Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango amekabidhi tuzo kwa washindi wa Tuzo za Rais kwa Mzalishaji Bora wa Mwaka ( PMAYA) huku akisisitiza umuhimu wa viwanda vya ndani kuongeza thamani ya bidhaa ghafi .
Amevitaka viwanda kuachana na mtindo wa kuuza nje ya nchi bidhaa nyingi za mazao ya kilimo na maliasili zikiwa ghafi hivyo kusababisha nchi kupata mapato kidogo ya fedha za kigeni na kuhamisha ajira nchi za nje.
Ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa uyoaji wa tuzo za mzalishaji bora wa mwaka (PMAYA), ambazo zinandaaliwa kila mwaka na Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), ambapo alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Mshindi wa kwanza wa jumla ni Kiwanda cha saruji cha Tanga Cement, Kilimanjaro Cable na Ando Roofing kilibuka mshindi wa tatu.
“Nilipokutana nanyi mwaka jana nilieleza kutofurahishwa na ongezeko la uagizaji wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa humu nchini. Changamoto hii bado ni kubwa kwa mfano, takribani asilimia 12 ya fedha za mauzo nje ya nchizinatumika kulipia uagizaji wa bidhaa za walaji ambazo nyingi tunaweza kuzalisha wenyewe hapa nchini na kwa mwaka unaoishia Septemba 2022, tumetumia takribani dola za Marekani milioni 346 kuagiza mbolea,” amesema
“Naomba nitumie fursa hii kuhimiza wenye viwanda wote hapa nchini mfanye jitihada na kuongeza uwezo wa uzalishaji katika viwanda vyenu ili kukidhi mahitaji ya ndani na hivyo kupunguza upotevu huu wa rasilimali hii ya fedha za kigeni,” alisisitiza.
Alisema serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji hapa nchini kwa kufanya maboresho zaidi ya kitaasisi, sheria, sera za fedha na bajeti na kwamba hadi sasa, zaidi ya kodi na tozo 230 zisizo na tija zimefutwa na takribani sheria na miongozo 40 imeboreshwa na majukumu ya baadhi ya taasisi yameendelea kuboreshwa ili kuongeza ufanisi.
Aidha, ameipongeza CTI kwa kuandaa tuzo hizo na alisema Serikali imeendelea kuongeza na kuimarisha miundombinu ikiwamo ya usafirishaji ili kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanafikika kwa urahisi na imeendelea na ujenzi wa miradi ya umeme, ili kuwa na nishati ya uhakika, huku ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaendelea kwa kasi kubwa, ili iweze kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo kutoka sehemu moja hadi nyingine.
„Sambamba na hili, tunadhamiria pia kuiunganisha reli yetu na nchi jirani kama Burundi na DRC ili kuchochea biashara ya kikanda na kuwezesha Taifa kunufaika na huduma (logistics) na usafirishaji wa madini na bidhaa mbalimbali kutoka katika nchi hizo,” amesema.
Aidha, alisema serikali inaendelea na jitihada za upanuzi na kuongeza ufanisi wa Bandari kuu za Dar es salaam, Mtwara na Tanga pia Bandari katika Maziwa Makuu na kuimarisha mfumo wa forodha kwa ajili ya upitishaji na utoaji wa mizigo kwa haraka.
Amesema Serikali pia inaendelea na ujenzi wa bandari kavu nchini ikiwa ni pamoja na bandari kavu ya Kwala, Mkoa wa Pwani ili kupunguza msongamano wa makasha (containers) na magari kutoka bandari ya Dar es Salaam.
“Sambamba na jitihada hizo za ndani, Mheshimiwa Rais ameendelea kukuza uhusiano wa kimataifa. Kwa mfano, Mheshimiwa Rais aliridhia kusainiwa kwa Mikataba ya Kutotoza Kodi Mara Mbili na nchi kumi ili kuvutia na kuimarisha biashara na uwekezaji. Vilevile, Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini kupitia Filamu ya Royal Tour na kufanya mazungumzo na Viongozi wa wafanyabiashara na wawekezaji katika nchi mbalimbali za kimkakati alizotembelea ndani na nje ya Bara la Afrika,” amesema.
Dk. Mpango amesema hatua hizi zote zimeleta matokeo chanya na kuendelea kuvutia idadi kubwa ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi akitolea mfano wa mwaka 2021 miradi iliyosajiriwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) ilikuwa 256 ikiwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 3.7 kutoka 208 mwaka 2020 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.1.
Amesema kwa kipindi cha Julai 2021 – Machi 2022, Serikali imeweza kuvutia jumla ya wawekezaji wakubwa 206 na kati yao, waliowekeza katika viwanda ni 99, sawa na asilimia 49.
Amesema idadi ya watalii ambao ni watumiaji wakubwa wa bidhaa za viwanda, pia iliongezeka kwa takribani asilimia 49 hadi kufikia watalii 922,692 mwaka 2021 ukilinganisha na idadi ya watalii 620,867 iliyofikiwa mwaka 2020.
„Mmeeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya viwanda nchini. Naomba niseme tu kwamba nimezipokea kwa niaba ya Serikali. Hata hivyo, ni vyema pia nieleze kwa ufupi hatua zilizochukuliwa na Serikali hadi sasa,” amesema .