*Malawi waendelea kukomaa wachukue ziwa lote

*Tanzania yasema mgawo ni nusu kwa nusu tu

*Wazee wa hekima Afrika kuitwa kusuluhisha

*Wasipoafikiana kutinga Mahakama ya ICJ

*Yote hayo yakishindikana JWTZ wataamua

 

Kumekuwapo desturi ya wanasiasa kutafuta jambo la kuwawezesha kuwajenga kisiasa, ili waweze kushinda uchaguzi, hasa Uchaguzi Mkuu. Mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa unaozihusisha nchi za Tanzania na Malawi unatajwa kuwamo mwenye mtiririko huo wa kidesturi. Malawi inatarajia kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2014, hivyo kete inayotumiwa na chama cha Rais Joyce Banda, pamoja na vyama vingine vya siasa ni kutaka kutunisha msuli kupitia mzozo wa mpaka kati yao na Tanzania kwa lengo la kujipa kuungwa mkono na Wamalawi wengi.

Kwa wapigakura wa Malawi, kipimo cha chama na mgombea anayewafaa ni yule atakayehakikisha Ziwa Nyasa lote (wenyewe wanaliita Ziwa Malawi), linabaki kwenye umiliki wa nchi hiyo bila kujali historia ya watumiaji wake. Agosti 25, mwaka huu timu za mawaziri na wataalamu kutoka Malawi na Tanzania zilikutana katika Ukumbi wa Bingu jijini Lilongwe, kuendelea na majadiliano kuhusu mpaka huo. Kikao cha mawaziri kilitanguliwa na kikao cha timu za wataalamu kilichoanza Agosti 20 katika mji wa Mzuzu uliopo Kaskazini mwa nchi hiyo.

 

Kufanyika kwa kikao cha Mzuzu na baadaye Lilongwe kulitokana na kikao cha awali kabisa kilichofanyika Julai 27-28, mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kwenye kikao hicho ndipo ulipowekwa utaratibu wa viongozi kukutana wakiwa katika makundi ya wataalamu, maofisa wa Serikali na hatimaye mawaziri kutoka pande zote mbili. Kwenye kikao cha mawaziri, Malawi iliwakilishwa na ujumbe mzito. Ujumbe huo uliwahusisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ephraim Chiume.

 

Wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Patrick Kabambe; Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Makazi, Ivy Luhanga; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rahel Zulu na Balozi wa Malawi nchini Tanzania, Flossie Chidyaonga.  Katika kuonyesha kuwa wamedhamiria, Malawi ilimwingiza kwenye kikao hicho Waziri wa Ulinzi, Ken Kandondo.

 

Kwa upande wa Tanzania, ujumbe uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka; Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa; Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule; na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Patrick Tsere.

 

Pande zote zilionekana kuupa uzito unaostahili mkutano huo. Kwa upande wa Tanzania, kitendo cha kutumia ndege maalumu ya Serikali kuliongeza uzito kwenye suala hilo. Mkutano wa Lilongwe, kwa mujibu wa Membe, ulikuwa mzuri kwa maana ya mapokezi kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Malawi na jinsi walivyojumuika kidugu.

 

Hata hivyo, shaka ya Malawi juu ya mzozo huo inatokana na ukweli kwamba huenda Tanzania ikaamua kutumia nguvu za kijeshi kumaliza mgogoro huo, ingawa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete, amemweleza mwenzake wa Malawi, Rais Banda kwamba hakuna kusudio la vita. Ingawa kauli ya Rais Kikwete ilishusha pumzi ya Wamalawi wanaoitambua Tanzania katika medani ya kivita, bado wapo wanaoamini kuwa kauli yake ilikuwa ya kuwalainisha tu.

 

Katika mitaa mbalimbali ya Lilongwe gumzo kubwa ni mzozo wa mpaka. Wananchi wengi wanatamka wazi kwamba wapo tayari kufa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Ziwa Nyasa linabaki kuwa mali ya Malawi. Ndani ya kikao, kuna habari za uhakika kwamba Waziri Membe alikuwa mbogo katika kujenga hoja akisaidiana na wenzake, Profesa Tibaijuka, Rutabanzibwa, Haule na watalaamu wengine. Membe alipoona msimamo wa Malawi ni mkali, hakusita kuwaambia ukweli kwamba kama wangeendelea kukaidi suala la kutoendelea na utafiti wa gesi na mafuta upande wa Tanzania, nguvu za kijeshi zingetumika kuzima mpango huo.

 

Waliokuwamo mwenye kikao wanasema Membe alitoa kauli hiyo bila kumung’unya maneno, hali iliyowafanya Wamalawi wapunguze jazba na kauli za “hatutaki, hatutaki” ambazo zilikuwa zikifunika nguvu za hoja na vielelezo kutoka upande wa Tanzania. Baada ya majadilino ya saa kadhaa, timu hizo mbili zilikubaliana kusaini “makubaliano ya kutokubaliana.” Makubaliano hayo yalitiwa saini na Membe kwa niaba ya Tanzania; na Chiume kwa upande wa Malawi.

 

Akizungumza baada ya utiaji saini, Chiume akionekana kuwa mpole tofauti na kauli zake kali za awali. Alitaka mzozo wa mpaka kati ya nchi hizi mbili umalizike mapema ili wananchi, hasa Wamalawi waendelee na shughuli zao za kila siku bila hofu yoyote.

 

“Sisi Malawi tungependa jambo hili lijadiliwe mapema. Limalizwe moja kwa moja ili Wamalawi wafanye biashara zao. Sisi na Watanzania ni ndugu – tena kwa kuwa usiku umeshingia mnaweza kulala. Hapa ni kwenu. Kuna ugali, matoke, ndizi, samaki,” alisema Chiume na kushangiliwa na ujumbe wa pande zote.

 

Kauli ya Membe

Membe wakati akizungumza alianza kwa kuzipongeza timu zote mbili kwa kazi kubwa na ngumu waliyoweza kuifanya hata kama haikutoa suluhisho la moja kwa moja. Akasema kazi kubwa ilifanywa na watalaamu na maofisa wa serikali mbili, na kwamba kilichofanywa na mawaziri ni “kutia nyama” katika kile kilichofikiwa. Mosi, licha ya mazungumzo kumalizika, tofauti za misimamo kati ya pande zote mbili zimebaki pale pale. Malawi wanaendelea kushikilia msimamo kwamba ziwa lote ni mali yao; ilhali Tanzania wakisema mpaka ni katikati ya Ziwa Nyasa.

 

Pili, akasema pande zote zimekubaliana kwamba sasa zimefika mahali pa kuomba msaada. Kazi hiyo imeelekezwa kwenye timu za watalaamu kutoa mapendekezo ya nini kifanyike. Mapendekezo hayo yatolewe kwenye kikao kitakachofanyika kati ya Oktoba 10 na 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam. “Kikao kitushauri cha kufanya. Je, tulete wazee wa Afrika tunaowaamini watusuluhishe? Je, tupate msuluhishi mmoja au wawili waamue kesi hii? Au je, tupelekane katika Mahakama ya Kimataifa (ICJ)? Tumewaagiza wataalamu wakae, kila pendekezo watoe faida, hasara ili tutoke hapa tulipokwama,” alisema.

 

Membe alisema kikao kilikubaliana mambo kadhaa ya kuzingatia wakati huu wa kutafuta suluhisho la kutatua mgogoro. Miongoni mwa mambo hayo ni kuacha kuhamasisha wasiwasi, hofu, mtafaraku miongoni mwa wananchi. Kubwa katika makubaliano hayo, Membe alisema kwamba wamewaomba wenzao na wamekubali kuacha utafiti wa mafuta na gesi kwa upande wa Tanzania hadi hapo suluhisho la mpaka litakapokuwa limepatikana. “Tunaomba Watanzania watuombee tuendelee na mchakato huu kwa amani ili tufike salama,” alisema.

 

Membe na historia ya mgogoro wa mpaka

Mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi ni matokeo ya mkutano wa Berlin wa mwaka 1884-85 ulioigawa Afrika. Mataifa 13 ya Ulaya ndiyo yaliyohusika katika udhalili huo. Tatizo lenyewe, wenzetu wa Malawi wanadai kwamba mpaka wetu na wao kwenye Ziwa Nyasa unapita pwani, na kwa maana hiyo ziwa lote la Nyasa kutoka kwenye mpaka wa Mozambique (Msumbiji) hadi Malawi ni mali yao. Msingi wa madai yao ni kwamba mkataba uliotiwa saini kati ya Waingereza na Wajerumani mwaka 1890 uliweka mpaka kwenye pwani au ufukwe wa Ziwa Nyasa. Mkataba huo unajulikana kama Anglo-German Agreement au Heligoland.

 

“Mheshimiwa Spika, Tanzania kwa upande wetu tunadai kwamba mpaka kati yetu na Malawi kwa Ziwa Nyasa unapita katikati ya ziwa hilo, kutoka pale Malawi na Mozambique (Msumbiji) wanapopakana, usawa wa nyuzi 11 kusini hadi mwisho wa ziwa kule Kyela kwenye digrii 9 katikati ya ziwa. Msingi wa madai yetu hayo ni kwamba kwa mujibu wa nyaraka na ramani zilizotengenezwa na wakoloni wetu Waingereza mwaka 1928, 1937 na mwaka 1939 zinaonyesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati.

 

Aidha, mkataba huo huo wa Anglo-German wa mwaka 1890 unaotumiwa kama msingi wa madai yao, umebainisha katika ibara ya 6 kwamba nchi zinazohusika yaani Tanganyika na Nyasaland wakati huo au Tanzania na Malawi sasa, zikutane ili kurekebisha kasoro katika mazingira yatakayolazimu.

 

Madai ya Tanzania yanakuwa na nguvu zaidi tunapolinganisha ‘case’ kama hii na iliyotokea kati ya Cameroon na Nigeria kuhusu mpaka wao kwenye Ziwa Chad lililopo katikati ya Nigeria na Cameroon. Katika ‘case’ hiyo iliyopelekwa kwenye Mahakama Kuu ya Dunia, Mahakama Kuu ya Dunia iliamua kwamba mpaka huu upite katikati ya Ziwa Chad ukifuata mstari ulionyooka, yaani ‘median line’ hadi kwenye mdomo wa mto….

 

Uamuzi huu ulitokana na sheria za kimataifa ambazo zinaeleza, pamoja na mambo mengine, kuwa mstari upitao katikati ya ziwa ndiyo mpaka unaokubalika kati ya nchi na nchi zinazopakana na ziwa. Kutokana na maelezo yote haya ni dhahiri kuwa tunalo tatizo linalopaswa kutatuliwa kati yetu na Malawi kuhusu mpaka wa Ziwa Nyasa.

 

Tatizo hili ni la muda mrefu. Kutokana na mazingira ya miaka ya 1960 na 1970 suala hilo lisingeliweza kutatuliwa kwa sababu mbili kubwa; mosi, kiongozi wa Malawi wa kipindi hicho Dk. Hastings Kamuzu Banda alikuwa rafiki wa serikali ya makaburu wa Afrika Kusini, wakati sisi tulikuwa marafiki wa wapigania ukombozi ikiwamo ANC ya Afrika Kusini.

 

Lakini kulikuwa na sababu ya pili, nayo ni kuwa kutokana na Tanzania kuwa makao makuu ya vyama vya ukombozi duniani, wapinzani wa Serikali ya Malawi walikimbilia Tanzania na hivyo kumfanya kiongozi wa Malawi wa wakati huo kuamini kuwa Tanzania ilikuwa kichaka cha maadui dhidi ya Serikali ya Malawi. Haya hayakuwa mazingira mazuri ya kuanza mazungumzo ya kidiplomasia kutatua tatizo la mpaka wetu kati ya Tanzania na Malawi.

 

Hitimisho

Wananchi wa Tanzania na Malawi ni ndugu wa damu. Vita si jambo jema hata kidogo. Hata hivyo, ikibidi kulinda mipaka na maslahi ya Watanzania kwa mtutu wa bunduki hilo si jambo la mjadala. Haiwezekani asilani Watanzania kando ya Ziwa Nyasa waliofaidi maji kwa muda wote wa kuumbwa dunia, leo wazuiwe kwa mikataba ya kikoloni.