Tanzania na Oman zimedhamiria kuchukua jitihada za makusudi kuimarisha ushikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo zenye uhusiano madhubuti wa kihistoria.
Hayo yamebainishwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo, Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) na mwenyeji wake, Mhe. Sayyid Badr Al Busaidi walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Oman uliohitimishwa jijini Muscat Desemba11, 2022.
Katika hotuba zao za kufunga Mkutano wa Pili wa JPC, Viongozi hao walieleza kuwa nchi zao zimekubaliana kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Kufuatilia Utekelezaji wa Maazimio ya Mkutano huo ili kuwa na tija kwa pande zote mbili.
Kamati hiyo pamoja na mambo meningine, itahkikisha rasimu zote za mikataba na makubaliano zinakamilika na kutiwa saini ili kujenga mazingira ya kisheria ya kuimarisha uhusiano wa kindugu uliopo baina ya Tanzania na Oman.
Maeneo yaliyojadiliwa na ujumbe wa nchi hizo na kuwekewa mikakati ya utekelezaji ni pamoja na kilimo, elimu, nishati, biashara, uwekezaji, mawasiliano, mifugo na usafirishaji. Maeneo mengine ni uvuvi, utalii, michezo, utamaduni, madini, uhamiaji, fedha na udhibiti wa majanga ya moto.
Mkutano wa JPC kati ya Tanzania na Oman ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax; Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu; Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab; Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Ndugu Kheri Mahimbali; na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Mwanahamisi Adam.