Maafisa ugani watakiwa kujitathmini kwa kuwafikia wafugaji
JamhuriComments Off on Maafisa ugani watakiwa kujitathmini kwa kuwafikia wafugaji
Na Edward Kondela,JamhuriMedia,Tabora
MAAFISA Ugani wametakiwa kujitathmini na kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata weledi na kushirikiana na wafugaji ili wafugaji hao wafuge kibiashara pamoja na kutokomeza migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima.
Mkuu wa Wilaya ya Nzenga Mkoani Tabora Kamishna Msaidizi (ACP) Advera Bulimba, amebainisha hayo leo Desemba 15,2022 wakati akifungua mafunzo rejea ya siku mbili kwa baadhi ya maafisa hao kuanzia ngazi ya kata kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Tabora na Kigoma na wengine kutoka sekta binafsi, ambapo amesema baadhi ya kata katika wilaya hiyo zimekuwa zikihusishwa na migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima hivyo kurudisha nyuma jitihada za sekta hizo mbili kukua zaidi.
Kamishna Msaidizi Bulimba ameongeza kuwa ni wakati kwa maafisa ugani kubadilisha fikra zaidi za wafugaji kufuga kisasa na mchango wa Sekta ya Mifugo kuonekana zaidi katika pato la taifa na kubainisha kutoridhishwa na baadhi ya maafisa ugani ambao wanashindwa kufanya jitihada mbalimbali za kutokomeza migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Ugani) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Samwel Mdachi amesema mafunzo rejea kwa maafisa ugani yamekamilika katika Kanda ya Kusini na kwamba wizara inaendelea kutoa mafunzo katika kanda nyingine nchini ili kuhakikisha mafunzo hayo yanawajengea uwezo zaidi maafisa hao kufanya kazi kwa weledi zaidi.
Ameongeza kuwa mapitio ya vigezo vya kupima utendaji kazi wa maafisa ugani ni muhimu katika kupata kipimo sahihi cha utendaji kazi wao kwa kuwa una matokeo ya moja kwa moja kwa wafugaji ambao wanategemea zaidi huduma kutoka kwa maafisa hao ili kubadili fikra katika ufugaji wao.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo Afisa Mifugo na Uvuvi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora, Bw. Magesa Makaranga amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao ili kwenda kubadilisha fikra za wafugaji kufuga kwa tija.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Mifugo ukiwemo uhaba wa maafisa ugani, watahakikisha wanafanya jitihada za kuwafikia wafugaji popote walipo kadri inavyowezekana na kutatua changamoto za migogoro.