Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

MKUU wa Mkoa Rukwa Queen Sendiga ameagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za serikali za mitaa kuchukua hatua za kuwarejesha watendaji na watumishi wa serikali wanaotuhumiwa kuharibu miradi ya wananchi ili wajibu tuhuma zao.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Kabwe wilaya ya Nkasi ambapo walilalamika kuwa Mtendaji amehamishwa baada ya kuharibu mradi wa zahanati.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akikagua bandari ya Kabwe jana alipofanya ziara wilayani Nkasi kuangalia miradi ya sekata ya afya.Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijualikali na wa kwanza kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Theopista Mallya.

Mkuu wa Mkoa huyo alitembelea zahanati ya kijiji cha Kabwe na kujionea hali ya kukwama kwa ujenzi wa jengo la mama na mtoto ambalo linadaiwa kupatiwa vifaa vya mabati na saruji toka kwa wafadhili mwaka 202o lakini halijakamilika.

“Mtendaji wa Kata aliyekuwa hapa arejeshwe kuja kutoa majawabu ya tuhuma za kutokamilika zahanati ya kijiji cha Kabwe wakati vifaa vya ujenzi vilitolewa na wafadhili” alisema Sendiga.

Katika hatua nyingine Sendiga ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza mradi wa ujenzi wa zahanati hiyo na kwa wahusika watakaobainika hatua za kisheria zichukuliwe haraka.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Kabwe wilaya ya Nkasi wakifuatilia mkutano ulihutubiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (hayupo pichani ) ambapo aliwahakikishia kuwa seerikali itatekeleza miradi yote kwa ufanisi .

Kwa upande wake Diwani Kata ya Kabwe Asante Lubisa alikiri kupokelewa kwa vifaa vya ujenzi wa zahanati hiyo toka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mwaka 2020 lakini kutokana na ramani iliyopangwa kubadilika mradi umeshindwa kukamilika hadi sasa.

Mkuu wa Mkoa huyo akiwa wilayani ya Nkasi alikagua kituo cha Afya Kasu, Hospitali ya Wilaya, ujenzi wa madarasa sekondari ya Kabwe na bandari ya Kabwe ambapo alisema hatokubali kuona miradi ikisua sua.