Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amesema licha ya uwepo wa sheria na kanuni za kuwadhibiti wachafuzi wa mazingira hususani wanaotupa taka hovyo ni vyema pia ikaenda sambamba na kuwazomea kama sehemu ya kuwafanya wajisikie aibu kwa kosa walilolifanya.

Makalla ametoa kauli hiyo leo, Novemba 14,2022, wakati wa kikao kazi na viongozi wa wilaya wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi, meya na maafisa mazingira wakati wakipanga mipango bora ya matumizi ya ardhi kulingana mpangilio wa mkoa na mikakati endelevu ya kuimarisha suala la usafi na utunzaji wa mazingira.

Katika kikao kazi hicho kwa pamoja wamekubaliana kuweka nguvu katika kusimamia mikakati ya mwaka 2020-2030 kwa kuhimiza utoaji wa vibali vya ujenzi kwa wakati na utekelezaji wa agizo la Wizara ya Ardhi kuhusu usitishaji vibali vya ujenzi wa vituo vya mafuta.

Aidha RC Makalla ameelekeza watendaji kuanzia ngazi ya mtaa kuhakikisha wanabeba jukumu la usafi kwa kuweka mkazo kwenye kampeni ya usafi wa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi na kudhibiti machinga kufanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa.

Pamoja na hayo akalla amewataka wakandarasi wa utoaji taka kuhakikisha taka zinaondolewa kwa wakati na wananchi walipe ada ya taka.

Hata hivyo ameelekeza halmashauri za mkoa huo kuangalia upya suala la utoaji wa mikataba ya muda mrefu kwa wakandarasi wa usafi ili waweze kukopesheka na kununua vifaa vya kisasa tofauti na sasa ambapo wanapatiwa mikataba ya muda mfupi.

Makalla amesema tayari amefanikiwa kupata vifaa vya taka ambavyo amepanga kuvigawa kwenye daladala na vituo vya basi muda wowote kuanzia sasa.