Kasi aliyoanza nayo Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dk. John Magufuli inatia moyo.
Kama kweli kelele zote za kutaka mabadiliko zilikuwa za kweli bila ajenda nyuma ya pazia ni wakati mwafaka wa kumuunga mkono kwa kasi hii aliyoanza nayo bila kujali itikadi zetu za kisiasa.
Watanzania wataendelea kuamini katika moto huu wa Rais Magufuli kutokana na kazi moja muhimu iliyobaki-nayo ni uteuzi wa wasaidizi wake kuanzia Waziri Mkuu na mawaziri.
Watanzania watashangaa na kusikitika mno kama watakaochaguliwa ni wale tuliowahi kuambiwa na viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ni MIZIGO, lakini katika hali ya kushangaza Serikali iliyopita ikaendelea kuibeba mizigo hiyo.
Watanzania watashangaa kama Baraza la Mheshimiwa Magufuli litakuwa na yule waziri tuliyewahi kuambiwa kuwa ni mzururaji. Ni kweli neno mzururaji ndilo lililosadifu tabia na hulka ya waziri huyo.
Katika hali ya kawaida inawezekana vipi waziri akasafiri kwenda Marekani na kurejea baada ya siku tatu na kupanda tena ndege kurudi huko? Inawezekana vipi waziri kulala Arusha na kuamkia Dar es Salaam kila siku? Tena akifika Dar es Salaam asiingie ofisini, aishie kwenye mahoteli?
Haya mambo yanashangaza sana. Ila pengine wa kumshangaa zaidi ni yule aliyemweka ambaye aliweka chuma masikioni asisikie kashfa hizi na kuchukua hatua.
Badala yake alisifiwa sana na Rais (Mstaafu) jambo lililoashiria kuwa pengine zile tambo zake kuwa yeye na familia ya huyo mkubwa walikuwa kitu kimoja, ni za kweli.
Nimeamua kuandika makala hii kwa lengo la kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu, kumkumbusha madudu ya Waziri huyu. Rais Magufuli, alikuwa katika Baraza moja la Mawaziri na huyu ninayemsema.
Naamini amewahi kusikia madudu hayo.
Ushahidi wa wizi, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka ya huyu mtu vipo. Si vibaya Mheshimiwa Rais akafuatilia kwa karibu ili ajiridhishe.
Nimesukumwa kuandika makala hii baada ya kusikia kuwa Nyalandu yuko kwenye ndoto eti akiuota Uwaziri Mkuu, na Uwaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Si hivyo tu, tayari ameanza kuwashirikisha marafiki zake Ubalozi wa Marekani eti wahakikishe wanamshinikiza Dk. Magufuli, ili amrejeshe Wizara ya Maliasili na Utalii. Anatumia mbinu hiyo kwa kigezo kuwa endapo hatarudishwa hapo, bado Marekani itakata misaada yake yote ya kupambana na ujangili na uhifadhi Tanzania! Mimi nasema na waikate tu. Tanzania ni nchi huru. Rais Magufuli amechaguliwa na Watanzania walio huru kifikra. Tanzania ina ukwasi wa kujiendesha yenyewe bila misaada hii yenye masharti ya udhalilishaji kwa Rais wetu na kwa Taifa letu.
Si mara moja kusikia na kusoma vituko vya Nyalandu. Madudu yake yaliwahi kuwekwa hadharani kwa ushahidi si mara moja wala mbili tu. Wengi walionyesha kushangazwa na ukimya wa aliyemteua! Ikafikia wengine kuhoji endapo alikuwa na kismati (bahati) tu au kulikuwa na kingine zaidi.
Kimsingi Rais makini alitakiwa awe amemfukuza na kumfungulia kesi kwa matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na ubadhirifu, lakini badala yake akabakia kuwa waziri huku akitamba tena kwa kiburi cha ajabu!
Baada ya kuandikwa na kulalamikiwa sana alijitokeza akijitetea. Waandishi walimshauri kwamba kama anaona kuwa hatendewi haki aende mahakamani. Baada ya kubanwa sana aliandaa taarifa kwa umma aliyodai kuwa ilitoka wizarani. Taarifa hiyo ambayo watendaji wakuu wizarani kwake walishangaa kuiona magazetini (kwa maana kwamba haikuwa imeandaliwa wizarani) haikujibu hoja yoyote zaidi ya kulalamika kuwa eti “Tuhuma dhidi yake zililenga kumchafua, kumwondolea heshima mbele ya jamii na kupunguza kasi na dhamira yake ya kupambana na ujangili”!
Tumewahi kuonyesha kwa ushahidi kuwa Nyalandu alihamishia ofisi ya wizara hotelini; alikuwa analala Arusha na kuamkia Dar kila siku awapo nchini kwa gharama na ndege ya serikali; alikwenda kuzurura Marekani na vimada kwa gharama za serikali; alikuwa anajilipa posho tatu kwa safari moja; alishiriki kugawa kinyemela vitalu vya uwindaji kwa rafiki zake Wamarekani; alitumia vibaya Leseni ya Rais kuua wanyama 700 kinyume cha sheria; alirefusha msimu wa uwindaji ili kuwafurahisha rafiki zake (Wamarekani wa TGTS); gari yake iliwahi kuhusika kwenye ujangili wa tembo; aliwahi kutishia walinzi kwa silaha huko Singida na kuvunja vizuizi pale walipotaka kukagua gari lake lillosadikiwa kuwa na nyara za serikali; alikula njama na wenye wenye mahoteli akiwashauri waishitaki Serikali kugomea tozo akiwa waziri; alisaidia baadhi ya kampuni ya utalii kukwepa kulipa kodi za serikali; alihakikisha kuwa anafukuza kazi watumishi waadilifu na kuwaweka watuhumiwa wa ujangili madarakani; alikula njama na Wakenya ili kufungua mpaka wa Bologonja huku akiwa waziri; alihusika katika kashfa ya kuagiza ndege chakavu iliyoua marubani wazalendo watatu; na alishiriki katika jaribio la kuuza mbuga zetu akishirikiana na James Lembeli kabla ya kuumbuliwa na JAMHURI.
Amebadilisha mara tatu GN inayohusu gharama katika hoteli za kitalii, amesubiri juzi Bunge limevunjwa, ametunga Kanuni Mpya za Uwindaji na kufuta zile za mwaka 2012. Ameshanaswa kwenye kamera akimpa rushwa mmoja wa viongozi wa kidini Dar es Salaam. Ametumia mamilioni ya fedha kuandaa safari nje ya nchi kama hongo kwa wabunge ili wasimtimue.
Bahati nzuri kashfa hizi ziliandikwa kwa kina kwenye magazeti na kutoa vielelezo vyote. Alifika mahali hata watumishi wa wizara wakakata tamaa. Pengine aliyemweka alijua kwa nini alifanya hivyo. Kama tembo wangeisha waishe tu, lakini yeye asingeng’oka ng’o! Watu wote walioonekana kikwazo kwake waling’oka ili abaki na kundi lake la ulaji.
Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Dk. Cyril Chami, Balozi Khamis Kagasheki, Maimuna Tarishi, Profesa Alex Songoro, Profesa Japhari Kidengesho; na Aloyce Nzuki.
Nyalandu, zaidi ya vituko alikuwa akidhihirisha kiburi hadharani kwa yeyote anayehoji tabia zake, hata kwa mawaziri wenzake. Rejea majibu yake dhidi kauli ya William Lukuvi ambaye alimlalamikia kutopatikana ofisini kwa ajili ya kutolea suluhu migogoro ya uhifadhi ikiwemo ile ya Jumuiya ya MBOMIPA; majibu yake kwa Ole Telele juu ya mgogoro wa Loliondo; na kejeli zake dhidi ya Katibu Mkuu wa chama chake, Komredi Abdurahman Kinana. Kiburi hiki na kejeli kwa wazee hawa kilitokana na imani yake kuwa yupo mwenye mamlaka zaidi aliyekuwa anamlinda.
Nakumbuka katika mkutano wake na wanaCCM wilayani Kondoa, ambako kuna mgogoro mkubwa kati ya wananchi na Pori la Akiba la Mkungunero, Katibu Mkuu wa CCM Kinana alionyesha kukerwa na tabia ya uzururaji na ubabaishaji wake kwa ziara ambazo hazina tija.
Akataka atoe mfano wa mgogoro gani amewahi kuutatua katika migogoro lukuki inayohusu watu na wanyamapori nchini kote.
Majibu kwa hoja hii, badala ya kujirekebisha, yakawa kijembe au kijeli kwa bosi wake huyu wa Chama. Kwamba eti ‘sasa nitakuwa nazurura angani (kwenye ndege)! Zaidi alichofanya ni kuwanunua baadhi ya viongozi wa dini ambao walijipambanua kama Kamati ya Amani ya Madhehebu ambao walijitokeza kumponda Kinana kwa kumtaka achunge kauli zake dhidi ya eti “mchapakazi” Nyalandu!
Wengi walihisi kuwa tamko hilo la viongozi hao wa dini aliliandaa mwenyewe! Viongozi hawa aliwaandalia ziara mbugani na hafla kadhaa kwenye hoteli za kitalii kwa kile alichowalaghai watu kuwa eti ni juhudi zake za kupambana na ujangili! Watu walihoji kuwa ujangili unafanyikaje Iringa au Serengeti halafu viongozi wa dini kutoka Dar es Salaam ndio watumiwe kupambana na ujangili?
Kwani Iringa na Serengeti hakuna viongozi wa dini? Ni wazi kuwa viongozi hawa wa dini walikuwa wanaganga njaa na Nyalandu aliwatumia kufikia malengo yake kwa kuwalipa mamilioni ya fedha za walipakodi wa nchi hii huku Muhimbili wagonjwa wakikosa asprini na vipimo mbalimbali muhimu.
Kwa sasa anafanya harakati ili kuingia kwenye Serikali ya Magufuli kama Waziri Mkuu au Waziri wa Mambo ya nchi za nje au Waziri wa Maliasili na Utalii. Tunamuomba na kumtahadharisha sana Mheshimiwa Rais Dk. Magufuli awe macho na mtu huyu. Aelewe kuwa sifa moja kubwa ya Nyalandu ni ujasiri wa kufanya mambo ya hovyo. Kubwa ni hili la uthubutu wa kununua watu kufanikisha malengo yake na kuwatumia vilivyo. Tumeshuhudia Peter Msigwa, Waziri Kivuli wa Maliasili, alivyoufyata na kuanza kujialika katika vyombo vya habari kusafisha kashfa za Nyalandu japo kwa hoja zilizochoka huku akisema mwenyewe kuwa Nyalandu anamshirikisha kwenye mambo yake ndiyo maana hakemei tena ubadhirifu wake!
Ni wazi kuwa Msigwa anayejiita mchungaji asingepata ujasiri wa kukemea madudu ya Nyalandu kutokana na kuingizwa kwenye ulaji kupitia vikao vyenye posho nene na safari nyingi za nje ya nchi. Kwa Baba Mchungaji Msigwa, maneno yaliyo kwenye kumbukumbu la Torati 16:19 kwamba “Usikubali rushwa, kwa maana rushwa hupofusha watu wanaoona vizuri” yakapoteza maana. Pengine angepewa fursa kufuta baadhi ya vifungu vya Biblia angeviondoa vifungu vyote vinavyokemea rushwa kama Ezekiel 22:12; Amosi 5:12; Mika 3:11 na 7:3; Kumbukumbu la Torati 10 na 16:19; Muhubiri 7:7; Kutoka 23:8; Ayubu 15:34; Mithali 17:23 na 29:4 na Isaya 1:23.
Tuliwahi kushuhudia Nyalandu akithubutu kuwanunua baadhi ya wabunge ili kukwamisha bajeti yake yeye mwenyewe kama shinikizo ili uamuzi wake wa kufukuza wakurugenzi na kuweka wa kwake kinyume cha sheria yaheshimiwe; tuliona alivyogomea uhamisho wa wateule wake kwenda vituo vingine na hatimaye baada ya kukwama kukimbilia ubalozi wa Marekani kuishtaki Ikulu!
Ni huyu huyu ambaye alituingiza mkenge na Wakenya baada ya kuwahakikishia kuwa angefungua mpaka wa Bologonja. Baada ya kukwama akawashauri Wakenya kuzuia magari ya watalii kutoka Tanzania kuingia Jomo Kenyatta Airport kushinikiza mpaka ufunguliwe!
Na hata baada ya hali kuwa mbaya akavunja itifaki na kwenda kukutana na mawaziri wa Kenya bila hata Balozi wetu huko kuwa na taarifa! Kama si msimamo wa Waziri Samuel Sitta kuhusu hili sijui hali ingekuwaje!
Nyalandu, bila kumshirikisha Mkurugenzi wa Wanyamapori na wataalamu wa wizara, aliandaa Tangazo la Serikali, kurefusha msimu wa uwindaji. Hii aliifanya kwa kupuuza taarifa za utafiti za TAWIRI, tamko la Waziri Kivuli wa Maliasili (japo baadaye alikaa kimyaa baada ya kuwekwa sawa!) na ushauri uliotolewa bungeni. Kwa nia ya kuwafurahisha waliomtuma (kampuni za uwindaji, hasa ya Wamarekani) Nyalandu mwenyewe alivujisha siri za serikali kwa kuwapa rasimu ya nakala ya Tangazo la serikali (GN) na hivyo kuwafanya wauze safari za uwindaji nje ya nchi.
Ni baada ya kukwama, akashirikiana na wenye kampuni kumlaumu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba amekwamisha Tangazo hilo, akidai kuwa hii ingeiletea nchi hasara kubwa kiuchumi na kidiplomasia.
Wakati analamlaumu Mwanasheria Mkuu kwa kusababisha athari kiuchumi na kidiplomasia, Nyalandu huyo huyo akasahau kuwa Julai alishirikiana na kampuni hizo hizo za rafiki zake kumnyang’anya kwa dhuluma Mtanzania vitalu na kumfutia vibali vyote vya kufanya biashara ya uwindaji hapa nchini.
Makosa aliyomtuhumu nayo mzawa akayaruhusu yafanywe na rafiki zake Wamarekani siku chache baadaye, tena kwa kutumia vibaya Leseni ya Rais! Akaruhusu watoto chini ya miaka 18 kuwaua wanyama. Picha hizi zimechapishwa, na zipo. Kama Mheshimiwa Rais anazitaka, tutampatia. Akasahau kuwa wageni wa mzawa huyu aliyekuwa na hadhi ya ukuu wa nchi walishafika nchini na kulazimika kurejea kwao baada ya Nyalandu kuwanyima vibali.
Vituko vya Nyalandu ni vingi mno. Watanzania watafarijika kama Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano atachunguza kashfa hizi ambazo kwa kiwango kikubwa zimeiumiza nchi yetu. Mheshimiwa Rais
ubarikiwe sana!