Bweni la kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Buhangija limeteketea kwa moto na kusababisha vifo vya wanafunzi watatu wa kike wenye ulemavu wa macho Mkoani Shinyanga.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema moto huo umetokea jana Novemba 23,2022 majira ya saa 2 na nusu usiku katika bweni B lililokuwa na watoto 32 katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu (watoto wenye ualbino, viziwi na wasioona).

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linafanya uchunguzi wa tukio la moto ambao haujafahamika chanzo chake na kuteketeza bweni katika kituo cha kulelea watoto walemavu Buhangija kilichopo mkoa wa Shinyanga na kusababisha vifo vya watoto watatu wa kike,amesema Kamanda Magomi.

Amewataja watoto waliofariki dunia kuwa ni Niliam Limbu (12), Caren Mayenga (10), Catherine Paulo (10) wote ni walemavu wa macho (wasioona), wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya Msingi Buhangija.

Amesema kufuatia tukio hilo mali mbalimbali za wanafunzi na za shule zimeharibika ambazo bado thamani yake haijafahamika na hakuna majeruhi yeyote.

Baada ya taarifa za tukio hili kupatikana Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio, Pia jeshi la zimamoto na uokoaji nalo lilifika katika eneo la tukio na kufanikiwa kuzima moto ule pamoja na TANESCO kufanikisha uzimaji wa umeme haraka katika eneo lile ili kuzuia madhara makubwa ambayo yangeweza kutokea kutokana na moto ule”,ameeleza Kamanda Magomi.

Amefafanua kuwa kituo cha kulelea watoto Buhangija kilikuwa na watoto 163 waliolala bwenini kituoni hapo siku ya tukio ambapo watoto wenye ualbino ni 77 kati yao wa kike 38, wa kiume 39, wasioona 20 wa kiume 9, kike 11 ambapo watatu wamefariki dunia na Viziwi 66 kati yao wa kiume ni 31 na wa kike 35.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dkt. John Luzila amethibitisha kupokea miili mitatu ya watoto waliofariki dunia kutokana na ajali ya moto katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Buhangija.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema amefika shuleni hapo na kutoa pole kwa walimu na wanafunzi, ambapo ametumia nafasi hiyo kutoa agizo kwa walezi katika shule zote za bweni mkoani Shinyanga, kulala bweni moja na wanafunzi ili waweze kujua na kufuatilia  usalama wa watoto.

Pia, amelitaka jeshi la Zimamoto na uokoaji kutoa elimu ya namna ya kutumia vizimamoto (fire extinguisher) kwa taasisi zote ikiwemo shule, ili moto uweze kuzimwa mapema kwa kutumia vifaa hivyo pindi majanga ya moto yanapotokea.