Uchaguzi Mkuu wa tano katika Tanzania ya Vyama vingi umemalizika.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeshindwa uchaguzi huu ambao kila mtu (hata mwanachama wa Chama cha Mapinduzi au CCM) aliamini kuwa Ukawa ungeshinda.
Kulikuwa na sababu nyingi zilizowaaminisha wananchi kwamba Ukawa ungeshinda uchaguzi huu, lakini nitazijaza sita.
Kwanza, kitendo cha vyama vinne kuungana katika mapambano dhidi ya chama kimoja cha CCM.
Pili, tofauti na miaka ya nyuma ambapo ni vyama vya upinzani peke yao vilivyoonekana kupambana na CCM, safari hii Watanzania waliungana nyuma ya Ukawa kupambana na CCM.
Tatu, zaidi ya nusu ya wapigakura (asilimia 57) walikuwa vijana ambao walikuwa vijana ambao walikuwa wanataka mabadiliko yaliyohubiriwa na Ukawa.
Nne, wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga) akinamama lishe, na waendesha bodaboda ni baadhi ya makundi ya Watanzania yaliyonyanyaswa sana na Serikali ya CCM na yaliunga mkono juhudi za kutafuta mabadiliko zilizoongozwa na Ukawa.
Tano, utendaji mbovu wa Serikali ya awamu ya nne ulichochea sana wananchi kuichukia CCM wakaamua kupambana nayo. Sita, nguvu ambayo Ukawa, iliongezewa na makada wa CCM waliohamia upinzani kutoka CCM.
Lakini ulipofikia uchaguzi Ukawa umeshindwa. Katika mazingira hayo ni muhimu tutafute kwa uwazi na ukweli mambo yaliyosababisha Ukawa kushindwa uchaguzi huu kwa lengo la kusaidia Ukawa kufanya vizuri Katika chaguzi zijazo.
Mosi, Ukawa ulikosa umoja kamili. Umoja kamili ungepatikana kama vyama vinavyounda Ukawa vingeungana kuunda chama kimoja kabla ya uchaguzi. Matokeo ya kukosekana umoja huo kamili yalikuwa vyama vinavyounda Ukawa kushindana vyenyewe maeneo mbalimbali na kutoa nafasi kwa CCM kushinda uchaguzi katika maeneo hayo.
Vilikuwa vita vya siafu vilivyomnufaisha kunguru. Kwa mfano katika majimbo ya uchaguzi 264 vyama vinavyounda Ukawa vilishindwa katika majimbo yasiyopungua 58.
Ushindani mkubwa zaidi ulikuwa kati ya Chadema na CUF ambavyo vilishindana majimbo 54. Chadema, CUF na NCCR Mageuzi vilishindana majimbo 11.
Kwa hivyo tunaona kwamba kura ambazo vyama vinavyounda Ukawa vilipata katika jimbo (au kata fulani) zilizidi kura za mgombea uchaguzi kwa tiketi ya CCM.
Lakini kura za urais kwa mgombea wa Ukawa zilizidi zile za mgombea urais wa CCM kwa kuwa wanachama na wafuasi wote wa Ukawa walimpigia kura mtu mmoja.
Katika hali hiyo Ukawa inalazimika kutafuta njia itakayowalazimisha wanachama wake kuheshimu makubaliano ya kuachia majimbo na kata.
Pili, CCM iligeuza ushindani wa vyama kuwa ushindani wa wagombea. Wananchi kwa kukosa elimu ya uraia wakabaki wanamshindanisha Dk. John Magufuli na Edward Lowassa.
Hata baadhi ya magazeti yalimzungumzia zaidi Lowassa badala ya kuzungumzia vyama vilivyokuwa vikishindana. Hii ilitokea kutokana na ukweli kwamba CCM iliona mapema kwamba baada ya serikali yake ya awamu ya nne kuboronga sana mambo wasingeweza kushindanisha chama chao na Ukawa.
Wakabaki wanamsifu mgombea wao (badala ya kukisifu chama chao) kwamba ni mchapakazi, mwadilifu, mfuatiliaji na kadhalika. Hawakuwa na jambo la kusifu chama chao.
Tatu, CCM ilidandia hoja ya mabadiliko ambayo ilikuwa hoja ya Ukawa. CCM hutamba kwamba wananchi walihitaji mabadiliko na kwamba bila CCM kujihusisha na hoja hiyo wasingeshinda uchaguzi.
CCM wakaenda mbali zaidi kiasi cha kudai kwamba mabadiliko ya kweli yangeletwa na wao na wala si watu wa Ukawa waliokuwa wakiongoza juhudi za kuleta mabadiliko.
Nne, Ukawa hawajajipanga vizuri, kwa mfano kabla ya uchaguzi wangeweza kuitisha semina mikoani ambako wangewaeleza viongozi umuhimu wa kuwaeleza wananchi serikali ya CCM ilivyowapa shida katika mambo mbalimbali.
Badala ya kufanya hivyo Ukawa haikuwaeleza sana wananchi serikali ya CCM ilivyowapa shida wananchi na walivyohitaji mabadiliko. Halafu wakati mgombea urais wa CCM aliendelea kutoa ahadi serikali yake ingewafanyia nini watu wa eneo ambalo alikuwa akihutubia.
Kwa njia hiyo aliwagusa wananchi wakati Ukawa iliendelea kuwaeleza sera zake na mambo ambayo serikali ya Ukawa ingefanya kitaifa. Halafu Ukawa hawakuingia sana vijijini wakati CCM iliingia vijijini na imeota mizizi vijijini.
Mgombea urais wa CCM ilikutana na watu wengi wa vijijini na kuzungumza nao tena vyama vinavyounda Ukawa hawakushughulika sana kufungua matawi vijijini.
Wakaenda wakati wa kampeni ambako walionekana kama wageni na watalii. Hii ilisababisha Ukawa kukosa kabisa mawakala au kupata mawakala ambao walikuwa rahisi “kununulika”.
Lakini pia Ukawa hawakuwatumia vizuri mawakala waliohama CCM. Kuna wale wenyeviti wa CCM na mikoa waliohamia Ukawa ambao wangeweza kupelekwa mikoani na vijijini kuleleza ubaya wa CCM na kwa nini waliamua kuhama chama hicho.
Pia Ukawa ungeweza kuwa na timu ambazo zingekwenda mikoani. Kwa mfano Lowassa, Sumaye na Mwenyekiti wa CCM mkoa aliyehamia huko wangetosha kusafiri pamoja. Mgombea mwenza, Kingunge Ngombale Mwiru na Mwenyekiti mwingine wa CCM aliyehamia huko wangekuwa pia timu kamili, Na kadhalika.
Tano, madai ya Mwenyekiti wa Chadema kutumia vibaya fedha za wahisani. Zilidaiwa kuwa zingeweza kusaidia wagombea ubunge na udiwani kwa tiketi ya Chadema na Ukawa kwa ujumla. Inadaiwa Mwenyekiti wa Chadema alihamishia fedha hizo Dubai kisha Hong Kong fedha zilipotolewa na wafadhili kwa ajili ya kugharamia uchaguzi huu.
Madai kama hayo yalitolewa pia katika uchaguzi wa mwaka 2005 ambapo ilidaiwa kuwa fedha iliyokuwa imetolewa na chama rafiki cha Uingereza kwa ajili ya kununua pikipiki kwa wagombea ubunge na baiskeli kwa ajili ya wagombea wa udiwani haikuwafikia walengwa.
Inavyoonekana Chadema haina uwazi katika masuala ya mapato na matumizi ya chama. Lakini kitu kimoja ni wazi, wanachama wanapogundua kuwa wanatumia nguvu kubwa katika kukijenga chama kinachonufaisha watu wachache chama kama hicho hakiwi nna mwisho mwema. Lakini pia kitendo hicho kinakatisha tamaa wafadhili.
Sita, Matumizi ya rushwa katika uchaguzi. Mwanachama wa CCM anayepewa rushwa ya kanga, fulana na kofia kabla ya uchaguzi hana uhuru wa kuchagua chama kingine hata kama ataona kwamba Serikali ya bchama chake haikufanya vizuri. Halafu kuna tatizo la muda mrefu la chama fulani kununua shahada kutoka kwa wapigakura na tatizo la chama fulani kununua mawakala ili wapindishe matokeo.
Tatizo la rushwa katika uchaguzi halitakufa nchini kwa sababu linaendelea kumwagiliwa maji na CCM.
Saba, kukosekana kwa Tume huru ya Uchaguzi wananchi walifarijika waliposikia kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeamua kura zote (pamoja na za urais) zingehesabika kwenye vituo vyua kupigia kura ili kuepusha malalamiko kwamba tume inasaidia CCM kuiba kura. Lakini haikusaidia kitu.
Inavyoonekana wasimamizi wa uchaguzi vituoni walikuwa wamepewa mbinu za kuiba kura za wapinzani. Kwa hiyo kuna madai kwamba kura za mgombea urais wa Chadema na Ukawa zilipunguzwa au ziliibwa kwa lengo la kunufaisha CCM.
Kwa mfano, imedaiwa kuwa wakati Lowassa alipata kura 32,000 Tunduma ametangazwa kuwa alipata kura 6,000 tu. Wakati huo huo ushindi wa wapinzani katika maeneo mbalimbali umepatikana baada ya wapinzani kufanya vurugu wakati wasimamizi walipochelewesha kutoa matokeo wakitafuta mbinu za kuisadia CCM kushinda uchaguzi. Katika hali hii kuna kila sababu ya wapinzani kutafuta kuanzia sasa njia ya kuiwezesha Tanzania kupata tume huru.
Nane, matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa mahakamani. Hapana shaka kitendo hicho kinachangia kwa kiasi kikubwa Tume ya Uchaguzi kufanya mambo hata mabaya ya kusaidia CCM kushinda uchaguzi katika kutambua kwamba haiwezi kufikishwa mahakamani.
Yote haya yanatendeka kwa sababu CCM ilikubali mfumo wa vyama vingi kwa shingo upande ikavuruga haki ndani ya katiba ya nchi kwa manufaa ya chama kimoja.
Hatuwezi kuorodhesha kila kitu kilichosababisha wapinzani (hususani Ukawa) kushindwa uchaguzi. Kazi iliyobaki ni kwa vyama vya upinzani kujipanga kwa ajili ya chaguzi zijazo. Kujipanga huko kuhusishe zoezi la kueneza na kufungua matawi vijijini kote nchini.
Pia kuhusisha uwezekano wa vyama vinavyounda Ukawa kugeuza Ukawa kuwa chama kamili cha siasa kudhirika kwamba wazo la kuachiana maeneo mbalimbali limeshindwa.
Hatuwezi kukamilisha makala haya bila kuwasifu makada waliohamia Ukawa kutoka CCM wakiwamo Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Kingunge Ngombale-Mwiru na wenyeviti wa CCM wa mikoa hawakupoteza wakati wametoa mchango mkubwa katika ujenzi na uimarishaji wa demokrasia Tanzania kiasi kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Watanzania wameshuhudia ushindani wa kweli wa kisiasa.
Huku nyuma CCM kilikuwa na uhakika wa kushinda mapema uchaguzi. Tena, kwa mgombea urais aliyeteuliwa na CCM alikuwa na hakika ya kuwa Rais wa Tanzania. Safari hii mambo yalikuwa tofauti. CCM na mgombea wao wote roho zao zilikuwa juu. Kwa sababu wananchi walikuwa wameamua kuikataa CCM. Kwanini walikuwa wameamua kuikataa CCM? Tutapata jibu katika toleo lijalo la gazeti hili.