Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha kuwa linachambua na kupitia kwa umakini wawekezaji watakaoleta maombi ya ujenzi wa miradi ya ubia na Shirika hilo ili kupata wawekezaji wenye uwezo wa kukamilisha ujenzi kwa viwango na wakati.
Amesema kuwa kupitia sera mpya ya ubia Serikali inatarajia kuona wawekezaji na shirika wanajenga ubia imara utakaosaidia ukuaji wa Sekta ya nyumba nchini ambayo ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi.
Ameyasema hayo leo Novemba 16, 2022 wakati akizindua sera ya ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Lengo la sera hiyo ni kuishirikisha sekta binafsi kuwekeza mitaji yake katika kujenga nyumba na majengo makubwa yenye tija kwa uchumi wa Taifa.
Amesema kuwa ushirikishwaji wa sekta binafsi katika mbalimbali utaongeza kasi na kuwa chachu ya mabadiliko katika miji yetu, hivyo Serikali itashirikiana na wawekezaji kuondoa changamoto zitakazojitokeza ili azma ya kuwekeza mitaji katika sekta hiyo iweze kutimia.
Waziri Mkuu amesema amefurahi kuona kuwa shirika hilo limedhamiria kuishirikisha sekta binafsi katika kujenga nyumba za ghorofa katika maeneo inayoyamiliki ambayo ama yamepitwa na wakati ama yana viwanja ambavyo havijaendelezwa.
“Huu ni uamuzi mzuri, unathibitisha kwa vitendo na kuunga mkono maono na maelekezo ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuvutia wawekezaji kutoka sekta binafsi kuwekeza mitaji yao ili kukuza uchumi wa nchi yetu. Serikali inafahamu kuwa ushirikishwaji wa sekta binafsi utaongeza kasi ya ujenzi na kuwa chachu ya mabadiliko katika miji yetu.”
Waziri Mkuu Amesema kuwa tangu kuanza kwa sera ya ubia mwaka 2012 shirika hilo limeingia mikataba 194 na sekta binafsi ambapo mikataba 73 ilifutwa kwa sababu ya ukiukwaji wa masharti, mikataba 111 yenye thamani ya shilingi bilioni 300, utekelezaji wake umefanyika ambapo mikataba 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 240 utekelezaji wake umekamilika na mikataba 30 yenye thamani ya shilingi bilioni 60 utekelezaji unaendelea.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ina uhaba wa nyumba milioni tatu na mahitaji hayo yanaongezeka kwa wastani wa nyumba 200,000 kila mwaka. “Upungufu huo, unachangia wamiliki wa nyumba binafsi kutoza kodi kubwa na wakati mwingine kudai kodi ya mwaka mzima kwa mkupuo mmoja.”
Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kuwezesha wananchi wengi zaidi kumiliki nyumba zinazojengwa na Shirika hilo na waendelezaji wengine wa nyumba, hivyo uamuzi huo wa kuishirikisha sekta bianfsi unaenda kuongeza idadi ya nyumba nchini na kupunguza pengo la uhaba wa nyumba.
Naye, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula amesema kuwa maboresho ya sera ya ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) yamelenga kuongeza ufanisi na tija kwa wabia wa Shirika hilo.
Aliongeza kuwa Shirika hilo litafanya uchambuzi wa kina ili kupata wawekezaji makini ambao watashikiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali na kuhakikisha wanaopata fursa hiyo ni wale wenye uwezo wa kuridhisha wa kukamilisha miradi kwa wakati na viwango.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC Nehemia Mchechu amesema kuwa sera hiyo imezingatia fursa za uchumi katika kipindi hiki, mafanikio na changamoto katika sera zilizopita.
“Sera hii pia itaongeza uwazi na mtu akitaka kuwezekeza kwenye miradi yetu isiwe lazima kumfahamu mtu yeyote ili uweze kupata fursa za miradi ya Shirika la Nyumba”