Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 21 kutokana na madini ya makaa ya mawe katika kipindi cha mwaka 2021/2022.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas wakati anatoa salama za Mkoa,kwenye mkutano wa wadau wa madini ya makaa ya mawe,uliofanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.
Kanali Thomas amesema makusanyo hayo ni saw ana asilimia 179 ya lengo la mwaka,ambapo Mkoa ulipangiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 12.
“Katika kipindi cha hivi karibuni,makaa ya mawe yamekuwa yanahitajika sana ulimwenguni kama chanzo cha nishati na hivyo kuwa moja ya chanzo kikubwa cha mapato ya serikali’’amesisitiza.
Hata hivyo amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/2023 Mkoa wa Ruvuma umepangiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 17 ambapo hadi kufikia Novemba 11,2022 tayari Mkoa umekusanya zaidi ya shilingi bilioni 15 sawa na asilimia 88.72.
Amesema hadi kufikia Juni 30,2023,Mkoa wa Ruvuma umelenga kukusanya mapato kutokana na madini ya makaa ya mawe yatakayofikia kati ya shilingi bilioni 35 hadi bilioni 40.
Naye Mgeni rasmi kwenye mkutano huo,Waziri wa Madini Dkt.Doto Biteko amewataka wawekezaji kwenye sekta ndogo ya makaa ya mawe kujenga mahusiano na jamii inayowazunguka.
“Wewe Mwekezaji uone aibu kuchimba makaa ya mawe halafu watu Jirani ya mgodi wako pale ni masikini wa kutupa,Watoto wao shuleni wanakaa chini,Mwekezaji unaingiza mapato ya bilioni mbili, lakini umeshindwa kujenga darasa la milioni 20 hiyo ni aibu’’,amesema Waziri Biteko.
Hata hivyo Waziri wa Madini amesema hivi sasa ushirikishaji watanzania katika sekta ya madini,serikali inafanya vizuri ambapo katika migodi yote nchini wafanyakazi waliopo,asilimia 97 ni watanzania na katika migodi mingine asilimia 100 ni watanzania.
Amesisitiza kuwa katika hatua ya ushirikishwaji watanzania kwenye sekta ya madini,serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inastahili kupongezwa kwa sababu zamani sekta hiyo ilimezwa kwa asilimia kubwa na wageni na kwamba zaidi ya asilimia 70 ya bajeti yote ya manunuzi katika migodi mikubwa inanunuliwa na watanzania.
Mkutano wa wadau wa makaa ya mawe umefanyika mkoani Ruvuma ukishirikisha watendaji wote wa Wizara ya Madini na mikoa inayozalisha madini hayo ikiwemo Ruvuma, Njombe,Songwe na Mbeya.
Mkoa wa Ruvuma una hazina ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 227 ambayo yanatarajiwa kuchimbwa kwa miaka 300.