Siku moja tu baada ya Arsenal kufungua pazia la Ligi Kuu ya England msimu huu kwa kwenda suluhu, kiungo mpya wa timu hiyo, Santi Carzola alimuomba kocha wake, Arsene Wenger kuingia sokoni ili kusaka wachezaji wa kuziba mapengo yaliyoachwa wazi na beki Alexander Song na mshambuliaji Robin Van Persie.

Carzola, mmoja wa wachezaji wapya watatu waliosajiliwa na kocha huyo hivi karibuni – wenzake wakiwa Olivier Giroud na Lukas Podolski – alisema kuondoka kwa Song aliyetimkia FC Barcleona ya Hispania na Robin Van Persie aliyekwenda Manchester United, kumeiathiri kwa kiasi kikubwa timu hiyo yenye makazi yake jijini London.

Dirisha la usajili kwa klabu za soka za Ulaya lilifungwa saa 6.00 usiku wa kuamkia Jumamosi. Wachezaji mbalimbali wamehama kutoka timu moja kwenda nyingine huku uhamisho wao ukifanywa na makocha wenyewe. Ndiyo maana Carzola naye alimuonyesha Wenger kuhusu mapengo hayo na siyo viongozi wa Arsenal.

Mbali na timu hizo mbili, kocha wa Tottenham Hotspurs, Andre Villas-Boas naye alikuwa amefanikiwa kumsajili mshambuliaji Emmanuel Adebayor kutoka Manchester City. Baada ya kuichezea timu hiyo kwa mkopo msimu uliopita, mchezaji huo raia wa Togo hatimaye amesajiliwa jumla kwa malipo ya pauni milioni sita, kiasi ambacho ni sawa na Sh. bilioni 15 za Kitanzania.

Timu nyingine ambazo makocha wake wamesajili wachezaji waliotajwa majina yao kwenye mabano hadi siku ya mwisho, Ijumaa iliyopita, ni Humburg (Rafael Van der Vaart), Inter Milan (Nigel de Jong), Tottenham Hotspur (Emmanuel Adebayor), Liverpool (Joe Allen), Malaga (Javier Saviola), Manchester City (Maicon), Marseille (Joey Barton), Southampton (Emmanuel Mayuka), West Ham (Modibo Maiga) na kadhalika.

Huko ndiko Ulaya, mbali kutoka Tanzania ambayo makocha wa timu zote za kandanda, bila kujali zinacheza ligi gani zikiwamo kongwe na kubwa za Simba na Yanga, hawana mamlaka ya kusajili wachezaji wanaowataka kwa kuzingatia vigezo vyao wenyewe.

Mathalani, kocha wa Simba Milovan Cirkovic anasema katika usajili wote wa timu yake msimu huu, yeye aliyekuwa akimhitaji ni Mrisho Ngassa pekee, kiungo wa pembeni aliyetua kwa Wekundu wa Msimbazi akitokea Azam FC.

“Ngassa ndiye niliyependekeza kuwa asajiliwe, lakini hao wengine wala nilikuwa siwafahamu, nililetewa tu na Kamati (ya Usajili) pamoja na mawakala wa timu. Kwa hiyo, ninachofanya ni kuwaangalia uwezo wao anayefaa nampitisha, hafai nawaambia aondoke zake,” anasema Cirkovic.

Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet, naye amekaririwa akisema kuwa hajasajili mchezaji mpya yeyote wa timu hiyo, lakini inafahamika wengi wao wamesajiliwa wakati akiwa tayari ameanza kuifundisha.

Mashabiki wa soka nchini bado wanakumbuka kile kilichoitwa “Sinema ya Kigali” ya mbio za kumsajili aliyekuwa beki wa kati wa APR ya Rwanda, Mbuyu Twitte, siku chache baada ya kumalizika kwa Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame.

Waliokuwa wakimgombea mjini Kigali hawakuwa makocha isipokuwa viongozi. Alikuwa ni Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, katika upande wa kwanza, na pia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga katika upande wa pili, Abdallah bin Kleb.

Kama alivyobainisha Cirkovic, makocha wa timu za soka hapa nchini hawasajili wachezaji. Hawapewi heshima hiyo ingawa ni wao wanaopaswa kusajili, halafu baadhi yao wanaingilia hadi kupanga wachezaji wa kucheza mechi hasa za ligi. Wanaelekezwa nani anayetakiwa acheze au akae benchi na kadhalika.

Inafikia hatua kwa baadhi ya klabu wachezaji hawawaheshimu makocha maana hawawezi kuwafanya chochote. Hawana mamlaka ya kuwaweka benchi – iwe kwenye mechi za ligi au hata za kirafiki ama vinginevyo.

Wakati Saintfiet, kwa mfano, hakusajili mchezaji yeyote, kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson ndiye aliyehangaika mwenyewe kumsajili Van Persie kutoka Arsenal, kazi aliyoifanya akichuana na makocha wenzake; Roberto de Mateo wa Chelsea na Roberto Mancini wa Manchester City.

Kama ingekuwa ni Tanzania Van Persie asingeonana na Sir Ferguson, na pia kusingekuwa na mchuano wowote kati ya kocha huyo, Mancini na De Mateo. Hapo tungeona yakiibuka mapambano ya viongozi kama ya Rage na Bin Kleb walipokuwa wakimgombea Twitte.

Van Persie angepelekwa tu kwa Ferguson kama akina Twitte na Didier Kavumbagu walivyokabidhiwa kwa Saintfiet; au akina Daniel Akuffo, Ramadhan Chombo Redondo, Kiggi Makassi, Salum Kinje, Pascal Ochieng na Komanbilli Keita walivyotambulishwa kwa Cirkovic.

Cirkovic pia hakuhusishwa wala kushauriwa chochote wakati baadhi yao walipotemwa kwa sababu mbalimbali, kubwa kuliko zote ni madai kwamba viwango vyao kisoka vimeshuka.

Kinachotakiwa kwa makocha hapa nchini ni kupokea tu wachezaji waliosajiliwa na viongozi wa timu zao. Hawashirikishwi wala hakuna maelezo yoyote wanayopewa kuhusu jinsi gani wanafanyiwa tathmini, vinatumika vigezo vipi, unatumika muda gani na kadhalika ili kujua uwezo wao wanapokuwa uwanjani.

Badala ya makocha kuhusika na usajili, wao wanapelekewa tu wachezaji na ndiyo maana pia wanatambulishwa na viongozi kama vile Mrisho Ngassa alivyotambulishwa na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange Kaburu, Didier Kavumbagu alivyotambulishwa na Bin Kleb alipotua Yanga na kadhalika.

Huwa hawajui chochote kuhusu uwezo walionao wachezaji hao wa kumiliki mipira, kupiga chenga, kutoa pasi, kukaba au wa kupanga, kuanzisha ama kushambulia lango la adui kama alivyosema Cirkovic. Ndiyo maana pia wanasajiliwa hata bila kufanya majaribio yoyote kabla ya kuingia mikataba ya kuzichezea timu hizo, na pia hawapimwi afya zao kwa sababu wanazolewa bila utaratibu wowote unaopaswa kufuatwa.

Hata hivyo, wachezaji hao wenyewe wanaposajiliwa ovyo ovyo ndivyo pia wanavyoachwa wakati wowote na mahali popote kama akina Lino Masombo, Nkanu Mbiyavanga, Mussa Mudde na Dan Mrwanda kwa Simba.

Hiyo ndiyo hali inayowakabili makocha wa timu zote 14 zitakazoshiriki michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao, ile ambayo imepangwa kuanza kutimua vumbi kwenye viwanja saba tofauti nchini, Jumamosi wiki ijayo.