Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imebainisha kuwa maelfu ya namba za simu zilizojihusisha na wizi, utapeli na ulaghai kupitia Mtandao wa simu zimefungwa.
Akizungumza jijini Dodoma hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt Jabiri Bakari, amesema kuwa jumla ya namba tambulishi 52,087 zikiwemo zilizoripotiwa kupotea, kuibiwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu zimezuiliwa kupokea na kutoa huduma za Mawasiliano.
“Kwa mfano, Kuanzia Julai 2021 hadi kufikia Septemba 2022 jumla ya namba tambulishi (IMEI) zilizofungiwa na mfumo huu ni 52,087 ambazo ziliripotiwa kupotea, kuibiwa au kuhusika katika matukio ya kihalifu, hivyo kuwezesha kupunguza matukio ya wizi na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya Mawasiliano vyenye ubora kwenye soko,” amesisitiza Dkt. Bakari.
Ameeleza kuwa, kupitia kanzidata ya Namba Tambulishi (Central Equipment Identity Register), moduli hiyo imewezesha uhakiki wa vifaa vyote vinavyounganishwa na mitandao ya watoa huduma kama vinakidhi viwango vya kimataifa na ni salama kwa watumiaji.
Moduli hiyo iliyopo katika Mfumo wa Usimamizi wa Mawasiliano (TTMS), imewezesha kuzuia matumizi ya simu zilizoripotiwa kuibiwa, kupotea au kuharibika pamoja na kuzuia matumizi ya simu zisizokuwa na viwango.
“Usimamizi huu unawezesha kubaini na kufungia namba tambulishi za vifaa vya Mawasiliano zilizonakiliwa (Duplicate IMEIs), namba tambulishi za vifaa vilivyotumika kwenye udanganyifu pamoja na namba tambulishi zilizotolewa taarifa ya kupotea au kuibiwa,” ameongeza.
Mamlaka hiyo awali ilieleza kuwa watumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu mara wanapobaini kupokea simu au ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) wenye viashiria vya utapeli wanapaswa kutoa taarifa kwa kutuma ujumbe mfupi wenye neno “utapeli” kwenda namba 15040 na kutuma namba ya tapeli kwenda namba hiyohiyo.
Aidha TCRA ilisisitiza kila mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ahakikishe anahakiki namba zake za simu zilizosajiliwa kwa njia ya kibayometria, kwa kutumia namba ya kitambulisho cha Taifa wanapaswa kubofya *106 kisha kufuata maelekezo. Hatua ambazo Mamlaka hiyo ilieleza zinasaidia kupunguza utapeli kwa njia ya simu.