Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Serikali imekabidhi hati miliki za kimila 305 kwa wananchi wa vijiji vya Haubi na Mafai wilayani Kondoa ikiwa ni sehemu hya utekelezaji wa Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo kame nchini (LDSF).
Akikabidhi hati hizo Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Hamisi Mkanacha aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais inayotekeleza mradi huo kwa ushirikiano na Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi kwa kufanikisha zoezi hilo.
Alisema kuwa kupatikana kwa hati hizo ni fursa kubwa kwa wananchi wa vijiji hivyo na wilaya kwa ujumla kwani zitawasaidia kuepusha migogoro ya ardhi na kuwwawezesha kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha.
Hata hivyo, Dkt. Mkanacha aliwataka wanufaika wa mradi huo kuheshimu matumizi ya ardhi yaliyopangwa na kuwa ni kosa kisheria kuitumia kwa namna nyingine.
Aliwataka viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani humo kusimamia kikamilifu mipango ya ardhi iliyowekwa ili wananchi wasiende kinyume hali inayoweza kuibua migogoro.
“Ndugu zangu wananchi baadhi ya maeneo utakuta mnapanga matumzi ya ardhi lakini anatokea mtu mmoja mjuaji, mjanja anatafuta mteja anamuumizia ardhi, kwa hili tutakuwa wakali mno,” alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa kitaifa wa Mradi wa LDFS Bw. Joseph Kihaule alisema hati miliki za kimila zinazotolewa hazihamishiki na zinabaki kwa ndugu husika hivyo haruhusiwi kuuzwa.
Pia alisema mojawapo ya faida za hati hizo ni kuwa hazitalipiwa kodi ya mwaka kama ilivyo kwa hati zingine za mijini hivyo wananchi wana fursa ya kutumia ardhi hiyo kwa maendeleo endelevu.
Aidha, akizungumzia shughuli zingine za mradi huo, Bw. Kihaule alisema kwa sasa vijiji vya Haubi na Mafai vinatarajia kuchimbiwa visima ili kupunguza makali ya ukame unaokabili wilaya hiyo.
Vilevile shughuli zingine kupitia mradi huo ni kuundwa kwa vikundi vya uzalishaji mali ikiwemo ufugaji wa nyuki, mifugo pamoja na uchimbaji wa visima ambavyo vikikamilika vitatumika katika umwagiliaji.