Watanzania takribani 70,000 kati ya 800,000 wanaotumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs) huenda wakapoteza maisha ifikapo mwaka 2017.
Hatua hiyo inatokana na Serikali kutenga kiasi cha asilimia 9.1 pekee katika bajeti ya sekta ya afya ya 2015/16 huku zaidi ya asilimia 90 ya bajeti hiyo ikitegemea wahisani kutoka nje ya nchi, ambao pia wameanza kujiondoa kukukabili maambukizo hayo.
Kwa kiasi kikubwa jamii ya Watanzania imekuwa ikiishi kwa hofu kubwa kutokana na tatizo sugu la athari ya Ukimwi, ambalo limedumu kwa takribani miaka 32 pasipo kuwa na tiba.
Licha ya kaulimbiu mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali katika mapambano hayo ikiwamo ya Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, ya ‘Tanzania bila Ukimwi inawezekana’, Ukimwi bado ni tishio kwa jamii.
Ninachokusudia hapa ni kwamba tusiwe na utamaduni wa kutunga kaulimbiu ambazo zinakuwa na mitazamo fulani wakati utekelezaji wake hauonekani kiasi kwamba mabadiliko hayapatikani.
Ninaposema kaulimbiu ambazo hazina matunda, ninatazama kwa mapana yake kwamba Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku mbalimbali ambazo zimepangwa na Umoja wa Mataifa pamoja na zilizo kwenye kalenda yake, hata hivyo hakuna mabadiliko makubwa kama yanavyokusudiwa na wengi.
Kinachotokea katika maadhimisho ya siku hiyo ni matumizi mabaya ya fedha za umma, ambao ndiyo kwa asilimia kubwa wanaoshindwa kupata huduma bora za kukabiliana na ugonjwa huo hatari unaopukutisha nguvu kazi ya Taifa.
Hakuna kificho kuwa maisha duni ni moja ya sababu znazochangia kuongezeka kwa maambukizi ya Ukimwi hasa katika maeneo ya vijijini, ambako elimu sahihi ya ugonjwa huo haijawafikia kikamilifu.
Pamoja na kuwa ni janga la kitaifa, Serikali haijawekeza vya kutosha katika bajeti yake kutokana na ukweli kwamba asilimia 93 ya huduma za Ukimwi zimekuwa zikitegemea wahisani, huku Serikali ikitenga kiasi cha dola milioni 7 pekee kwa ajili ya usafirishaji na utunzaji wa ARV.
Tanzania pekee inakadiriwa kuwa na takribani watu 800,000 wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi, ambao wamesajiliwa kwenye vituo vya kutolea tiba. Idadi hiyo haikujumuisha watu wanaoishi na virus vya Ukimwi na wale ambao hawajapima afya zao kujua iwapo wana VVU.
Wakati Serikali ikitegemea kwa kiwango kikubwa cha uhisani kutoka nje ya nchi kugharamia sekta ya afya, taarifa zinaeleza kwamba baadhi ya wahisani hao wameshaanza kujiondoa kuisaidia Tanzania hasa katika mapambano ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.
Miongoni mwa sababu zilizofanya nchi hizo kujiondoa ni pamoja na kutoridhishwa na matumizi ya fedha wanazotoa pamoja na mdororo wa kiuchumi katika nchi zao.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa licha ya kuwapo kwa wagonjwa 800,000 wanaotumia dawa za ARV nchini Tanzania, wahisani wamesaidia ununuzi wa dozi za wagonjwa 600,000 pekee.
Wakati wahisani wakigharamia ununuzi wa dawa hizo kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 90 katika bajeti ya Taifa ya mwaka 2015/16, Serikali ya Tanzania haikuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo.
“Swali la kujiuliza; watu 200,000 wanaotumia dawa hizo nje ya bajeti iliyotolewa na wahisani wanapata dawa hizo kutoka katika bajeti gani”?
Ukweli uliofichika ni kwamba idadi hiyo inatumia bajeti ya wagonjwa 600,000 iliyotolewa na wahisani na kwamba kuna uwezekano mkubwa wa wagonjwa 70,000 kupoteza maisha ifikapo mwaka 2017 iwapo wahisani hao wataendelea kufungasha virago vyao.
Kutokana na hali hiyo, kuna haja kubwa kwa Serikali na wadau wa maendeleo pamoja na jamii kwa ujumla kuungana pamoja kukabiliana na tatizo hilo,ambalo limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa kupunguza nguvu kazi ya Taifa na wakati mwingine kuwa kundi hatarishi katika jamii.
Licha ya kwamba Tanzania ni moja ya nchi ambazo zilitia saini Azimio la Abuja nchini Nigeria, lililoagiza nchi za Afrika kutenga kiasi cha asilimia 15 ya bajeti yake katika sekta ya afya, Azimio hilo halijatekelezwa ipasavyo.
Kutokana na hali hiyo, gazeti hili limezungumza na wadau mbalimbali akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Kisukari nchini, Profesa Andrew Swai, ambaye anasema licha ya wagonjwa wa Ukimwi kutumia dawa za ARVs, wapo katika hatari kubwa ya kuugua magonjwa ya kisukari ambayo pia ni hatari katika afya zao.
Anasema uwezekano huo unatokana na vyakula wanavyotumia ili kuupa mwili nguvu wakati wakiendelea na dozi ya dawa za Ukimwi kuwa na sukari nyingi ambayo hujaa ndani ya damu kuliko inavyotakiwa.
Kwamba hulazimika kula chakula kingi wakiamini itawaepusha kuelemewa nguvu na dawa wanazotumia pasipo kujua wanaweza kuibua tatizo jingine la kisukari.
“Kitaalamu katika matibabu ya ugonjwa wa kisukari; tunashauri mtu atumie chakula cha kawaida, apunguze unene, uzito na kufanya mazoezi ili kulisaidia kongosho kufanya kazi yake vizuri,” anasema Swai.
Profesa Swai anasema utafiti uliofanywa na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari nchini mwaka 2012 ulibaini kuwa dawa za ARVs zinachochea ongezeko la watu kupata ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, huku akisema hiyo isiwe sababu ya wagonjwa kuacha kutumia ARV iwapo watabainika kuwa na maambukizi ya VVU.
Kuhusu nini kifanyike ili kunusuru maisha ya Watanzania wanaoishi na Ukimwi iwapo wahisani wote watajiondoa, mchambuzi wa masuala ya bajeti kutoka taasisi ya Policy Forum, Nichoraus Lekule, anasema mwarobaini wa tatizo hilo ni kuhakikisha jamii inalipa kodi inavyopaswa ili kuisaidia Serikali kuongeza uwezo wa kuwahudumia wananchi wake.
Kadhalika, anasema matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa kutoka kwa wananchi kwenda serikalini imesababisha jamii kutoona sababu za kulipa kodi na kwamba kinachopaswa kufanyika ni Serikali kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ili fedha zinazokusanywa zielekezwe kwenye sekta ya afya.
“Unajua utegemezi wa fedha kutoka kwa wahisani una matatizo makubwa sana…maana wakati mwingine misaada kama hiyo huja kwa masharti ya wahisani na inaweza kuchelewa na kamwe huwezi kuwashinikiza kukupa kwa wakati unaotaka wewe,” anasema.
Lekule anasema hakuna jambo la msingi katika maisha ya binadamu kama afya, hivyo kuna kila sababu kwa Serikali kuona kuwa suala hilo ni muhimu kuliko jambo jingine lolote na kwamba muda umewadia kwa Serikali kuacha kutegemea bajeti yake kutoka kwa wahisani, badala yake ijikite kukusanya mapato ya ndani na kuyatumia vizuri.
“Tanzania ina uwezo mkubwa sana wa kukusanya mapato na kuendesha shughuli zake pasipo kutegemea wahisani kama ilivyo sasa…cha msingi viongozi waliokabidhiwa dhamana ya kuongoza umma watimize wajibu wao ipasavyo badala ya wachache kuhujumu pesa zinazokusanywa kwa ajili ya maendeleo ya nchi,” anasema
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, mwaka jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, anasema Tanzania imepiga hatua katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake, baada ya kufanikiwa kutenga kiasi cha dola 49 katika matibabu ya kila Mtanzania.
Wakati akieleza hayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza mwananchi wa nchi yoyote duniani atengewe kiasi cha dola 82 katika huduma za afya kwa mwaka mzima.
Wakati Tanzania tukiendelea kusuasua katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi, Uganda, Kenya na Rwanda zimeonekana kufanya vizuri kufikia Azimio la Abuja.
Hatua hiyo inaonesha wazi kuwa Uganda imepiga hatua kubwa baada ya kutenga kiasi cha dola 53 na Kenya wakitenga dola 67 kwa ajili ya huduma za afya kwa wananchi wao ukilinganisha na Tanzania.
Kwa upande wa huduma za Ukimwi, Uganda wametenga dola milioni 25 huku Kenya wakiwa wametenga dola milioni 19 kwa ajili ya ununuzi wa dawa za kufubaza makali ya Ukimwi, wakati Tanzania tukiwa hatujatenga hata shilingi moja kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo.
Mwandishi wa makala hii ni msomaji wa gazeti la JAMHURI. Anapatikana kwa namba 0767 404501/0658 404501