Jumapili hii, Watanzania tupatao milioni 23.7 tunatarajiwa kumiminika vituoni kwa lengo moja tu la kupiga kura kuchagua viongozi bora, watakao tuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Baada ya viongozi waliopo sasa kumaliza muda wao wa uongozi wa miaka mitano iliyopita.

Viongozi  hao tunaowakusudia kuwachagua ni Rais, Wabunge na Madiwani. Hapana shaka tumewasikia kauli zao ndani ya kipindi cha miezi miwili na nusu. Baadhi ya kauli zikiwa na dalili za ukweli na baadhi ya kauli zikiwa na dalili za hadaa. Mpimaji wa kauli hizo mbili ni wewe tu. Hakuna mwengine.

Tutapokwenda kupiga kura tutakuwa tunatekeleza demokrasia. Ukweli tunakwenda kukubaliana kati yetu wapigakura na wapigiwa kura (wagombea) kuhusu mustakabali wa kuendesha maisha yetu na maendeleo ya taifa letu; kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hii ni siku muhimu sana.

Demokrasia ni dhana tu yenye mfumo wa kuendesha Serikali iliyochagukiwa na watu kwa manufaa ya watu. Mfumo huo usiposimamiwa kikamilifu na viongozi na usipokemewa barabara na wanaoongozwa (wananchi) matokeo yake ya uendeshaji maisha huwa ni hasara badala ya faida.

Wewe mpigakura hutakiwi kushabikia mgombea udiwani, ubunge au urais kwa vile ana sura na umbo la mvuto. Ni muumini mwenzio katika madhehebu au dini. Ni kabila moja. Ni swahibu wa kiongozi umpendaye. Ni mhisani wako mkubwa. Ni kipenzi wa watu nakadhalika.

Huo si uamuzi wa kidemokrasia na wala si uwamuzi wa kibusara. Ni  uwamuzi wa kijinga na wakukuangamiza katika mustakabali wa maisha yako na maendeleo  ya taifa lako kwa miaka mitano ijayo. Jipime kwanza kabla ya kumchagua kiongozi bora na utambue nini maana ya kuwa na kiongozi bora.

Jumapili ikifika na Mwenyezi Mungu amekujalia pumzi, afya njema na busara kamchague mgombea mwenye kauli ya ukweli na vitendo vyake ni majibu ya kweli ya kauli zake. Mpenda haki, mchukia dhuluma ndani ya roho yake, kinywani mwake na hadi kwenye sura yake. Na wewe uwe na jibu la kweli, ndiyo huyu ni kiongozi bora.

Miongoni mwa wagombea wamo wenye kasoro na wamo wenye timilifu za sifa za uongozi. Daima tambua kuwa wote hao wanapenda uongozi iwe kwa maslahi yao au kwa maskahi ya taifa. Ndiyo maana mwananchi mwelevu huchagua kiongozi bora kwa maana ya kiongozi mkweli na muaminifu.

Kwa sisi wanafasihi  tunasema kiongozi bora ni yule asiye mnafiki. Mnafiki ni mtu anayesema kinyume cha anavyotenda; mtu anayetoa ahadi kisha asitimize; mzandiki. Mzandiki ni mdanganyifu na mwongo. Mtu kama huyo daima hukwepa kujibu hoja za msingi pindi  zinapomkabili mbele ya watu.

Ndani ya miezi miwili  na nusu hii ya kampeni, sura zote hizo nilizozitaja zimejichomoza bila shida yo yote mbele ya wananchi. Baadhi ya wagombea na wapambe wao pamoja na viongozi wa vyama vya siasa wamejidhihirisha udhaifu na ubora wa kauli zao. Kazi iko kwako wewe utakaye mchagua mgombea safi kuwa kiongozi wetu.

Ukweli, baada ya uchaguzi nitasikitika na kuhuzunika kusikia baadhi ya watu wakilalama na kusingizia eti aliyemchagua hakuwa chaguo lake!! Eti alishawishiwa au alirubuniwa na rafiki, ndugu, kiongozi au mpambe wa mgombea. Huo ni ushetani.

Binafsi naamini shetani au ibilisi wa mtu ni mtu mwenyewe. Inawezekana hata wewe una amini hivyo! Kama hivyo ndivyo; siamini iwapo ni kweli binadamu hakukamilika. Hii maana yake ni nini?  Ni kumtia dosari Muumba? Hapana. Hapana hata kidogo. Muumba-mwenyezi Mungu hana dosari katika uumbaji wake viumbe. Ndiyo maana tutamwita Mtukufu.

Dosari alizonazo binadamu ni tamaa ya kumkaribisha na kumkumbatia shetani katika matendo yake ya maasi kwa Mwenyezi Mungu. Shetani hupenda mambo maovu. Dhuluma, wizi, ulevi, uzinzi, uwongo na mengineyo ya aina hiyo. Mathalani, kumtetea muovu ni ushetani!! Kukimbia nyumba yako ni ushetani!! Kumfuata mlevi ni ushetani!!  Kutoa na kupokea rushwa ni ushetani!!

Kwa hiyo, Oktoba 25, mwaka huu ni siku muhimu sana sana kwa Watanzania, kwa sababu tutafunga mkataba na kupitisha mageuzi tuliyoyapa jina la MABADILIKO. Tunahitaji mabadiliko ya kweli.. Hatuhitaji mabadiliko tu.

Mabadiliko ya kweli yanaanzia kwako. Kwa sababu wewe ndiye muhusika wa maisha na maendeleo yako. Ukichezea kura yako ukadhani ni mchezo wa karata kuwa na dume “ukaoa” seti na ukatamba UMEOA ili hali hujaoa ni upuuzi mtupu. Epuka hilo.

Nakushauri usidharau hata chembe kuzama ndani ya lindi la maisha lenye theluthi tatu ya maisha ya kila siku ya kiumbe mtu. Alikotoka, Alipo na Aendako. Pima theluthi mbili za mwanzo kwa makini upate jibu la kukuangazia huko unakotaka kwenda kwa faida au hasara yako.

Je, ulikotoka hali ilikuwaje? Je, ulipo hali ikoje? Iwapo mizania inaonesha mambo mengi ni mafanikio au si mafanikio, bado unahitaji mabadiliko kulingana na tathimini yako. Hapo ndipo dhana mabadiliko inapotakiwa kufanyiwakazi. Kinyume cha hivyo ni upuuzi.

Nawatakia kila la heri Watanzania kuchagua viongozi bora waliojaa sifa za uongozi. Namuomba Mwenyezi Mungu atubariki na atujalie hekima na busara wakati wa kupiga kura zetu. Nyoyo zetu zitawaliwe na utulivu, upendo, umoja na amani. MUNGU IBARIKI TANZANIA.