JamhuriComments Off on Rais Samia atoa wito kwa viongozi wa dini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali kuwahimiza waumini wa dini zao kuzingatia mila, utamaduni na maadili ya Kitanzania.
Rais Samia ametoa wito huo leo katika hafla ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Kazi ya Utume na Huduma ya Kanisa la Waadventista wa Sabato yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.
Aidha, Rais Samia amewataka Viongozi wa dini kuendelea kuwaandaa watoto na vijana katika malezi yenye maadili na tabia njema ambayo yatawajenga kuwa wazalendo kwa nchi yao.
Serikali inatambua mchango wa Waadventista wa Sabato katika kuelimisha jamii katika ngazi zote kuhusu masuala ya afya na maisha bora kupitia machapisho mbalimbali na vyombo vya habari.
Vile vile, Rais Samia amewataka viongozi wa dini kuliombea taifa ili liendelee kudumu katika amani, umoja na mshikamano ambayo ndio msingi mkuu wa utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwaelimisha wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa wingi, kutunza misitu pamoja na vyanzo vya maji ili tabianchi irudi kuwa kama zamani.