Na Moses Ng’wat,JamhuriMedia,Songwe

Mchungaji wa Kanisa la Uinjilisti Tanzania, Julius Mwasimba (57), na watoto wake wawili wanashikiliwa Plisi mkoani Songwe wakituhumiwa kumfungia ndani mtoto (wa mchungaji) kwa siku tatu ili kumuombea.

Inadaiwa kuwa kwa siku zote hizo, watuhumiwa wote watatu pamoja na mgonjwa hawakula wala kunywa kitu chochote, ikiwa ni masharti ya maombi ya kumtoa mapepo mgonjwa.

Kamanda wa Polisi mkoani humo Alex Mkama amethibitisha kuwashirikilia watuhumiwa hao kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Amesema tukio hilo lilitokea Novemba 15,2022, majira ya mchana baada ya marehemu Anna Julius Mwasimba (30), Mkazi wa Iyunga Mkoani Mbeya kurudi kijijini kwao Ihowa wilayani Mbozi mkoani Songwe kwa nia ya kujiuguza.

Kamanda amesema kuwa marehemu alifikia uamuzi wa kurudi nyumbani kutokana na kusumbuliwa na maradhi ndipo baba yake mzazi (mchungaji) na wadogo zake wawili walipoanzisha huduma ya maombi nyumbani kwao.

Amewataja wanaoshikiriwa kuwa ni baba mzazi wa marehemu Julius Mwasimba (57) ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Uinjilisti Tanzania lilopo kijijini hapo Ihowa na wadogo zake marehemu Elia Julius (24) na Emmanuel Julius (21).

Kamanda Mkama amesema Jeshi la Polisi lilipata taarifa na kufika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu ambao ulionekana kubabuka na kuwa na mabaka maeneo ya usoni .

“Tunaendelea kuwashikilia watuhumiwa kwa ajili ya mahojiano zaidi na uchunguzi unaendelea,” amesema kamanda.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihowa, David Mgogo amesema watu hao walijifungia ndani katika kwa siku tatu bila kula wala kunywa wakimuombea marehemu ambaye alikuwa akiishi Iyunga Mbeya na alirudi nyumbani kwao kijijini hapo kujitazamia.

“Aliyegundua tukio hilo alikuwa mdogo wa marehemu ambaye anaishi Mlowo siku ya jana (Novemba 15) alikuja kumuona dada yake ambaye alisikia kuwa ni mgonjwa, lakini alipofika nyumbani kwao alikuta mlango umefungwa huku watu wakiendelea na kelele za maombi” amesema Mgogo

Ameongeza kuwa,baada ya kukuta mlango umefungwa na jitihada za kugonga ili afunguliwe kushindikana ndipo alipowaita majirani ambao walipofika na kuvunja mlango kisha kuingia ndani.

Amesema baada ya kuingia ndani walikuta marehemu amelala kitandani huku baba yake ambaye ni mchungaji na ndugu zake wawili wakiendelea kumuombea kwa kukemea mapepo.

Amesema baada ya kuona hali ile waliamua kupiga simu kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ihowa ambaye naye alitoa taarifa Polisi ambao walifika na kukuta mgonjwa huyo alikuwa amefariki.

Mwisho.