Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
SPIKA Mstaafu ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Hubert Kairuki (HKMU), Anne Makinda anatarajiwa kuwatunuku wahitimu 291 wa masomo mbalimbali kwenye mahafali ya 20 ya Chuo hicho.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Yohana Mashalla, amesema leo kuwa mahafali hayo yatakayofanyika siku ya Jumamosi tarehe 3 Desemba 2022 yatatanguliwa na Kusanyiko la Wahitimu (Convocation) siku ya Ijumaa tarehe 2 Desemba 2022 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Balozi wa Marekani nchini.
Amesema kauli mbiu ya kusanyiko hilo la wahitimu mwaka huu ni “kukuza ubunifu ili kuimarisha mifumo ya utoaji wa afya” na kuongeza kuwa kwenye tukio hilo wanafunzi waliofanya vizuri (best students) katika mitihani yao watapewa zawadi mbalimbali.
Kuhusu Mahafali amesema, yatahudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Afya na Elimu Kairuki (KHEN), Kokushubira Kairuki na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha (HKMU) Bwana John Ulanga, viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali, wadau wa mendeleo na wageni waalikwa.
Amesema kwenye mahafali hayo kutakuwa na jumla ya wahitimu 291, kati yao wanawake ni 170 na wanaume ni 121.
Ameongeza kuwa wahitimu 54 watatunukiwa Stashahada ya Uuguzi, 10 Stashahada ya Ustawi wa Jamii, 38 Shahada ya Uuguzi. Wahitimu 177 watatunukiwa Shahada ya Udaktari wa Binadamu kati yao wanawake ni 97 na wanaume ni 80.
Profesa Mashalla ameongeza kusema kwenye mahafali hayo pia jumla ya wahitimu 12 watatunukiwa shahada za Uzamili, kati yao 10 watatunukiwa Shahada ya Uzamili ya Tiba na Afya ya Watoto (MMED, Peadiatrics and Child Health).
Amesema mwanaume mmoja atatunukiwa Shahada ya Uzamili ya Upasuaji (MMED, surgery) na mwanamke mmoja atatunukiwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Afya ya Jamii (MSc, Public Health).
“Nawapongeza wahadhiri, maprofesa pamoja na watumishi wote wa HKMU kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya kuwalea na kuwafundisha wahitumu wote wanaotarajiwa kutunukiwa vyeti, stashahada na shahada siku ya Jumamosi,” amesema Profesa Mashalla.