Mbunge wa Nzega kupitia Chama Chama you Mapinduzi (CCM), Hamis Kigwangala, ameibua mjadala juu ya mabehewa ya SGR yaliyonunuliwa na Serikali na kuingizwa nchini hivi karibuni kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa Twitter Kigwangala amehoji uwepo wa maelezo mengi na tofautitl tofauti kuhusu ununuzi wa mabehewa hayo na kwamba ni mapya au ni yaliyotumika (mtumba) “used”, Kigwangala amehoji zaidi yalikonunuliwa kuwa ni Korea, Ujerumani au Uturuki?.
Baadhi ya wananchi kupitia mtandao huo pia wamekuwa na maoni tofauti wakihoji usahihi wa taarifa za Kigwangala.
Nalo Shirika la Reli Tanzania (TRC), kupitia mtandao huo huo limemjibu mbunge huyo wa Nzega likisema kuwa behewa zilizowasili nchini ni mpya, zimetengenezwa nchini Korea Kusini. “Behewa 14 zimewasili, Behewa 45 zinatarajiwa kuwasili nchini mwaka 2023.”
Mnamo Novemba 25, 2022 Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ilipokea behewa 14 kati ya 59 zilizotengenezwa na kampuni ya Sun Shin Rolling Stock Technology Limited ya Korea Kusini.