Baada ya kilio cha muda mrefu kuhusu kulipwa ujira unaoendana na mazingira magumu ya kazi zao, hatimaye Serikali imetimiza kile kilichokuwa kikipigiwa kelele na wabunge kuhusu kuwalipa askari polisi posho ya kujikimu, JAMHURI imebaini.

Askari wa jeshi hilo, mwishoni wa wiki iliyopita, walisherehekea wikiendi yao vizuri baada ya Serikali kuwajaza posho ya kujikimu maradufu katika miamala yao.

Vyanzo vya uhakika kutoa ndani ya jeshi hilo, vimedokeza kwamba posho hiyo ambayo ilitakiwa kulipwa kwa askari polisi hao tangu Julai, mwaka huu, sasa imelipwa Oktoba – siku chache kabla ya Taifa kumpata rais wa awamu ya tano.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, askari polisi hao wameingiziwa posho hizo za kujikimu kabla ya Oktoba 10, jambo ambalo ni nadra kutokea katika miezi yote wanayoifanyia kazi.

Askari polisi hao hivi sasa wameanza kulipwa rasmi posho ya Sh 300,000 kutoka Sh 180,000 waliyokuwa wakilipwa miezi ya nyuma, hatua ambayo imewafanya wengi wao kujiuliza maswali mengi kwamba kwa nini walipwe hivi sasa wakati walitakiwa kulipwa tangu Julai mwaka huu.

“Mwezi huu (Oktoba) tumeingiziwa posho ya Sh 300,000 kutoka Sh 180,000… usifanye mchezo na Serikali kwani inajua kula na kipofu sana, wameona vuguvugu la uchaguzi limepamba moto ndiyo maana wameamua kutufurahisha ili tusimamie vizuri uchaguzi.

“Mimi binafsi nilikwenda benki tarehe 9 nikakuta mambo mazuri kabisa, kwani badala ya kuona kiwango cha zamani ambacho nilikuwa nikikitarajia niliona tofauti kabisa, nilipowauliza wenzangu nao walinijulisha kwamba nao wameona neema hiyo,” kimesikika chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya jeshi hilo.

JAMHURI ilipodadisi kwa askari polisi kadhaa kuhusu hatua hiyo, wamesikika wakieleza kwamba hiyo ni danganya toto kutokana na hali halisi ilivyo, ikizingatiwa kwamba hivi sasa nchi imebakiza siku chache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani ambao kwa mwaka huu unaonesha kushika kasi ya ajabu.

Hata hivyo, habari zaidi zinaeleza kwamba hatua ya Serikali kuwapandishia posho askari polisi hao inatokana na ukweli kwamba hivi sasa askari hao wamechoka na utawala wa Serikali ya chama tawala cha CCM kutokana na kupewa ahadi zisizotekelezeka, badala yake wamepanga kufanya mabadiliko kwa kuwa upande wa upinzani kwa siri kubwa.

Jingine lililowafanya askari polisi hao kutenda ndivyo sivyo katika kazi zao, ni hatua ya wenzao wanaofanya kazi katika majeshi mengine mfano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kulipwa posho nono tofauti na wao, hali ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa. 

Mara kwa mara wakati wa mikutano mbalimbali ya Bunge, hasa la Bajeti, wabunge wengi bila kujali itikadi za vyama vyao wamekuwa wakiipigia kelele Serikali kuwaongezea posho na mishahara askari polisi hao ambao wameelezwa kufanya kazi katika mazingira magumu, hali ambayo imewafanya baadhi yao kujikuta wakijiingiza katika vitendo vya kudai na kupokea rushwa.

Wakati askari polisi wakila vizuri wikiendi na familia zao, Serikali imewatangazia pia neema walimu baada ya siku chache zilizopita kueleza kwamba itaanza kuwalipa malimbikizo ya mishahara kuanzia jana (Oktoba 12).

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hab Mkwizu, amethibitisha kuanza kulipwa kwa walimu hao alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo, malimbikizo ambayo walimu hao wataanza kulipwa ni yale ya kuanzia Agosti 2013 hadi Agosti 2015. Amesema kupitia rejesta ya madeni ya watumishi wa halmashauri zote inayoratibiwa na TAMISEMI, taarifa inaonesha kwamba mpaka sasa walimu 60,322 wanaidai Serikali Sh bilioni 29.8 na kati ya hizo Sh. bilioni 21.0 ni madai ya walimu 44,715 wa shule za msingi na Sh, bilioni 8.6 ni ya walimu 15,607 wa sekondari.

Katibu mkuu huyo ameeleza kwamba madai hayo yameshawalishwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kwa ajili ya uhakiki tayari kwa kuanza kulipwa kwa kutumwa kwenye halmashauri husika.

Akizungumzia maslahi mengine ya walimu, amesema kwamba Serikali ina taarifa kuwa wapo baadhi yao waliopandishwa madaraja mwaka 2014/2015 na hawajarekebishiwa ngazi za mishahara na kupewa barua za vyeo vyao vipya.

Mkwizu ameeleza kwamba tayari ameshatoa maelekezo kwa waajiri wote kuhakikisha wanawapatia walimu barua zao za vyeo vipya na kurekebishiwa mishahara kabla ya Desemba 2 mwaka huu.

Pia amewaagiza makatibu wa TSD katika kila halmashauri kuhakikisha wanafanya vikao vya kuwapandisha madaraja walimu waliokaa kwenye cheo kimoja kwa muda mrefu na wale waliokaribia kustaafu watapewa kipaumbele wakati wa upandishaji vyeo.

Sambamba na hilo ametoa rai kwa waajiri ambao hawajatekeleza kikamilifu muundo mpya wa kuwapanga watumishi kwa kuzingatia vyeo vipya, wafanye hivyo haraka na kutoa vipaumbele vya kuwapandisha madaraja walimu 41,000 waliokuwa wamegota katika muundo wa zamani.