Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kupitia Kupitia kikosi cha usalama barabarani mkoani humo limewaonya baadhi ya mawakala wanaopandisha nauli kiholela kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kuwa halitowafumbia macho mawakala na wamiliki wa magari hayo.
Akiongea mapenda leo Desemba 13,2022 katika kituo kikuu cha mabasi yaendeayo mikoani Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi SP Solomon Mwangamilo amesema kuwa kwa sasa tiketi zinakatwa kwa mfumo wa kieletroniki ambapo amebainisha kuwa hatopenda kusikia wamiliki na wakala wa mabasi hayo hawafuati utaratibu na maelekezo ya Serikali kwa ukataji tiketi kwa mfumo wa kieletroniki.
Mwangamilo ameeleza kuwa endapo atasikia mwananchi analalamika juu ya kupandishiwa nauli hatua kali zitachukuliwa kwa wakala atakaye bainika kukiuka maagizo ya Serikali pamoja na miliki kushindwa kusimamia watendaji wake.
Aidha SP Mwangamilo ameongeza kuwa madereva wanapaswa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikighalimu maisha ya watu ambapo amebainisha kuwa jeshi hilo halina ugomvi na madereva wanafuata sheria za usalama barabarani.
Naye Yahaya Mbwana ambaye pia ni dereva wa basi linalofanya safari zake kati ya Singida na Arusha amewataka madereva wenzake kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo chanzo chake ni ukikwaji wa sheria za usalama barabarani.
Nao baadhi ya mawakala wa mabasi yaendayo mikoani walisema changamoto kubwa kutoka kwa abiria wao ni uelewa mdogo juu ya mfumo mpya na bei elekezi ya serikali ambapo walisema imekuwa chanzo cha malalamiko kwa abiria.