Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua kiwanda cha kuchakata maziwa cha MSS kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mkoani Katavi ambacho kina uwezo wa kusindika wastani wa lita 10,000 kwa saa.
Akizungumza baada ya kuzindua kiwanda hicho ambacho uwekezaji wake umegharimu shilingi milioni 600, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kila mwenye uwezo awekeze.
Amesema hayo leo Desemba 13, 2022 wakati akizungumza na wananchi baada ya kuzindua kiwanda hicho ambacho kwa sasa kinazalisha maziwa ya mtindi na maziwa fresh na kinatarajia kuanza uzalishaji wa Samli hivi karibuni.
Pia, Majaliwa ametoa rai kwa wafugaji wanaozunguka kiwanda hicho kuuza maziwa kwa mwekezaji huyo ili waweze kujiongezea kipato na kumwezesha mwekezaji huyo kuwa na uhakika wa malighafi ya kutosha.
“Huyu Bwana Maliki anamuunga mkono Rais Mheshimiwa Dkt. Samia katika nia yake ya kuendeleza uwekezaji nchini. Uwepo wa kiwanda hiki kunaisaidia kuendeleza mkakati wa lishe bora kwa kila Mtanzania, kwa sasa tunamshauri aendelee kupanua kiwanda hiki ili aongeze uzalishaji na wananchi wengi wazidi kupata ajira.”
Awali, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi inayojengwa katika eneo la Ilembo, Mpanda, ambapo alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya sita imeendelea na mkakati wa kupeleka huduma karibu na wananchi kwa kuhakikisha inajenga majengo ya ofisi ya mikoa na wilaya mpya Katavi ukiwemo.
Aidha,alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kwamba Serikali yao itaendelea kuwatumikia, hivyo waendelee kuiamini na kuiunga mkono. “Serikali itaendelea kuwatumikia na haitowaangusha sisi wasaidizi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia tutafanya kazi wakati wote, wakati wa jua kali na hata wakati wa mvua, tunataka kuhakikisha dhamira ya Rais wetu ya kuleta maendeleo inatimia.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema kuwa Rais Dkt. Samia ameridhia kutoa shilingi milioni 200 kupitia Bodi ya Maziwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha ukusanyaji wa maziwa Mpanda, Katavi. “Vituo hivi vitajengwa takribani kumi nchi nzima na kila kimoja kitagharimu shilingi milioni 200.”
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitamba ya maziwa 500 na madume ya nyama 500 ambayo yatagawiwa nchi nzima, lengo likiwa ni kuboresha aina ya mifugo inayofugwa na wananchi. “Serikali inataka wananchi wafuge kisasa na kibiashara.”
Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini {DPP} kufanya mapitio ya kesi na majalada mbalimbali ili yasiyokuwa na mashiko au ushahidi wa kutosha yaondolewa ili wahusika wakaendelee na shughuli za uzalishaji mali.