,2022.
“Alitueleza kuwa kuna vita kali hivyo tunatakiwa kufunga kwa mwezi mmoja lakini inapofika jioni tulikuwa tukila pamoja na marehemu,” amesema.
Amesema kuwa ilipofika tarehe 2,asubuhi marehemu aliwaeleza kuwa yeye anaingia kwenye maombi maalumu ya kimungu zaidi hivyo aliwaeleza kuwa chochote kitakachotokea wasiogope kwani mwili wake utabadilika kwa ajili ya kujiandaa na mkutano huo kutokana na kuwepo kwa vita kali na maombi.
Amesema kuwa ilipofika jioni marehemu hakuamka kula chakula cha pamoja kama ambavyo ilivyozoeleka tangu kuanza kwa maombi wakiamini kuwa anaendelea na maombi chumbani kwake.
“Alitueleza kuwa anafanya maombi hayo kwa kuwa ameambiwa na Mungu kuwa kuna vita kali, hivyo ilipofika Desemba 3 asubuhi tuliamua kwenda kumgongea kwa kuwa jana usiku hakushiriki na sisi kwenye chakuka lakini ilichukua muda mrefu bila kufunguliwa.
“Kutokana na kitendo hicho tuliamua kuingia ndani kumkuta akiwa amelala kitandani kifudifudi huku akiwa amevaa bukta , tulifanya jitihada za kumtafutia godoro na kumlaza chini kwa kuwa alitueleza kuwa tusiogope chochote kitakachotokea wakati wa maombi kwani mwili wake utabadilika ili kujiandaa na mkutano hivyo nasi tukaamini kuwa ndio dalili hizo.
“Tukiwa kwenye maombi usiku anakuja na kutushika begani au mkono na mtu yeyote akiwa amelala alikuwa akimuamsha na kumweleza kuwa aendelee na maombi,hivyo hata alivyokufa tukaendelea kuomba tukijua kuwa ni kawaida ataamka lakini tukaona siku zinazidi kwenda.
“Tulikubaliana kuwa tusiseme chochote kuhusiana na tukio hilo tuliendelea na maombi lakini ilipofika Desemba 4 harufu ilianza kusikika na kadri siku zilivyokwenda ndivyo harufu kali iliendelea kusikika zaidi.
Amesema kuwa kadri siku ilivyonga mbele ndivyo harufu kali ikizidi zaidi na walipokuwa wakienda kumwangalia hali ile ilikuwa ikiwaogopesha hata hivyo walihitimisha maombi yao Desemba 8 , kama ambavyo walikubaliana lakini mchungaji huyo hakuamka kama ambavyo aliwaeleza awali.
“Kutokana na kitendo hicho tuliamua kwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji ambaye naye alitoa taarifa Polisi na kuuchukua mwili wa marehemu,” amesema.
Hata hivyo amesema kuwa marehemu alikuwa ni mtu wa pekee na wa ajabu kwa kwani kila jambo analowaeleza lilikuwa likitokea hivyo alikuwa ni mtu mwenye imani sana.