Kama yalivyomkuta Tim Sherwood wa Aston Villa kwa kutimuliwa, hatari zaidi inamnyemelea Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, ambaye tangu kuanza kwa msimu huu amekumbwa na balaa la matokeo mabaya katika michezo ya Ligi Kuu England (EPL).
Aston Villa wao hawajachelewa kwani wamemfukuza Sherwood baada ya kushika wadhifa huo kwa miezi minane tu kama ilivyopata kumtokea David Moyes aliyetupiwa virago Manchester United baada ya kuwaongoza Mashetani hao Wekundu kwa miezi minane msimu uliopita.
Sherwood alishuhudia timu yake ikiendelea kupoteza mchezo katika Ligi Kuu ya England kwa kuchapwa na Swansea kwa mabao 2-1.
Kevin MacDonald, Kocha wa Aston Villa, wa timu ya vijana chini ya miaka 21, ndiye atakayeshika umeneja kwa muda hadi atakapopatikana meneja mpya. Meneja wa zamani wa Everton na Manchester United, David Moyes, ametajwa katika orodha ya makocha wanaohitajika kuchukua nafasi hiyo.
Sherwood aliteuliwa kuwa meneja Februari mwaka huu kumbadili Paul Lambert na kufanikiwa kuwapeleka Villa fainali za FA Cup na pia kuwanusuru kushushwa daraja kutoka EPL walipomaliza nafasi ya 17.
Kuhusu Mourinho, Chelsea kwa upande wao wanajiandaa kuachana na raia huyo wa Ureno pia kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo, baada ya kichapo cha Jumamosi iliyopita dhidi ya West Ham United.
Kibarua cha Mourinho kipo mikononi mwa bodi ya Chelsea ambao tayari wameanza kumjadili na huenda nafasi yake akapewa ama Carlo Ancelotti au Guud Hiddink.
Taarifa zinasema kuna uwezekano wa Mourinho kupewa nafasi ya kutetea ajira yake katika mchezo ambao Chelsea itaikabili Stoke City kwenye Kombe la Capital One au ule mchezo dhidi ya Liverpool kwenye mechi ya ugenini.
Baada ya kipogo dhidi ya West Ham kwenye Uwanja wa Upton Park, Chelsea tayari imeshapoteza michezo sita ya EPL huku ikiwa nafasi ya 15 kwa kuwa na ponti 11 na macho ya uongozi wa Chelsea yanamwangazia Ancelotti.
Mbali ya Ancelotti, makocha wengine wanaotajwa kurithi mikoba yake ni Hiddink, Pep Guardiola na Diego Simeone kwani taarifa zinasema uongozi wa klabu hiyo tayari umewasiliana na makocha hao na kuwaeleza ‘wakae mkao wa kula’.
Kwa upande wake, Mourinho amekataa kuzungumza na wanahabari kwani mbali ya yeye kutolewa kwenye benchi, pia kiungo wa kati Nemanja Matic alitolewa uwanjani kwa kuoneshwa kadi mbili za njano hivyo kufanya nyekundu moja.
Mourinho naye alifukuzwa eneo wanalokaa makocha uwanjani wakati wa kuanza kwa kipindi cha pili baada ya kujaribu kuzungumza na refa, Jon Moss, wakati wa mapumziko.
Mauro Zarate aliiweka West Ham mbele dakika ya 17 baada ya Chelsea kushindwa kujilinda vyema wakati wa kupigwa kwa kona.
Gary Cahill alisawazisha kwenye dakika ya 56 lakini Carroll aliyeingia kama nguvu mpya aliifikia krosi kali ya Aaron Cresswell na kujitwisha ngoma dakika ya 79.
Wachezaji wengine watano wa Chelsea pia walioneshwa kadi za njano kwenye debi hiyo ya London Magharibi, ya mwisho kuchezewa Upton Park kabla ya West Ham kuhamia Olympic Stadium majira yajayo ya joto.
Aliyemtia doa Mourinho
Huenda Mourinho katiwa doa na kutumia lugha mbaya dhidi ya aliyekuwa daktari wa timu Eva Carneiro.
Dk. Carneiro aliingia uwanjani kumtibu mshambuliaji Eden Hazard wakati wa dakika za lala salama kwenye mchezo wa mwanzo za ligi dhidi ya Swansea, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Mara baada ya mechi hiyo na Swansea, tabibu huyo aliondolewa kuihudumia timu ya Kwanza ya Chelsea na hivyo kuamua kubwaga manyanga kuwapo Chelsea, licha ya kutakiwa kurudi kazini na sasa yuko mbioni kusaka sheria katika mamlaka husika.