Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Chamwino

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpwayungu, Chamwino mkoani Dodoma, Gabriel Hoya, amekana tuhuma za kwenda mkoani Tanga kutafuta ‘dawa’ kuzuia ‘asitumbuliwe’.

Tuhuma hizo zimetolewa baada ya Hoya kutoonekana kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Gift Msuya, kijijini hapo Novemba 29, mwaka huu.

Hata hivyo DC Msuya aliagiza kusimamishwa kazi kwa Hoya na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chiteleche, Peter Michael.

Hoya amekuwa akiandamwa na tuhuma mbalimbali zikiwamo za Diwani wa Mpwayungu, Anthony Sakalani, za kushindwa kuweka hadharani mapato na matumizi ya minara ya simu, kuuza eneo la hifadhi na la mnada, upotevu wa fedha za mradi wa maji na kutowapa vibali wanaofanya shughuli za usafirishaji abiria.

Akizungumza na JAMHURI, Hoya amesema hakufichwa na mganga wa kienyeji mkoani Tanga kuzuia asitumbuliwe na DC, isipokuwa alikuwa kwenye matibabu.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Gift Msuya (mwenye kofia), akiagana na viongozi na wananchi wa Mpwayungu baada ya kumaliza kikao.

“Hawa wanaonizushia ni wabaya wangu kisiasa, wenye nia ya kunichafua kwa maneno ya uongo. Wafahamu kuwa aibu hii si yangu peke yangu, bali wamekichafua pia chama changu (CCM).

“Wakati mkutano ukifanyika, mimi nilikuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma nikifanyiwa upasuaji. Anayedai kuniona nikifukizwa mavumba ili nisitumbuliwe si mkweli,” amesema Hoya.

Anasema kuna vikao halali ndani ya chama ambavyo wangepaswa kupeleka malalamiko dhidi yake bila kusababisha taharuki kwa wapiga kura na kukiaibisha chama.

Kuhusu mapato na matumizi ya minara ya simu, Hoya amesema ushahidi wote upo kwenye akaunti ya kijiji.

“‘Signatories’ (watia saini) wanao uthibitisho wa mapato na matumizi. Nyaraka halali za uchimbaji madini zipo na hata DC aliomba mchango wa Mwenge kwa wamiliki hawa halali,” amesema.

Hoya pia anakanusha yeye kuuza hifadhi ya ardhi ya mlima, akionyesha vielelezo na jinsi mauzo yalivyofanyika, mtendaji wa kijiji akiwa shuhuda.

JAMHURI linafahamu kwamba Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chamwino, George Malima, ameingilia kati sakata hilo kwa kuwaweka pamoja Hoya, wazee wa kata, viongozi wa dini na Diwani Sakalani.

Kikao hicho kimebaini na kuafiki kuwa Hoya hana kosa isipokuwa tu kutoitisha vikao wakati wa kilimo, hoja aliyojitetea akisema ni kwa kuwa siku hiyo akidi haikutimia
.
Kiongozi mwingine aliyetumbuliwa na DC, Michael, ameliambia JAMHURI kuwa hajahusika katika tuhuma yoyote iliyowasilishwa mkutanoni.

“Ni masilahi binafsi ya watu fulani. Hoja zao hazina ukweli wala hazina mashiko. Zinaleta vurugu na uvunjifu wa Amani, ni vema watu hawa wajifunze kuzungumza ukweli wa wanaposimama mbele ya watu,” amesema Michael.

Awali, DC Msuya alipopokea kero za wakazi wa Mpwayungu alisema ameacha kwenda kwenye sherehe za harusi ya ndugu yake ili kwenda Mpwayungu kuwaokoa wananchi.

Baada ya kumsimamisha Hoya kupisha uchunguzi, akamteua Festo Manjechi kukaimu nafasi yake na Damus Kadogosa kukaimu uenyekiti wa kitongoji badala ya Michael.
Ends