Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Morogoro

Mgonjwa aliyekwenda kutibiwa homa Hospitali ya Misheni Bwagala iliyopo Turiani, Mvomero mkoani Morogoro amenusurika kifo baada ya kunywa dawa ya kutibu upele akielekezwa kuwa ni ya homa.

Kisa hicho kimetokea Alhamisi ya Novemba 4, 2022 baada ya mfamasia hospitalini hapo (jina linahifadhiwa) kumpa mgonjwa wa homa dawa aina ya ‘Lindane Scoboma Lotion’ kwa maelekezo ya kuinywa.

Muonekano wa dawa ya upele ya Lindane Scaboma.Picha na Mtandao

Akizungumza na JAMHURI baada ya kupata fahamu, mgonjwa huyo, mama mwenye zaidi ya miaka 50, anasema alikwenda Hospitali ya Misheni Bwagala akihisi kuwa na homa.

“Baada ya kufanyiwa vipimo sikukutwa na ugonjwa wowote. Nikamweleza daktari kuwa ninahisi maumivu mengine mwilini. Akaniandikia dawa. Nikaenda dirishani kuchukua dawa,” anasema.

Akiwa dirishani, mfamasia aliyekuwapo, baada ya kusoma maelezo ya daktari kwenye cheti cha mgonjwa, akampa ‘Lindane Scoboma Lotion’ na kumpa maelekezo ya kunywa ‘mils’ 20 mara mbili kila siku kwa siku tano.

Hata hivyo, mama huyo hakunywa dawa hapo hapo, ila hadi aliporejea nyumbani kwake na baada ya kula chakula cha usiku ndipo akanywa.

“Muda mfupi baada ya kuimeza, ghafla nikaanza kutapika mfululizo huku nguvu zikiniishia. Nikapoteza fahamu hadi asubuhi!

“Majirani wanasema kwa muda wote walijitahidi kunipa huduma ya kwanza; kuninywesha maziwa na kunimwagia maji,” anasema.

Asubuhi hiyo yeye na majirani wakachukua kasha la dawa na kusoma kwa makini maelezo yaliyoandikwa ndipo wakabaini kwamba ile si dawa ya kunywa kama alivyoelekezwa na mfamasia, bali ni ya kupaka kwa ajili ya kutibu upele (scabies).

Akisaidiwa na wasamaria wema, mama huyo akarudi hospitali kwa daktari aliyemuandikia dawa, lakini hakumkuta.

“Nikaenda kwa daktari niliyemkuta siku hiyo ya pili; nikamhadithia yaliyonikuta na kuhoji kwa nini daktari aliyekuwapo jana aliniandikia kunywa dawa ya upele?

Dawa ya upele ya kupaka mwilini ambayo mfamasia
alisema anywe mils 10×2 kwa siku tano

“Yule daktari akaingia kwenye mfumo kuona ni nini alichokiandika mwenzake na kugundua kuwa dawa iliyoandikwa si niliyopewa na mfamasia,” anasema.

RMO azungumza

Akizungumza na JAMHURI, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (RMO), Dk. Kusirye Ukio, amesema ni makosa makubwa kumpa mgonjwa aina hiyo ya dawa ili ainywe kwa kuwa ni ya kupaka mwilini.

“Kilichomsaidia huyu mama ni kutapika. Asingetapika angepata athari kubwa zaidi,” anasema Dk. Ukio na kuahidi kufuatilia kwa undani tukio hilo.

Baadhi ya wauguzi na wagonjwa waliokuwapo wakati malalamiko yakiwasilishwa na mama mhusika siku ya pili baada ya kunusurika kifo, wamelalamikia kauli au ushauri uliotolewa na mganga wa zamu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (RMO), Dk. Kusirye Uki

Mchungaji wa Kanisa la Kibaptisti, Patrick Mgaya, aliyekuwapo siku hiyo, anasema kauli kwamba mama huyo arudi nyumbani na kunywa maji kwa wingi pamoja na matunda, haina mashiko.

“Ni nani atakayebea gharama za matunda? Kinachotakiwa hapa ni ufuatiliaji wa kisa kizima,” anasema huku shuhuda mwingine akitaka kuchunguzwa kwa taaluma na vyeti vya mfamasia mhusika kwa kuwa anatia shaka.

Hivi karibuni, Baraza la Wauguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), liliwafutia leseni wauguzi wasaidizi wawili wa Wilaya ya Mkomaindo, Masasi, mkoani Mtwara baada ya kupatikana na hatia ya uzembe uliosababisha kifo cha mjamzito na mtoto wake.

Mwenyekiti wa TNMC, Lilian Msele, pia aliwatia hatiani madaktari wawili wa hospitali hiyo ambao taarifa zao zitapelekwa kwenye Baraza la Madaktari ili hatua stahili zichukuliwe.