Serikali imeombwa kukiunga Mkono Kijiji Cha Nambinda kilichopo katika Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi katika kufanikisha utekeleza wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo Ujenzi wa kituo Cha Afya.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kijiji Cha Nambinda Said Abdala Kowe wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wametembelea kijiji hicho wakiongozana na maofisa wa shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA) ambapo amesema kuwa kutokana na changamoto waliyokuwa wanaipata ya kituo cha Afya wameamua kujenga zahanati ili kurahisisha huduma hiyo.
Kowe amesema kuwa kupitia rasilimali misitu zilizopo kwenye Kijiji hicho wametumia Mill 33 kwa ajili ya kujenga zahanati jambo ambalo litaondoa changamoto iliyokuwa inawakabili ya kwenda umbali mrefu hususani wakina mama wamekuwa wakiteseka.
“Kutokana na kutokuwepo kwa zahanati katika kijiji chetu tulikuwa tunapata athari Kubwa sana maana tulikuwa tunaenda umbali wa kilomita nane hali ambayo tumepoteza watu wengi sana Kwa wagonjwa kufariki baada ya kucheleweshwa kupata matibabu”amesema Kowe
Amesema wamefarijika Kwa ujio wa Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoForEST) jambo lililowafanya kupata fedha za kuendeleza miradi katika kijiji chao hivyo wameiomba serikali kuwaunga mkono waweze kupata kituo Cha Afya kwani sera ya nchi inasema katika kila kata kuwe na kituo hicho.
“Naishauri serikali itusaidie katika ufanikishaji wa Mradi huu kwani tulikuwa na mwanakikundi mwenzetu wa Mkaa Endelevu Mmoja amepoteza Maisha akiwa mjamzito na wakati wanampeleka kituo cha afya hakufika Kwenye Kilomita nane akafariki Njiani”ameendelea kusema Mwenyekiti Kowe
Mwenyekiti Kowe amesema licha ya kwamba mradi huo walitakiwa kukamilisha Mwezi wa kumi pamoja na kusuasua kwa Fedha wanatarajia kukamilisha Mwezi wa kwanza Mwaka ujao.
Kuhusu utofauti ulipo baina ya Kijiji hicho na vingine Kowe amesema kuwa wamekuwa wa mfano katika kuhakikisha wanafanikisha Maendeleo ikiwemo mchango walioutoa kujenga vyoo vya Hostel ya sekondari yao ya kata.
Kowe amepongeza mashirika ya kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA) kwa kuwaletea Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoForEST) kwani mradi huo umesaidia sana kuwapa uelewa mpana juu ya umuhimu wa rasilimali za misitu ambazo zimeanza kuwaletea maendeleo katika kijiji chao na mwananchi mmoja mmoja.
Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii(USMJ) ambao unafikia ukingoni mwishoni mwa mwezi huu ulikuwa unatekelezwa chini ya Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoForEST) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC).