Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) linajenga Kituo cha Michezo katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam; huku likisema lengo kuu ni kuhakikisha Tanzania inashiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau, anasema dhamira kuu ya ujenzi wa kituo hicho ni kuibua vipaji vya vijana katika mchezo wa soka ili baadaye waweze kuuzwa katika ligi kubwa mbalimbali duniani.
Katika mahojiano na JAMHURI yaliyohusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne kwa NSSF, Dk. Dau anasema soka ni mchezo wenye utajiri mkubwa, hivyo wao kama Shirika, pamoja na kuwasaidia vijana, wamelenga zaidi kuona NSSF inapata faida kutokana na uwekezaji huo.
“Kwanza wanachama na wananchi kwa ujumla waelewe kuwa kila uwekezaji tunaofanya, lengo ni kwamba lazima tupate faida.
“Hatufanyi kama charity, kwa hiyo hata hili la Kituo cha Michezo, lengo la awali lilikuja kwamba tutafute njia mbalimbali za kuboresha mapato yetu ili kuboresha mafao kwa wanachama.
“Sasa mpira wa miguu ni biashara kubwa sana, na mimi nawaambia watu unfortunately nchi hii kwenye mpira-viongozi wa michezo watanisamehe, lakini haya ni maoni yangu. “Zamani, kwa kumbukumbu zangu wachezaji mpira walikuwa wanacheza kama starehe. Wengine wanacheza mpira kama ni mapenzi. Mtu anasema ‘mimi ni Yanga, baba yangu Yanga au baba yangu Simba, mimi ni Simba au Cosmo wakati ule.’
“Anacheza mpira huko mchangani nia yake akacheze Yanga, Simba, Cosmo na kadhalika. Anacheza kwa mapenzi, hobby kila mmoja ana kazi yake.
“Watakuja Jangwani pale jioni wanafanya mazoezi, anapachika begi lake, safari nyumbani. Kesho asubuhi yuko kazini. Akitoka kazini saa 9; saa 10 au 11 yuko Jangwani mazoezini. Ana kazi analipwa mshahara, lakini kadri muda unavyokwenda mpira umebadilika.
“Huku kwetu mpira sasa hivi si hobby, si mapenzi na ndiyo maana zamani kumpata mchezaji wa klabu moja kuacha kwenda klabu nyingine si rahisi kwa sababu yule yuko katika klabu ile kwa mapenzi. Mimi nakumbuka kipindi kile cha miaka ya 1960, 1970 unawahesabu Emanuel Albert, Gilbert Mahinya…Emanuel Albert alitoka Yanga akaenda Simba. Gilbert Mahinya akatoka Simba wakati ule Sunderland akaja Yanga.
“Marehemu Adam Juma akatoka Sunderland akaja Yanga. Unawahesabu. Si rahisi mchezaji wa katika klabu moja akaenda nyingine kwa sababu anacheza kwa mapenzi.
Sasa hivi mpira ni kazi. Bahati mbaya sana, kwa upande wa uchezaji tumeubadilisha tumeenda kwenye mpira wa kulipwa. Leo kuna mshahara, kuna mikataba. Mkataba ukiisha mnajadiliana mkataba mpya.
“Leo mchezaji wa Yanga kwenda Simba ni jambo la kawaida; au mchezaji yule yule anaweza akaenda Yanga baadaye akarudi Simba. Akatoka Simba akaenda Yanga akarudi Simba. Akatoka Yanga akaenda Simba akarudi Yanga. Tumeona kina Ivo (Ivo Mapunda), tumeona kina Bartez, tumeona kina Juma Kaseja na wengine wengi.
“Anakwenda klabu pinzani baadaye anarudi kwenye klabu yake ya zamani. Zamani yale huwezi kufanya. Kwa hiyo sasa hivi kiuchezaji tayari professionalism imeingia, siyo mapenzi ya klabu.
“Mchezaji anakwenda pale kama ofisini. Kazi imekwisha, mkataba umekwisha anamsikiliza mwajiri wake anasemaje. Akipata mwajiri mwingine-ikitokea timu pinzani anakwenda; na akienda kule anacheza kweli kweli.
“Huo ni kwa upande wa wachezaji, lakini kwenye upande wa menejimenti naomba waniwie radhi-bado tunameneji vilabu vyetu hivi kwa utaratibu wa zamani- amateur (ridhaa) kana kwamba bado tunagemea wachezaji wetu wana mapenzi na timu. Haiwezekani, hii ni kazi.
“Na sisi kwenye upande wa menejimenti na katika kuuandaa mchezo wenyewe wa mpira, lazima sasa tuutazame katika mtazamo wa kibiashara zaidi kuliko ki-hobby.
“Viongozi leo-akichaguliwa kiongozi wa klabu kubwa kwa mfano Yanga, lengo lake la kwanza ni kuifunga Simba. Kiongozi akichaguliwa Mwenyekiti wa Simba, kitu chake cha kwanza ligi inakuja lazima aifunge Yanga…lazima niwe bingwa; sasa muda wa kusema aanze kulea vipaji, hana.
“Kwa sababu leo nikichukua wachezaji chipukizi wa miaka 16 au miaka 17 ndiyo nikaanza kuwatumia wale, nitafungwa na mimi muda sina, nikifungwa kesho uchaguzi. Wanachama wanadai uchaguzi, wananifukuza. Hili ni tatizo.
“Sasa sisi tukaona hapana. Mpira kuna hela, lakini sasa tuuendee kisayansi kama ambavyo mchezo wenyewe unavyotaka. Kwa kuwa mchezo wenyewe umeshaingia kwenye ki-professionalism na menejimenti yake, maandalizi yake yote tuyaweke kibiashara zaidi.
“Ndiyo chimbuko la kuanzisha Kituo cha Michezo. Lengo ni kwamba tuchukue vijana kuanzia miaka 13 mpaka 14. Tunawalea. Akifika miaka 16 au miaka 17 anatafutiwa timu nje, anauzwa. Faida inayopatikana tunarudisha hela zetu na faida juu yake na pia kuendeleza kile Kituo. Faida ya kwanza ndiyo hiyo. Tutapata hela, tutaboresha mafao.
“Faida ya pili; mpira Tanzania utakua kwa sababu hawa wakienda kucheza mpira wa kulipwa (professional football) kila mwaka ikiundwa timu ya Taifa wakiitwa wachezaji, wale wataitwa. Tunaona akina Samatta na akina Ulimwengu na akina Kazimoto. Wataitwa tu. Wanapoitwa wale wataunda timu ya Taifa, matokeo yake timu yetu ya Taifa nayo itakuwa nzuri,” anasema Dk. Dau.
Matunda ya Kituo
Dk. Dau anasema malengo ya NSSF ni kuhakikisha Tanzania inashiriki Kombe la Dunia.
“Hii michuano inayokuja ya mwaka 2018 ya Urusi hii hatuwezi. Ile ya Qatar ya mwaka 2022 ni borderline (nusu kwa nusu), lakini ile inayofuata ya 2026 ile ni achievable. Hiyo ndiyo tumelenga. Ya mwaka 2022 tutajaribu, lakini ya mwaka 2026 is almost definitely, lazima twende Fainali za Kombe la Dunia.
“Kwenye Kituo wachezaji wakishapokewa, wanafundishwa mpira na wakati huo tutakuwa tunawasomesha shule kwa sababu mpira ni mchezo, ikitokea bahati mbaya akavunjika mguu akawa mlemavu maisha, hawezi kuendelea kucheza.
“Kama hukumpa masomo -hawa vijana wa darasa la saba au kidato cha kwanza kama hukumwendeleza kwenye taaluma ya masomo, bahati mbaya akaumia hawezi tena kucheza, umemharibia maisha.
“Au akacheza lakini bahati mbaya mchezo wake haukuendelea sana, hakupata timu ya kumuuza, umempotezea maisha yake. Kwa hiyo tutakuwa tunawafundisha mpira, lakini pia tunawasomesha.
“Wenye uwezo wa kusoma shule-wenye uwezo mzuri wataendelea mpaka kidato cha sita huko mpaka vyuo vikuu. Wale ambao uwezo wao siyo mzuri sana shuleni tutawafundisha ufundi stadi ili ifike mahali kama atafanikiwa kwenye mpira atakwenda kucheza, la amefeli kwenye mpira, akiondoka kwenye Kituo awe fundi seremala, fundi wa umeme, fundi wa kompyuta, fundi wa magari, fundi rangi na kadhalika,” anasema.
Dk. Dau anasema wamelenga zaidi kuwauza wachezaji katika soko le nje, lakini endapo soko la ndani watakaowahitaji watakuwa na fedha, hawatasita kuwauzia.
“Soko la nje ndiyo lengo letu kuu, lakini vilabu vya ndani kama itatokea wakitupa bei ambayo inafanana na hadhi ya mchezaji- sisi haja yetu ni hela ili uwekezaji ule uweze kurudi.
“Pengine kwa sababu huenda viwango vyao havitakuwa vikubwa sana wakakosa timu nje, akipata timu ya ndani Yanga au Simba au Azam au timu yoyote tukisema mchezaji huyu thamani yake ni dola 500,000; wakitupatia dola 500,000 tutamuuza. Tukisema huyu ni dola 1,000,000 Azam wakisema sisi tutakupeni, tutamuuza,” anasema.
Kwanini iwe kwenye soka tu? Dk. Dau anajibu swali hilo kwa kusema: “Soka ndiyo mchezo ambao unalipa. Sisi tunaangalia zaidi mapato. Tatizo la riadha wachezaji wa riadha hawauzwi. Huwezi ukamuuza. Tukiwezeka kwenye riadha, hela zetu zinarudi vipi?”