Na Mwandishi Wetu, Jamhuri
WADAU wa Haki ya Kupata Habari nchini (CoRI), wamekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya wabunge, kwa lengo la kuongeza ufahamu kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma tarehe 10 Novemba 2022 ambapo kuliongozwa na mmoja wa wajumbe wa CoRI ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.
Katika kikao hicho, James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), pamoja na Balile waliwapitisha wabunge hao kwenye baadhi ya vipengele vya sheria ya habari ya mwaka 2016 pia mapendekezo ya wadau wa habari.
Pia wabunge hao walipata nafasi ya kuuliza maswali ambayo baadaye yalitolewa ufafanuzi kutoka kwa Balile na Marenga.
Wabunge hao walieleza kufurahishwa na umoja wa wadau wa habari ulioundwa kwa ajili ya kusukuma mbele mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari.
Baada ya kukabidhiwa nakala za mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari, waliahidi kuendelea kufanyika kazi na hatimaye kuwa na uelewa wa juu ili jambo hilo litakapofikishwa mbele yao, wapate kuishauri serikali kwa malengo mapana ya taifa.