Na. Veronica Mwafisi,JamhuriMedia
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa umma nchini kujihusisha na vitendo vya wizi ambavyo vinakwenda kinyume na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora.
Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Wilaya ya Ilala,Ndejembi alisema Dkt. Samia Suluhu Hassan ana maono makubwa ya kuujenga utumishi wa umma wenye uadilifu, hivyo amewataka watumishi wa umma nchini kutokumuangusha badala yake wafanye kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa katika kulitumikia taifa.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua wazi kututhamini watumishi wa umma kwa kuboresha maslahi na stahili zetu hivyo, hatuna budi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuunga mkono kwa vitendo dhamira yake ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi,” amesisitiza Ndejembi.
Aidha,Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma kutafakari madhara ya wizi na kutathmini mienendo yao ili kutokuwa ni sehemu ya kukwamisha dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma kwa wananchi na kuliletea taifa maendeleo katika sekta zote muhimu kama vile afya, kilimo, uvuvi, biashara, uwekezaji na miundombinu.
Sanjari na hilo,Ndejembi amewataka Waajiri na Maafisa Utumishi Serikalini kuwasimamia vema watumishi wanaowaongoza badala ya kusubiria mpaka viongozi wa juu wa kitaifa kufika katika maeneo yao ya kazi kukemea uovu pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
Akizungumzia matumizi ya fedha za umma,Ndejembi amesema kuwa fedha za umma zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali kwani kinyume na hilo ni ukosefu wa maadili katika Utumishi wa Umma.
Ndejembi ameeleza bayana kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita haitomvumilia mtumishi yeyote atakayekwenda kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma kwa kujihusisha na vitendo vya wizi katika eneo lake la kazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameendelea na ziara ya kikazi Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).