Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeahidi kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazokikabili Chuo ch bahari Dar es Salaam (DMI).
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Atupele Mwakibete, wakati wa mahafali ya 18 ya chuo hicho ambapo wahitimu 904 walitunukiwa vyeti wakiwemo 11 wa Shahada za Uzamili.
Amesema anatambua jitihada kubwa zilizofanywa na chuo katika kukabiliana na changamoto mbali mbali ikiwemo suala la meli ya mafunzo, uhaba wa madarasa, ofisi, na vifaa vingine vya kufundishia zimekuwa changamoto sugu kwa chuo hiki.
“Kama hatua ya awali ya utatuzi wa changamoto husika, ningependa sasa kuishauri Menejimenti ya chuo iandae muhtasari ikibainisha changamoto na mapedekezo kuhusu namna gani bora Wizara isaidie katika kumaliza changamoto zote kulingana na uharaka, uzito au athari za changamoto husika,” amesema.
“Napenda kuwahakikishia kwamba, mara baada ya kupokea muhtasari wa changamoto hizo Ofisi yangu itazishughulikia mapema iwezekanavyo ili nanyi muweze kuboresha huduma zenu maana ni jukumu letu sote kwa pamoja kuhakikisha kwamba shughuli za bahari zinatekelezwa katika mfumo endelevu kwa lengo la kupata maendeleo endelevu kwa taifa letu kupitia uchumi wa bluu kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa mara kwa mara na viongozi wakuu wa Serikali,” amesema Mwakibete
Ametoa wito kwa wahitimu wakatumie ujuzi walioupata kwa manufaa yenu na manufaa ya taifa kwa ujumla na waweke maslahi ya taifa mbele wakitambua kuwa dhana ya uchumi wa bluu ni pana na ina fursa nyingi ikilinganishwa na sekta nyingine.
“Nendeni mkachape kazi katika hatua yoyote inayofuata baada ya hapa mkatumie ujuzi mlioupata kama nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kupitia fursa zilizoko baharini na mkawe kivutio kwa vijana wenzenu wanaochipukia ili nao waone faida ya kusoma hapa DMI,” amesema.
Aliwataka wasibweteke na elimu mliyoipata na badala yake wakajiendeleze zaidi ili hatimaye waweze kuwa wabobezi wa masuala ya bahari kwa ustawi wa taifa na dunia kwa ujumla.
“Ninaamini kwamba, mkiyazingatia hayo mtafanikiwa na hatimaye kuwa mabalozi wazuri wa Chuo chetu cha DMI mkikitangaza vyema ndani na nje ya mipaka ya Tanzania huku mkinufaika na ajira nyingi zinazohitaji vigezo ambavyo tayari sasa mnavyo yaani ujuzi, elimu na mafunzo ya bahari,” amesema .
Aidha, amesema kwa kuzingatia kuwa mchango wa sekta ya usafirishaji wa shehena za kimataifa kwa njia ya bahari ndiyo muhimili wa uchumi wa dunia, Serikali ilipanua wigo wa majukumu ya chuo hiki ili kiwe chachu ya kukuza uchumi wa taifa letu kupitia matumizi sahihi ya vyanzo vya maji.
Amesema hivi sasa kuna ongezeko zaidi la wataalam katika sekta ya bahari kutokana na nchi kutekeleza zana ya uchumi wa buluu.
“Hii ina maana kwamba, wahitimu wa chuo hiki cha DMI ndio wanaotegemewa kwa kiasi kikubwa kuwa watenda kazi kwenye sekta ya bahari ikiwemo vyombo vya usafirishaji majini kama vile meli, uendeshaji na usimamizi wa bandari zetu, uchukuzi na lojistik, mafuta na gesi na usanifu na ujenzi wa meli,” alisema.
Amesema taaluma hizo zina mchango mkubwa katika ukuaji uchumi wa buluu na kwamba kwa msingi huu aliwapa changamoto wahitimu wa DMI ya kuhakikisha ujuzi na elimu waliyopata hapa DMI inaenda sambamba na lengo la Serikali la kufanya kazi kwa weledi na umahiri ili kujenga uchumi wa taifa letu kupitia sekta ya bahari.