Takwimu zinaonesha kuwa watoto takribani elfu Kumi na Moja huzaliwa na ugonjwa wa Sikoseli kila mwaka nchini Tanzania hali ambayo imekuwa tishio kwa Taifa la baadae.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa huduma za Tiba Prof. Paschal Ruggajo wakati wa uzinduzi wa mashirikiano baina ya Wizara ya Afya, TANCDA na NOVARTIS katika kukabiliana na Ugonjwa wa Sikoseli nchini.
“Hii ina maana kwamba kwa kila watoto elfu moja wanaozaliwa nchini Tanzania, watoto kumi na moja wana ugonjwa wa Sikoseli.” Amesema Prof. Ruggajo
Prof. Ruggajo amesema kuwa takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya Tano Duniani kwa kuwa na wingi wa wagonjwa wa Sikoseli na kuwa ya Tatu katika Afrika.
Pia, amesema katika vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano ugonjwa wa Sikoseli husababisha vifo elfu Kumi na Tano kwa mwaka.
Aidha, kutokana na changamoto hizo Prof. Ruggajo amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kukabiliana na ugonjwa huo ambao umekua na athari kubwa katika jamii.
“Miongoni mwa hatua ambazo zimechukuliwa ni pamoja na Wizara ya Afya kuingia makubaliano ya mashirikiano na Chama cha Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) na Kampuni ya dawa ya Vovartis ya nchini Switzerland kwa lengo la kudhibiti ugonjwa wa Sikoseli.” Amesema Prof. Ruggajo
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi-Magonjwa Yasiyoambukiza Dkt. James Kiologwe amewashukuru wadau hao kwa kuendelea kushirikiana na Serikali hasa katika kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza.
“Niwashukuru sana kwa mashirikiano haya, tutaendelea kushirikiana kwa kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuwahudumia wananchi, kwa pamoja tutaweza kudhibiti magonjwa haya.” Amesema Dkt. Kiologwe
Mashirikiano hayo baina ya Wizara ya Afya, Chama cha Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) na Kampuni ya dawa Novartis yamezinduliwa rasmi katika kongamano la Nne la Kisayansi la Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza Jijini Mwanza.