Nianze kwa kutoa pole nyingi sana kwa wafiwa wa Mchungaji Christopher Mtikila. Mchungaji Mtikila alikuwa mtu wa jirani sana kwangu na nimezungumza naye mara nyingi sana, maono yake ni dhahiri alikuwa anajua siku moja yatatimia akiwa hajaifungia macho dunia. 

Lakini Mungu amempenda zaidi, sitaki kuamini kuwa kuna hujuma yoyote, na sitaki kuzungumzia sana jambo hili, niweke koma kwa kusema Mungu ailaze mahali pema peponi roho yake.

Leo niseme tu nimesikiliza pande zote zikinadi sera zao juu ya namna ya kuongoza Taifa iwapo wananchi watatoa ridhaa kwa chama hicho, nimewasikiliza wananchi ambao kwa nyakati tofauti nimeshuhudia jinsi kulivyo na mnyukano wa mawazo na ngumi katika kutetea hoja zao. Nafasi hiyo inawachanganya wapiga kura hasa baada ya kushiba sera mbalimbali za ulainishi kwa wapiga kura. Wapo ambao wamesikia sera ambazo zinawagusa moja kwa moja wenyewe na wanahisi kuna afua baada tu ya kuapishwa rais ambaye watakuwa wamemchagua kwa ajili ya kutatua kero zao.

Najua katika siasa kuna uvumi na ukweli, uvumi utabaki kuwa uvumi na ukweli utabaki kuwa ukweli daima. Wagombea wanatakiwa kuacha uvumi na badala yake waseme ukweli ili ubaki kuwa ukweli hata kama unauma, matarajio ya wapiga kura hayatakuwa na radhi ya uvumi, na uvumi una mwisho wake ambapo mvumishaji atashindwa kukidhi matakwa ya ukweli.

Nimependa uendeshaji wa mikutano ya hadhara kwa kupeana nafasi na vyama vingine, nimependa amani tuliyoitunza katika kipindi hiki kigumu cha kukubaliana kutokukubaliana kiitikadi na kuitumia vizuri demokrasia tuliyonayo, nimependa jinsi ambavyo kila mmoja –  nazungumzia uwezo mdogo wa mshindani wake kwa hoja – hata kama hoja hizo kwa sisi mashabiki tumeziita ni matusi, lakini bora salama.

Nimependa mikutano isiyo rasmi ya wananchi pasi na uwepo wa viongozi wenyewe, kila mmoja akisimamia hoja na mteule wake. Wapo walioshawishika na wapo watakaoendelea kushawishika kila siku na kubadili mawazo na mwisho wa siku watatoa ushindi kwa mgombea mmoja.

Hoja yangu ya msingi leo ni kumtaka atakayechaguliwa kufanya yale aliyoahidi kwa wananchi ambao wengine wamevaa mabomu ya kuweka dhamana ya wagombea wao, ngazi hiyo ya taasisi ya urais ni ngumu na kubwa sana, ahadi zilizotolewa na wagombea wote ni nyingi na kubwa sana, matumaini ya watu ni makubwa sana.

Hoja yangu ni namna kiongozi huyo atakavyojiandalia mikakati thabiti ya kuweza kukidhi haja ya waliomchagua, naamini kwa mawazo yao wameridhika kabisa kuwa wataweza lakini wanasahau kuwa kuna wasaidizi ambao ndiyo watakaowakwamisha katika kutekeleza ilani za vyama vyao, wengi wa wapambe hawa ni wale wenye majina mabaya katika kampeni kwamba ndiyo waliowazunguka na ndiyo vinara wa kukwamisha maendeleo.

Pamoja na kwamba urais ni taasisi, mimi ningeshauri rais ajaye ajenge upya taasisi yake ili iwe nafasi ya kupata lawama za moja kwa moja kwa huyo rais atakayeapishwa mara baada ya kutangazwa, kusiwepo na lawama ya kutotekeleza ahadi kwa sababu za kiutendaji na kushindwa kuchukuliwa hatua stahiki kwa wanaohusika.

Yote mema yaliyozungumzwa nafsi zetu zimemeza na kuamini kuwa sasa kutakuwa na ahueni ya maisha baada ya ahadi zenu nzuri za kututakia maisha mazuri zaidi na kutupa kipato na ajira za kutosha, Tanzania ya mafanikio naiona ipo mbele yetu kama ilani hizo zikifanya kazi ipasavyo.

Ikiwa Magufuli utachaguliwa kumbuka ahadi zako, inawezekana ukashindwa kutimiza kwa asilimia zote kutokana na uwajibikaji wa watu wako, lakini wananchi wataridhika zaidi na kiasi utakachowafanyia, na jinsi utakavyoonesha kuwa umejali ulichoahidi. Hiyo itakusaidia awamu ijayo badala ya kusema nitafanya utasema nimefanya.

Iwapo Lowassa utashinda matarajio ya wapiga kura ni mabadiliko, kuna uwezekano mkubwa wanaokuzunguka wakakwamisha ndoto zako, lakini jitahidi kuwa na watu watakaotimiza ndoto zako ili awamu ijayo watu waseme mabadiliko waliyoyapata na kuweza kukupa tena ridhaa yao.

Nimeamua kusema haya kwa kuwa siku zinayoyoma na watu wanabadilika pasi na maono yenu, kuna mazungumzo mengi nje ya mikutano yenu, kuna uchambuzi mwingi nje ya mikutano yenu, sasa wapiga kura wana uamuzi mpya na siyo wa vyama bali mtu kwa jinsi ninavyowaona, kila kiongozi atatazamwa yeye na siyo taasisi, kila mmoja atapata kikombe chake, bora iwe salama.

Kwangu mimi nikiulizwa sina jibu mpaka sasa, nasikiliza minong’ono inasemaje ili nijue mbichi na mbivu halafu kimyakimya katika chumba cha kupigia kura. Naamini nitakayempa alama ya vema ndiye rais wa Tanzania ya wote.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.