*Mbunge Shabiby alia naye, alalamikia ukabila
Kwenye Mkutano wa Nane wa Bunge uliomalizika hivi karibuni, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, alizungumzia kero ya maji jimboni kwake na mkoani Morogoro kwa jumla. Alishangazwa na Mkurugenzi wa MORUWASA kuendelea kuajiriwa licha ya kuzeeka, na pia alihoji ukabila ndani ya mamlaka hiyo. Endelea
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na hii paper ya taarifa ya utekelezaji ya programu ya maji vijiji, miradi katika vijiji 10. Nimeingia bungeni toka mwaka 2005 na kila mwaka katika kipindi cha bajeti lazima hii taarifa iletwe. Hii yote ni kwa ajili ya kuwaweka sawa wabunge kukubaliana na kuipitisha bajeti pasipo utekelezaji. Wabunge wote waliopo katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Nne wameshuhudia, kitu cha kwanza lazima hii ripoti iletwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi sielewi kuna matatizo gani? Ukiangalia katika Wilaya yangu ya Kilosa ambayo sasa hivi tumegawanyika na kuwa na Wilaya ya Gairo. Huu Mradi wa Vijiji Kumi vya World Bank bado uko pale pale kwenye usanifu wa miradi. Maana bado tuko namba moja hatujafika namba nne. Kuanzia 2006 mpaka sasa hivi tupo namba moja, usanifu wa mradi. Jana ndiyo limekuja lile gari la kisima kwenye Kijiji cha Kibedya na kuchimba kisima kimoja, jana na mpaka sasa hivi ninavyozungumza maji yamepatikana, lakini najua hiyo itakuwa ni hadithi tu inayoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niulize kitu kimoja, hii Wizara kama kila siku kwenye hii miradi ambayo Wabunge wengi tunalalamika haitekelezeki na kila siku haiendelei, basi ni bora ifutwe tufahamu kwamba hii miradi haipo. Kuliko kwenda vijijini kuwadanganya watu halafu miradi yenyewe haitekelezeki. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kuna mradi wa maji wa Gairo. Naishukuru Serikali imenipa mradi wa maji wa shilingi bilioni 6.664 katika Mji Mdogo wa Gairo. Huu Mji Mdogo wa Gairo ni moja ya miji saba iliyopata huu mradi na mradi huu ulitakiwa tangu mkandarasi anasaini hadi kwisha kwa mradi huu ni miezi 18. Lakini tunavyozungumza mpaka sasa hivi tayari ni miezi 24, miaka miwili na ndani ya miezi 24 bado hapa Hotuba ya Waziri katika hii miji saba anazungumzia mji mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimnukuu, anasema: “Mji wa Ikwiriri umefikia asilimia 80 ya mradi huu na Miji ya Gairo, Kibaigwa, Turiani, Kilosa na Mvomero inaendelea vizuri na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.” Lakini hajazungumzia imefikia asilimia ngapi? Sasa hii naona ni propaganda. Kwa sababu ina maana hapa hata haelewi miradi hii imefikia wapi. Kwa nini katika miji saba azungumzie asilimilia 80 ya Mji wa Ikwiriri. Kwa nini anazungumza
hivi, kuna tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie kwamba katika mradi wa Gairo mradi huu
umesimama na hauendelei kama alivyoandika hapa. Mkandarasi yupo pale matanki yote yamejengwa kuna tanki la lita milioni moja limekwisha, kuna matanki mawili ya lita laki tatu tatu yameshakwisha, lakini kwenye kuchimba kisima, kilichimbwa kimoja kikapatikana maji, viwili havina maji. Baadaye wakaja wataalamu wa kutoka Wami Ruvu, wakatoa ushauri kwamba kile kisima kilichochimbwa badala ya inchi nane sasa kipanuliwe kiende inchi kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, yule mkandarasi ameleta lile gari la kuchimbia visima pale limekaa siku kumi. Mkandarasi ameandika barua kwa Mtaalamu Mshauri, Mtaalam Mshauri akaandika MORUWASA mkoani, MORUWASA wamekaa hawatoi majibu kwamba yule mkandarasi aendelee na kipimo cha mwanzo au na hiki ambacho amepewa ushauri na Ruvu One. Mpaka leo ule mradi umesimama tu, hauendelei na mkandarasi naye amekaa tu haendelei. Sasa sijui tunafanya nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeongea na Mheshimiwa Waziri mwenyewe ananiambia tu tayari,
tayari. Majibu yale ya haraka haraka, yaani yale anakufurahisha. Mimi sitaki kufurahishwa na mtu, nataka kufurahishwa wananchi wa Jimbo la Gairo tu. Sasa ukiangalia kwa mfano, kama MORUWASA pale, wanachelewesha huu mradi. Huyo Mkurugenzi mwenyewe wa MORUWASA ameajiriwa toka mwaka 1993 mpaka leo. Amestaafu, kaongezewa muda,
amestaafu tena ameongezewa muda na mabadiliko hakuna mkoa mzima wa Morogoro hauna maji. Kwa vile tu anakula na wakubwa kule wizarani bado yupo
mpaka leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkoa mzima wa Morogoro una matatizo ya maji tu na amestaafu kwa ajili ya uzee. Sasa kama tunaendelea hivi, hivi hawa wataalamu ni hawa wazee tu, hivyo vyuo vikuu vyote wanavyosoma hawawezi kuwa wataalamu au hizi ajira za ukoo sasa? Maana umri wake unaweza ukamzaa Kapuya (Profesa Juma Kapuya), lakini mpaka leo bado yupo palepale na hii miradi haiendelei.
Sasa sio kwamba tu siungi hoja mkono kwa sababu ya kumwogopa Mheshimiwa Keissy, hapana, isipokuwa siungi mkono hoja kwa sababu nataka maelezo ya kutosha. Kwamba huu mradi utaisha lini kwa sababu muda wake wa kuisha umeshakwisha tangu miezi sita iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale pale maji inatakiwa maji yakishatoka kwenye kisima, iletwe mashine ya kuchuja maji, lakini mpaka leo, hiyo mashine haikuagizwa. Kwa hiyo, mradi ule bado utachukua muda wa mwaka mzima tena. Sasa nikikaa hapa naunga hoja mkono itakuwa haina maana yoyote na Mheshimiwa Waziri kama watu wanakuficha hapa, wakati Baraza limevunjwa na sisi tulijua na wewe ni mmoja wa wasiorudi.
Lakini kwa vile umerudi, tunajua Mheshimiwa Rais ana imani na wewe na ufanye mambo mazuri kwenye Wizara ya Maji kuonesha wananchi kwamba wewe kweli unamudu hii Wizara na unamudu uwaziri. Kwa hiyo, nategemea kwamba na ukabila uliopo MORUWASA kwa Waziri wetu mpya na hutaongeza tena muda kwa Mkurugenzi anayefuata kwa sababu mwezi huu muda wake unakwisha.