Mhariri,

 

Kila siku migogoro ya ardhi inaripotiwa katika nchi yetu. Kuanzia Dar es Salaam hadi mikoani ni migogoro tu.

Baadhi ya watu wanahodhi maeneo makubwa bila kuyatumia huku kasi ya wananchi ya kuuza ardhi ikiwa kubwa sana.

 

Utaratibu huu wa serikali yetu wa kukaribisha wawekezaji wakubwa si mbaya, lakini inavyoelekea sasa ni kwamba miaka michache ijayo kutaibuka machafuko makubwa kutokana na uhaba wa ardhi.

 

Inasikitisha kuona kuwa wale makaburu tuliowaogopa kama ukoma sasa wanarejea kwa kasi kwa mgongo wa uwekezaji. Makabaila wa Ulaya na Marekani wanamiminika Afrika, na hasa katika mataifa kama Tanzania kujitwalia ardhi.

 

Miaka si mingi Tanzania na mataifa mengine ya Afrika yanaweza kujikuta katika mapigano ya kudai upya Uhuru. Haya tumeyaona Zimbabwe. Tusidhani kwamba hayawezi kutokea hapa kwetu.

 

Mwisho, natoa wito kwa wananchi kuwa makini katika uuzaji ardhi kwa wageni na matajiri. Pili, Serikali iwe makini katika kuhakikisha kuwa ardhi inabaki kuwa mikononi mwa wananchi. Bila kufanya hivyo, nchi yetu inaingia katika machafuko ya kugombea ardhi.

 

Joseph Kiswangah,

Makongo Juu,

Dar es Salaam