Katika gazeti moja la kila wiki, toleo la wiki iliyopita, mwandishi mmoja mahiri, Lula wa Ndali Mwananzela, ambaye huwa namchukulia kama mtu mwenye maono ya mbali, kaamua kujichanganya na kuniondolea kile nilichokuwa nacho kwa muda mrefu kuhusu mtazamo wake. Kafanya kitu cha ajabu ambacho ni kama kinaonesha kuwa upeo wake umeanza kufifia!
Katika toleo hilo lililopita, mwandishi huyo alitoka na makala iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka ‘Kosa kubwa la Chadema ni kuwanyima Watanzania uchaguzi’!
Mwandishi huyo anadai kwamba kitendo cha Edward Lowassa kuihama CCM na kujiunga na Ukawa kupitia Chadema, ambako ameteuliwa kuwa mgombea urais, kimewanyima Watanzania fursa ya kufanya uchaguzi wa mabadiliko.
Kabla sijakwenda mbali, niseme kwamba mwandishi huyo anazichukua chuki zake binafsi na kutaka kuzisambaza kwa Watanzania wote ili zigeuke kuwa sera ya nchi.
Hilo ni jambo linalotakiwa kuepukwa na kila mwananchi kuliko hata tunavyojiepusha na ugonjwa wa ebola. Kuzidandia chuki binafsi za mtu bila kujua zilikoanzia ni kutaka kuliangamiza Taifa kuliko ebola inavyoweza kufanya.
Ieleweke kwamba Lowassa ni binadamu, kuna wanaompenda na wanaomchukia kutokana na sababu mbalimbali za kimaisha, ila si vyema sababu hizo zikageuzwa kuwa za watu wote. Anayemchukia Lowassa ni kivyake, asilazimike kuwarubuni wengine kumuona Lowassa namna anavyomuona yeye binafsi.
Kwa nini nasema hivyo? Ni kwamba madai yanayotolewa ya kuwa Lowassa hawezi kutoka CCM na kuleta mabadiliko kwenye nchi kupitia upinzani yanadhihirisha ufupi wa fikra.
Sababu mabadiliko ya nchi yetu tunatarajia yaletwe na Watanzania wenyewe, sidhani kama tuna imani ya kwamba mabadiliko yetu yataletwa na mtu wa nje ya nchi yetu.
Kinachogomba katika mabadiliko tunayoyataka ni mfumo ambao kila mmoja anataka autumie kuyafikia mabadiliko. Mfumo unapogoma ujanja wa mabadiliko unakuwa umepotea.
Kwa hiyo, mtu kutoka kwenye mfumo usiolenga kwenye mabadiliko na kuingia kwenye mfumo wa mabadiliko ndani ya nchi si kitu cha kukishangaa, maana mtu anakuwa hajabadili uraia. Ni wazi kwamba Lowassa, kama Mtanzania, asingeweza kuleta mabadiliko akiwa ndani ya chama kilekile kisichoyapenda mabadiliko.
Niliwahi kuongea naye kuhusu jambo hilo akiwa bado ni mwana CCM, nikimwambia kuwa mabadiliko ndani ya CCM ni muhali, yeye akasema ngoja ajaribu, na katika kujaribu kwake niliyomwambia ndiyo yaliyojiri baadaye.
Na hakuna awezaye kufanya mabadiliko katika nchi hii kwa wote waliobaki ndani ya chama hicho, isipokuwa wale waliotoka nje ya chama hicho. Sababu kutoka nje ya CCM tu ni mabadiliko ya kwanza yaliyo makubwa yanayoashiria mabadiliko mengine kinchi.
Kama nilivyosema awali, mabadiliko tunayoyatamani nchini mwetu sidhani kama tunayatarajia yaletwe na mtu kutoka nje ya nchi, ni lazima yaletwe na mtu aliye Mtanzania.
Lowassa ni Mtanzania, mawazo ya kwamba katokea CCM hayamgeuzi kuwa Mrundi, Mnyarwanda wala Mkenya. Kibaya kwake ni ule mfumo aliokuwa akiutumia, basi. Kitendo cha kuachana na mfumo huo kinamfanya awe mtu mpya lakini akiwa bado ameushikilia uraia wake.
Ajabu, Lula wa Ndali anadai kwamba mtu ambaye angeleta mabadiliko ya kweli katika upinzani ni Dk. Willibrod Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema na baadaye kugeuka muasi wa kutaka kukizika chama hicho baada ya kuona matarajio yake binafsi ndani ya Chadema yanatetereka kufuatia ujio wa Lowassa ndani ya chama hicho.
Nimtazame kidogo Dk. Slaa ili tuone kama upatu wa Lula wa Ndali uko sahihi. Nashindwa kuelewa ni kwa nini mwandishi huyo anashindwa kuona kwamba njia aliyoitumia Slaa kuingia Chadema na baadaye kuwa mpinzani wakweli ndiyo aliyoitumia Lowassa hatua kwa hatua.
Dk. Slaa, kama alivyokuwa Lowassa, alikuwa kada kindakindaki wa CCM akitamani kugombea ubunge wa Jimbo la Karatu mwaka 1995 kwa tiketi ya chama chake. Tofauti pekee kati yao ni kwamba wakati Slaa alitamani ubunge Lowassa aliutamani urais.
Lakini kutokana na Dk. Slaa kutokidhi vigezo vya chama hicho kwa sababu zilizo wazi, jina lake likakatwa na yeye kuamua kukimbilia Chadema. Wananchi wa Karatu waliochoshwa na mizengwe ndani ya CCM wakamuunga mkono Dk. Slaa akashinda ubunge kwa tiketi ya Chadema.
Lakini hata hivyo, kilichoonekana kwa CCM mpaka kulazimika kulikata jina la Dk. Slaa, kimeendelea kumuandama mpaka kwenye chama chake cha Chadema alichokitumikia kwa juhudi na maarifa hadi kuonekana ni mpinzani wa kweli.
Ikumbukwe kwamba Dk. Slaa ni muasi mzoefu. Laana hiyo ilimpata tangu alipouasi utumishi wa Mungu – upadri. Ieleweke kwamba wengi wanaouasi utumishi huo mara nyingi hawabaki salama. Nadhani CCM walilitafakari hilo ndipo wakaamua wamuweke Slaa pembeni. Chadema nao wameishapata fundisho sasa.
Ninachotaka kusema kwa Lula wa Ndali ni kwamba kama Dk. Slaa alihama CCM na kuingia Chadema bila kuwanyima uchaguzi wana Karatu, waliomchagua na yeye kuwafanyia mengi makubwa ambayo yalikuwa hayajafanywa na mbunge yeyote wa CCM, kwa nini Watanzania waonekane wamenyimwa uchaguzi kwa kuletewa Lowassa? Kwa nini tusifikirie kwamba naye anaweza kufanya mengi makubwa kwa nchi hii kama ilivyokuwa kwa Slaa kule Karatu?
Baada ya kuyaangalia hayo ya Slaa tunawezaje kuwa na wasiwasi juu ya Lowassa kwamba kuondoka kwake CCM kunaweza kumfanya abaki na shombo la CCM linaloweza kumfanya ajikute anayafanya ya chama chake hicho cha zamani?
Ikumbukwe Lowassa hajawahi kuwa muasi hata mara moja, tofauti na alivyokuwa Dk. Slaa. Kwa mantiki hiyo nawashukuru sana viongozi wa Chadema kwa kuuona na kuutambua ukweli huo, ambao bahati mbaya unawashinda kuuona baadhi ya wananchi, akiwamo Lula wa Ndali, juu ya kasisi huyo mwenye tabia ya uasi.
Hebu fikiria kama Dk. Slaa angeweza kuingia Ikulu halafu tukasikia mke wake, “1st lady”, amemtupia rais nguo zake nje na kumlazimisha kulala kwenye gari akidai kwamba Ikulu ni mali yake, ni kitu gani kingetupata kama Watanzania? Si ni majanga matupu? Au kama Slaa angeamua kuiasi Ikulu kwa kuburuzwa na mkewe tungefanyaje?
Imeelezwa kwamba mke wa Dk. Slaa alishaanza maandalizi ya biashara ambayo angeifanya kama mke wa rais akiwa Ikulu, kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa kimataifa, kwa maana ya kwamba alishaanza maandalizi ya kuigeuza Ikulu yetu, sehemu takatifu, kuwa pango la wanyang’anyi!
Katika hilo hatuna budi kumshukuru Mungu kuwa afadhali katupishia mbali aibu hiyo iliyokuwa inatunyemelea kwa kusukumwa na laana ya uasi iliyomfunika padri huyo wa zamani. Kweli Mungu mkubwa. Ingefaa Lula wa Ndali akatueleze ni vipi Chadema imewanyima Watanzania uchaguzi.
0784 989 512