Tume ya Utumishi ya Mahakama imekutana na wajumbe wa kamati za maadili ngazi ya Mkoa na wilaya mkoani Shinyanga, kujadili maadili na utoaji haki kwa wananchi.


Mkutano huo umefanyika leo Novemba 22, 2022 katika ukumbi wa mikutano Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, ambao umeongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof Ibrahimu Juma, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.


Amesema jana walifanya kikao na watumishi wa mahakama pamoja na wadau, ambapo leo wamekutana na wajumbe wa kamati za maadili kuanzia ngazi ya wilaya hadi Mkoa, ili kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya kuzingatia maadili na utoaji haki kwa wananchi.

Amesema lengo la ziara hiyo ni kujadiliana kwa pamoja, kubadilisha uzoefu, na kuona namna ya kujadili changamoto ambazo zinasababisha ukwamishaji wa utoaji haki kwa wananchi na kwa wakati.

“Taarifa ambayo tumeipata jana kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Athumani Matuma kuwa, kumekuwa na changamoto ya matimizi ya mtandano katika usilikizwaji wa mashauri, upungufu wa vitendea kazi ikiwamo Kopyuta na kushindwa kutoa pia nakala za hukumu mapema,”anasema Jaji Mkuu Ibrahimu Juma.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa wilaya ya Kahama Timoth Ndanya akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu kamati za maadili Mkoa wa Shinyanga, amesema kumekuwa na changamoto ya uelewa mdogo kwa wananchi kuwasilisha malalamiko yao kujua namna ya kudai haki ambapo elimu inahitajika zaidi.